Jumatatu, 30 Machi 2026

NAIBU WASAJILI NA MAHAKIMU WAKAZI WANOLEWA MBINU ZA USULUHISHI

Na. MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) imeendesha mafunzo maalum ya Usihi na Usuluhishi kwa Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi toka katika Mahakama mbalimbali za mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Iringa, Njombe, Sumbawanga, Songwe, Songea na Katavi.

Mafunzo hayo ya siku tatu yalianza tarehe 24 Machi, 2026 hadi tarehe 26 Machi 2026 katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya yakiongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga ambaye pia ni alikuwa mwezeshaji akishirikiana na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Momba Mhe. Raymond Kaswaga pamoja na Mhe. Gloria Shuma kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA).

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Mhe. Tiganga alitoa shukrani zake za dhati kwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi Dar Es Salaam, Mhe. Zahara Maruma kwa kuandaa na kuratibu Mafunzo hayo. Vilevile, aliwaasa washiriki kuwa chachu ya mabadiliko katika kutatua migogoro mingi kwa njia ya usuluhishi.

“Kwa mafunzo haya mliyoyapata mkawe sababu ya mabadiliko katika kutatua migogoro mingi kwa njia ya usuluhishi na kuwa walimu wazuri kwa kuwapa wengine kile mlichojifunza kwa ambao hawakupata bahati ya kuwa sehemu ya mafunzo haya. Natamani mashauri mengi katika masjala zetu yaishe kwa njia ya Usuluhishi” alisema Mhe. Tiganga.’’ alisema Mhe. Tiganga.

Mafunzo hayo yanaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Mpango Mkakati wa Mahakama unaosisitiza umuhimu wa kutumia njia mbadala ya utatuzi wa migogoro (usuluhishi) ili kuharakisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo.

Na pia ni utekelezaji wa Ibara ya 107 A (2) (d) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Mafunzo hayo yalilenga pia maandalizi ya Wiki ya Usulujishi itakayozinduliwa tarehe 9 Aprili 2026 katika Ukumbi wa Golden Jubilee PSSSF Tower Dar Es Salaam na kufuatiwa na Wiki ya Usuluhishi itakayofanyika Nchi nzima kuanzia tarehe 13 hadi 17 Aprili, 2026.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbeya Mhe. Tedy Mlimba alitoa shukurani kwa waandaaji na wawezeshaji wa mafunzo hayo kwa kufanikisha mafunzo hayo na kuahidi kuwa watayafanyia kazi yale waliyofundishwa na watakuwa walimu wazuri kwa wengine ambao hawakupata bahati ya kuwa sehemu ya mafunzo hayo.

Sehemu ya mada zilizofundishwa ni pamoja na dhana ya Usuluhishi, sheria na kanuni za usuluhishi, mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa usuluhishi, nafasi ya sheria na mawakili katika usuluhishi, vikwazo na changamoto katika usuluhishi na pia mafunzo hayo yaliambatana na mazoezi ya vitendo (Practical sessions) yaliyowasaidia washiriki kuelewa kwa kina namna ya kuendesha vikao vya usuluhishi kwa ufanisi.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga, akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.

Viongozi wa Mahakama Kuu Mbeya wakiwa Meza Kuu wakati wa kufunga mafunzo ya Usuluhishi Nyanda za Juu Kusini katikati ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga, Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu (kushoto) na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Judith Lyimo (kulia)

Sehemu ya washiriki katika mafunzo hayo.

Sehemu ya washiriki katika mafunzo hayo.

Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu akikabidhiwa cheti na Jaji Mfawidhi Mahakama kuu kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga kwa kuwa sehemu ya mafunzo hayo.

Mhe. Raimond Kaswaga akikabidhiwa cheti na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga kwa kuwa sehemu ya wawezeshaji katika mafunzo hayo.

Washiriki katika mafunzo hayo wakiwa katika mazoezi ya vitendo (Practical session) ya namna ya kuendesha vikao vya usuluhishi.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akikabidhiwa cheti na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Songea Mhe. Elizabeth Nyembele kwa kuwa sehemu ya wawezeshaji katika mafunzo hayo.

Mwezeshaji katika mafunzo hayo ambaye ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga, akimwaga madini wakati wa mafunzo hayo.

Mwezeshaji katika mafunzo hayo ambaye ni Hakimu mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Momba Mhe. Raimond Kaswaga akifundisha wakati wa mafunzo hayo

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbeya Mhe. Tedy Mlimba akitoa neno la shukurani kwa waandaaji na wawezeshaji wa mafunzo hayo kwa niaba ya washiriki wa mafunzo.

Mhe. Gloria Shuma kutoka Chuo Cha Uongozi wa mahakama (IJA) akitoa neno la shukurani katika Ufungaji wa mafunzo hayo





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni