Jumatatu, 13 Aprili 2026

BARAZA LA WAFANYAKAZI KANDA YA ARUSHA LAKETI

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda hiyo, Mhe. Frank Mahimbali ameongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo na kuwataka wajumbe wa Kikao hicho kutumia fursa ya uwepo wa baraza hilo kama eneo muhimu la kujadili na kutoa mapendekezo juu ya kuboresha mazingira ya kazi.

Akifungua kikao cha Kikao cha Baraza hilo kilichofanyika tarehe 09 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha, Mhe. Mahimbali alisema kuwa, umuhimu wa mabaraza ya wafanyakazi ni mkubwa katika kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuleta amani na utulivu mahali pa kazi kwa kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo.

“Hivyo, ni matarajio yangu kuwa kila mjumbe katika kikao hiki atashiriki kikamilifu kwa kutoa michango huru ya mawazo na pia kwa pamoja tuweze kuibua na kujadili hoja za kuwasilisha Makao Makuu kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi au ufafanuzi zaidi,” alisema Jaji Mahimbali.

Aliongeza kuwa, Vikao vya Baraza la Wafanyakazi vinasaidia katika kuongeza uelewa wa wafanyakazi kuhusu sheria za kazi, usalama kazini na majukumu yao kwa waajiri.

Jaji Mfawidhi huyo aliwahamasisha wajumbe wa Baraza hilo kwamba watumie fursa ya uwepo wa baraza hilo ili kuendelea kuwa na weledi katika kutekeleza shughuli za Mahakama na ujenzi wa Taifa kwa ujumla.

Kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Arusha kilifanya uchaguzi wa Viongozi wa Baraza hususan katika nafasi za Katibu na Katibu Msaidizi, ikiwa ni pamoja na Mwakilishi wa watumishi katika Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ambapo Bi. Therezia Shetui ambae ni Msaidizi wa Kumbukumbu alichaguliwa kuwa Katibu wa Baraza la Wafanyakazi.

Aidha, Bw. Raphael Magoha ambae ni Ofisa Hesabu alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi na kwa upande wa nafasi ya Mwakilishi wa Wafanyakazi katika Baraza Kuu la Wafanyakazi, Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama Kuu Arusha, Bi. Felister Bisangwa alichaguliwa katika nafasi hiyo. Viongozi hao waliochaguliwa watahudumu kwa kipindi cha miaka miatatu ijayo.

Kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Arusha kilihudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Sophia Massati, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Arusha, Bi. Grace Kapama, Ofisa Kazi Mfawidhi wa Mkoa wa Arusha, Bw. Goodluck Luginga na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Arusha aliyewakilishwa na Bi. Christina Ngatunga.

Wengine ni Mahakimu Wakazi Wafawidhi na Maofisa Tawala na Utumishi wa Mahakama pamoja na watumishi wa kada nyingine walioalikwa katika kikao hicho kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Arusha.

Uwepo wa Mabaraza ya Wafanyakazi ni kwa mujibu wa Sheria na Agizo Na. 1 la mwaka 1970 ambalo linaelekeza utaratibu wa kuundwa kwa Mabaraza katika Taasisi na Ofisi za Umma kwa kuzingatia sheria mbalimbali za Kimataifa ikiwemo zile za Shirika la Kazi Dunia (ILO), na imesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta haki, usalama na ustawi mahali pa kazi na hatimaye kuleta maendeleo kwa mfanyakazi, mwajiri na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha na Mwenyekiti wa Baraza la Wanyakazi wa Mahakama mkoani Arusha, Mhe. Frank Mahimbali akiongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama kilichofanyika tarehe 09 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Ofisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Arusha, Bw. Goodluck Luginga akitoa ufafanuzi wa jambo fulani wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Arusha kilichofanyika tarehe 09 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.


Wajumbe mbalimbali wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Arusha wakifuatilia kwa makini kilichokuwa kikijiri katika Kikao cha Baraza hilo kilichofanyika tarehe 09 Aprili, 2026 katika ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

 (Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni