· Lajadili Ufanisi wa Utendaji kwa Ubunifu na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027
Na MICHAEL RITTE, Mahakama- Bukoba
Baraza la
Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba limekutana na kufanya
kikao chini ya Uenyekiti wa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Immaculata Banzi lengo likiwa ni kujadili masuala
muhimu ya utendaji kazi na kupitisha mwelekeo wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha
2026/2027.
Kikao hicho
kilichofanyika tarehe 10 Aprili, 2026 kilianza kwa utaratibu wa kufanya
uchaguzi wa Katibu wa Baraza, ambapo Bw. Rojas Rwanyumba alichaguliwa kushika
nafasi hiyo baada ya kupata kura nyingi za maoni kutoka kwa wajumbe.
Wakati wa kufungua
kikao hicho, Mwenyekiti alieleza matarajio yake kuwa baraza hilo litatoa
mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utendaji kazi wa Mahakama katika Kanda ya
Bukoba na kutangaza rasmi kufunguliwa kwa mkutano huo.
Akihutubia Baraza
hilo, Mwenyekiti, Jaji Banzi alisisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kufanya
kazi kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, weledi na uwajibikaji huku akiwahimiza
watumishi kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi licha ya changamoto za bajeti
ndogo inayoongezeka kidogo huku majukumu yakiongezeka.
Alieleza kuwa, kikao
hicho kina lengo la kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita na kuweka
mwelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuboresha utoaji wa huduma
za haki kwa wananchi.
Katika hotuba
yake, Jaji Mfawidhi huyo aliwahimiza watumishi kuwa wabunifu katika kukabiliana
na changamoto za kiutendaji, akitoa mfano wa matumizi ya rasilimali zilizopo
kama miti ya zamani kutengeneza samani za Mahakama, ikiwa ni njia ya kupunguza
gharama na kuongeza ufanisi.
Kwa upande wa
utendaji kazi, alibainisha kuwa hali ya uendeshaji wa mashauri kwa ujumla ni
nzuri katika Kanda hiyo, ingawa bado kuna changamoto ya mashauri yanayochelewa
kukamilika.
Alieleza kwamba,
kuna mashauri machache katika ngazi mbalimbali za Mahakama yaliyovuka muda
uliopangwa, na kusisitiza kuwepo kwa mikakati madhubuti ya kuhakikisha mashauri
hayo yanamalizika mapema ipasavyo ili kufikia lengo la kutokuwa na mlundikano
wa mashauri (zero backlog).
Aidha, aliwahimiza
watumishi kushirikiana kati ya vituo mbalimbali ili kusaidiana pale ambapo kuna
mzigo mkubwa wa mashauri pamoja na kuendelea kuongeza juhudi katika utoaji wa
maamuzi kwa wakati.
Viongozi wengine
waliohudhuria ni pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Bw. Edward
Mbara, Katibu wa TUGHE Mkoa, Bw. Kitanda pamoja na wajumbe na waalikwa kutoka Wilaya
mbalimbali ndani ya Kanda hiyo.
Katika kikao
hicho, wajumbe walipata fursa ya kuwasilisha hoja mbalimbali zilizolenga
kuboresha ustawi wa watumishi na mazingira ya kazi. Miongoni mwa hoja hizo ni
pamoja na Ulipaji wa posho za sare na likizo kwa wakati, kutengwa kwa bajeti
maalum ya mafunzo kwa watumishi, Uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama hususan
kwa maeneo yanayokumbwa na changamoto kama mafuriko.
Hoja nyingine ni kushughulikia
ucheleweshaji wa ada kwa watumishi wanaodhaminiwa masomoni, kuandaliwa kwa
semina za afya ya akili kwa watumishi, kuboresha maslahi ya Madereva na Wasaidizi
wa Ofisi, kuwepo kwa makazi karibu na vituo vya kazi kwa Mahakimu na kuboresha
mfumo wa uhamisho wa watumishi na utoaji wa mikopo kwa watumishi wa kipato cha
chini.
Baraza la Wafanyakazi linaendelea kuwa jukwaa muhimu la ushauri na maamuzi katika kuboresha utendaji wa Taasisi za umma nchini.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo, Mhe. Immaculata Banzi (kulia) pamoja na Katibu wa Baraza hilo, Bw. Rojas Rwebugisa Rwanyumba wakiongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Bukoba kilichofanyika tarehe 10 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama.
Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Bi. Monica Kalokola akiwasilisha hoja mbele ya viongozi, wajumbe na waalikwa wakati wa Kikao cha Baraza hilo.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba. Kutoka kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Biharamulo, Mhe. Flora Ndale (kushoto), katikati ni Terrysophia Tesha na kulia ni Flora Haule. Walioketi nyuma yao ni wajumbe na waalikwa wa Baraza hilo wakifuatilia na kusikiliza kwa makini na utulivu hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na wajumbe wa Baraza.

Ewaaaaa mambo mazuri Sana waatalamu
JibuFuta