Na. Hilary Lorry & Winifrida Kisamo– Mahakama, Lindi
Watumishi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Lindi, tarehe 11
Machi 2026 wamefanya kikao kazi na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Lindi,
Mhe. Elia
Joseph Mrema ambaye amesema Mahakama Kuu Kanda hiyo inayotarajiwa kuanza
kutoa huduma za Mahakama Kuu kwa wananchi hivi karibuni kuanzia sasa.
Kikao hicho kimefanyika
katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya kuanza kwa shughuli za Mahakama Kuu Kanda ya Lindi.
Akizungumza wakati
wa kikao hicho, Mtendaji wa Mahakama Lindi Bi. Quip Godfrey Mbeyela
aliwapongeza watumishi wa Mahakama hizo kwa uwajibikaji wao na
uchapakazi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Alieleza kuwa
watumishi hao wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa bidii na kila mmoja
anatambua wajibu wake katika kuhakikisha huduma za kimahakama zinatolewa kwa
ufanisi.
Aidha,
Mtendaji huyo aliwasisitiza watumishi kuendelea kudumisha usafi wa mazingira
katika majengo ya Mahakama pamoja na kuyatunza ipasavyo, akibainisha kuwa
mazingira safi na yakitunzwa vizuri huchangia kuongeza ufanisi katika utendaji
kazi na kutoa taswira nzuri kwa wananchi wanaofika kupata huduma.
Kwa upande
wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Mhe.Consolata Peter
Singano alisisitiza umuhimu wa utunzaji wa vifaa vya Ofisi pamoja na matumizi
sahihi ya rasilimali za Ofisi.
Alieleza
kuwa, utunzaji mzuri wa vifaa hivyo utasaidia kuvifanya vitumike kwa muda
mrefu, hivyo kuvifanya viweze kutumika kwa mahitaji ya sasa na ya baadaye. Pia
alibainisha kuwa matumizi sahihi ya rasilimali za Ofisi yatasaidia kupunguza
gharama zisizo za lazima katika uendeshaji wa shughuli za Mahakama.
Kwa upande
wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Lindi Mhe. Elia Joseph Mrema aliwashukuru
watumishi kwa ushirikiano waliyompatia tangu alipowasili katika Kituo hicho. Vilevile
aliahidi kutoa ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa majukumu ya Mahakama.
Mhe. Mrema
aliongeza kuwa, kwa mara ya kwanza katika Mkoa wa Lindi tunaenda kuwa na
Mahakama Kuu hivyo basi yatupasa kufanya maandalizi muhimu pamoja na kujianda
kwa ujio wa Jaji Mfawidhi, “Sisi
tupo kwenye kufanya maandalizi muhimu pamoja na kujiandaa kwa ujio wa Jaji Mfawidhi ” alisisitiza
Mhe. Mrema.
Aidha,
aliwapongeza watumishi wa Mahakama Kanda ya Lindi kwa kazi nzuri wanayoifanya,
akieleza kuwa tangu alipowasili mkoani humo na kutembelea baadhi ya ofisi, ikiwemo
ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Kamada wa
Polisi Mkoa, Takukuru, Ofisi ya Uhamiaji, Ofisi ya Mawakili wa kujitegemea(TLS)
na wadau wengine hakupokea malalamiko
yoyote kuhusu utendaji wa watumishi.
Mhe. Mrema alisema
hali hiyo inaonesha kiwango kizuri cha uwajibikaji na nidhamu ya kazi miongoni
mwa watumishi wa Mahakama katika Kanda hiyo hivyo aliwataka watumishi kuendeleza
juhudi hizo na ikiwezekana kufanya vizuri zaidi.
Naibu
Msajili pia alisisitiza umuhimu wa kudumisha upendo, kuaminiana na kuheshimiana
miongoni mwa watumishi pamoja na viongozi, huku akisisitiza kuwa kufanya kazi
kwa ushirikiano na kuheshimu mipaka ya majukumu ya kila mmoja ni msingi muhimu
wa mafanikio katika utendaji wa taasisi, “Tufanye kazi kwa ushirikiano huku tukiheshimu
mipaka na tuhakikishe Lindi inakuwa ya mfano” Alisisitiza Mhe. Mrema.
Vilevile,
aliwataka watumishi kuwa wabunifu na kuchapa kazi kwa bidii na kwa kuzingatia misingi ya uadilifu,
uwajibikaji na weledi katika kutekeleza majukumu yao, hivyo kuimarisha ufanisi
wa kazi na utoaji huduma bora kwa wananchi mapema ipasavyo.
Kikao hicho
ni sehemu ya maandalizi muhimu kuelekea kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama
Kuu Kanda ya Lindi, inayotarajiwa kuanzishwa hivi karibuni, hatua inayotarajiwa
kuimarisha upatikanaji wa huduma za utoaji haki kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi
na maeneo ya jirani.
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Lindi Mhe. Elia Joseph Mrema akizungumza na
watumishi wa Mahakama Lindi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Mhe.Consolata Peter Singano (aliyesimama) akitoa neno la utambulisho.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi. Quip Godfrey Mbeyela (aliyesimama) akitoa neno la ukaribisho.
Afisa Hesabu Mkuu Mahakama ya Wilaya ya Lindi Bw. Lucas M. Kadossa akitoa neno la shukurani kwa niaba ya watumishi.
Waandishi
Waendesha Ofisi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi wakitekeleza jukumu lao la
uchukuaji wa Muhtsari katika kikao hicho.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


.jpeg)


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni