Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Arusha, Mhe. Frank Mahimbali amesema kuwa, Mahakama ni mali ya wananchi na
kwamba Mahakama hizo zipo kwa ajili kuwahudumia wananchi.
Mhe. Mahimbali ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo mpya tatu za Ketembeine, Makuyuni na Terrat zilizopo mkoani Arusha uliofanyika tarehe 10 Aprili 2026 katika Mahakama ya Mwanzo Makuyuni wilayani Monduli.
Jaji Mfawidhi huyo alisisitiza kuwa, tukio hilo la uzinduzi na urasimishaji wa Mahakama hizo ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote wa Tanzania na ujenzi wa Mahakama hizo ni matunda ya dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa, wananchi wote wanapata haki mapema ipasavyo na kwa gharama nafuu.
“Kwa muda mrefu, wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za Mahakama, kwa mfano; wananchi wa Kata za Makuyuni, Mswakini, Esiraeli na Nanja walikuwa wakisafiri umbali wa kilomita 36 kwenda katika Mahakama ya Mwanzo Mto wa Mbu au kusafiri kilomita takribani 70 kwenda katika Mahakama ya Mwanzo Kisongo iliyopo Monduli mjini ili kupata huduma, hivyo ujenzi wa Mahakama hizi umesogeza huduma kwa wananchi hao,” alisema Jaji Mahimbali.
Vilevile Mhe. Mahimbali aliongeza kuwa, kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Mahakama kulisababisha baadhi ya wananchi kukata tamaa na kuacha kufuatilia mashauri yao na hivyo kupoteza haki zao. Pia wananchi wengine walikuwa wakiamua kujichukulia sheria mkononi mwao, hivyo Mahakama hizo zinazozinduliwa zinakwenda kuhudumia jamii zinazozizunguka Mahakama hizo kwa kusogeza huduma karibu na makazi yao na hivyo kurahisisha upatikanaji wa haki na kupunguza muda wa kupata haki, hivyo kutumia muda wao mwingi katika shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato.
Jaji Mahimbali amewashukuru wadau wa Mahakama hususan Halmashauri za Wilaya Arusha, Monduli na Longido wa kushiriki kikamilifu kufanikisha ujenzi wa Mahakama hizo mpya na kuongeza kuwa, ushirikiano huo ni kielelezo cha dhana ya kwamba ‘Mahakama ni ya Wananchi na kwa Wananchi.’ Amesisitiza kuwa huduma zitakazopatikana katika majengo hayo ya Mahakama ziwe ni kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi na si vinginevyo.
Aidha, ameongeza kwa kuwataka wananchi na watumishi wa Mahakama kutumia Mahakama hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akiwasisitiza wananchi kuwa, wanao wajibu wa kutambua kuwa majengo hayo ni mali yao na kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku na kuyalinda ikiwa ni pamoja na kuyaheshimu.
Kwa upande mwingine, Jaji Mfawidhi huyo amewasisitiza watumishi wa Mahakama hususan Mahakimu kwamba wanapaswa kuyatumia majengo hayo kama nyenzo ya kuimarisha imani ya wananchi kwa mfumo wa utoaji haki nchini.
Akiwasilisha taarifa fupi ya ujenzi wa Mahakama hizo, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bi. Grace Kapama alisema kuwa, ujenzi wa Mahakama hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa kwanza na wa pili wa Mahakama uliolenga kuboresha upatikananji na utoaji haki mapema ipasavyo kupitia uboreshaji wa Miundombinu ya Majengo na Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mijini na vijijini.
Bi. Kapama aliongeza kuwa jumla ya miradi minne ya
ujenzi ilitekelezwa, yaani ujenzi wa Mahakama za mwanzo Maji ya Chai, Terat,
Makuyuni na Ketumbeine. Mahakama ya Mwanzo Ketumbeine ilijengwa kwa fedha za
ndani wakati mahakama hizo nyingine zilijengwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki
ya Dunia.
Bi. Kapama alisema kuwa, ujenzi wa Mahakama za Mwanzo Makuyuni na Terrat ulianza tarehe 06 Julai, 2024 na kukamilika tarehe 31 Mei, 2025. Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Ketumbeine ulianza 01 Juni, 2024 na kukamilika 06 Oktoba, 2025.
Mahakama za Mwanzo Makuyuni na Terrat zimeanza kutoa huduma kwa wananchi mnamo mwezi Agosti, 2025 na Mahakama ya Mwanzo Ketumbeine ilianza kutoa huduma kwa wananchi tarehe 22 Oktoba, 2025.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Groliana Kimathi alisema kuwa, Serikali itaendelea kuhakikisha kuna amani na usalama ili kuwezesha shughuli mbalimbali za Kiserikali na wananchi kufanyika katika hali tulivu. Ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa Mahakama za Mwanzo zilizozinduliwa na kuongeza kuwa, ujenzi wa Mahakama hizo ni ishara ya dhati ya Serikali kuwajengea mazingira mazuri watumishi wa Mahakama katika kutekeleza majukumu yao na kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha, amewasihi watumishi wa Mahakama kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaweza kutia doa Mhimili wa Mahakama.
Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama katika kutekeleza majukumu yote ambayo yapo kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Aidha, ameiomba Mahakama kuendelea kutenga siku maalum ya kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kwani itasaidia kupunguza ukiukwaji wa sheria miongoni mwa wananchi na hatimaye kuwa na jamii iliyostaarabika.
Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani wa Kata ya Makuyuni, Mhe. Ngayok Mollel ameishukuru Serikali kwa kuwaletea Mahakama katika Kata yao na kuongeza kuwa, wananchi wa Kata yake katika vijiji vya Makuyuni, Mbuyuni na Naiti ikiwa ni pamoja na Kata za jirani wanafurahia kupata huduma katika Mahakama ya Mwanzo Makuyuni kwani ni karibu na makazi yao.
Uzinduzi wa Mahakama hizo unafanya jumla ya Mahakama za Mwanzo zinazofanya kazi mkoani Arusha kufikia 22 na hivyo kupanua wigo na kusogeza karibu utoaji wa huduma za Mahakama kwa wananchi katika Wilaya ya Arusha, wananchi wa Kata za Murieti, Terrat, Sombetini, Mbauda, Eleroi, Sokoni 1 na Olasiti ambao walikuwa wakisafiri umbali wa takribani kilomita 19 hadi 23 kufuata huduma katika Mahakama za Mwanzo Arusha Mjini na Themi, sasa wamesogezewa huduma karibu yao kwa kujengewa Mahakama ya Mwanzo Terrat.
Pia, Katika Wilaya ya Longido, wananchi wa Kata za Ketumbeine, Lang’atabash, Elerininto, Nondoto, Gelarirumbwa na Gelarimerugwe walikuwa wakisafiri umbali wa Kilomita 50 kufuata huduma za Mahakama ya Mwanzo Longido Mjini, kwa sasa wanapata huduma hizo katika Mahakama ya Mwanzo Ketumbeine.
Hafla hiyo ya uzinduzi rasmi wa Mahakama za Mwanzo
mpya mkoani Arusha imehudhuriwa na Viongozi na Wadau mbalimbali wa Mahakama
wakiwemo Majaji na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Arusha, Mkuu wa Wilaya ya
Monduli, Mahakimu, Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Diwani wa
Kata ya Makuyuni, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Kimila na wananchi kwa ujumla.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali akizungumza na wananchi pamoja na wadau waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama mpya za Mwanzo Makuyuni, Ketumbeine na Terrat tarehe 10 Aprili, 2026 katika Mahakama ya Mwanzo Makuyuni iliyopo wilayani Monduli.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Gloriana Kimath akitoa salamu kwa wananchi na wadau waliofika katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo mpya za Makuyuni, Ketumbeine na Terrat uliofanyika tarehe 10 Aprili, 2026 katika Mahakama ya Mwanzo Makuyuni wilayani Monduli.
Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bi. Grace Kapama akisoma historia fupi ya ujenzi wa Mahakama hizo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo mpya za Makuyuni, Ketumbeine na Terrat uliofanyika tarehe 10 Aprili, 2026 katika Mahakama ya Mwanzo Makuyuni.
Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bi. Grace
Kapama (kushoto) akikabidhi taarifa fupi ya historia ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo Makuyuni,
Ketumbeine na Terrat kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kanda ya Arusha, Mhe. Frank
Mahimbali wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama hizo uliofanyika tarehe 10
Aprili, 2026 katika Mahakama ya Mwanzo Makuyuni wilayani Monduli.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali (kushoto picha ya chini) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo Makuyuni, Ketumbeine na Terrat wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama hizo uliofanyika tarehe 10 Aprili, 2026 katika Mahakama ya Mwanzo Makuyuni wilayani Monduli. Picha ya juu akiwa na viongozi mbalimbali walioalikwa katika hafla hiyo.
Wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo mpya za Makuyuni, Ketumbeine na Terrat uliofanyika tarehe 10 Aprili 2026 katika Mahakama ya Mwanzo Makuyuni wilayani Monduli.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe.
Frank Mahimbali akipanda mti ikiwa ni ishara ya kumbukumbu na sehemu ya kuboresha mazingira
ya Mahakama ya Mwanzo Makuyuni wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo mpya za Makuyuni, Ketumbeine na Terrat iliyofanyika tarehe 10 Aprili, 2026.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali (katika) pamoja na Majaji wengine wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Gloriana
Kimathi (wa pili kushoto mstari wa mbele) wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi
wa Mahakama za Mwanzo mpya za Makuyuni, Ketumbeine na Terrat uliofanyika tarehe 10
Aprili, 2026 katika Mahakama ya Mwanzo Makuyuni Monduli. Waliosimama nyuma ni kulia Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Dkt. Kassian
Mshomba na kushoto ni Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Bi. Grace
Kapama.
Diwani wa Kata ya Makuyuni, Mhe. Ngayok Mollel akitoa salamu za wananchi wa Kata ya Makuyuni wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Mahakama za Mwanzo Makuyuni, Ketumbeine na Terrat uliofanyika tarehe 10 Aprili, 2026 Makuyuni Monduli.
Kiongozi wa Mila wa Kabila la Maasai Monduli, Bw. Samwel Laiza akisoma dua wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo Makuyuni, Ketumbeine na Terrat uliofanyika tarehe 10 Aprili, 2026 Makuyuni Monduli.
Kikundi cha Burudani cha Kabila la Wamaasai kutoka Makuyuni Juu kiitwacho Nashpai Eko kikitumbuiza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo Makuyuni, Ketumbeine na Terrat uliofanyika tarehe 10 Aprili, 2026 Makuyuni Monduli.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni