Jumapili, 12 Aprili 2026

BARAZA LA WAFANYAKAZI MAHAKAMA BUKOBA LAKUTANA

 ·       Lajadili Ufanisi wa Utendaji kwa Ubunifu na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027

Na MICHAEL RITTE, Mahakama- Bukoba

Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba limekutana na kufanya kikao chini ya Uenyekiti wa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Immaculata Banzi lengo likiwa ni kujadili masuala muhimu ya utendaji kazi na kupitisha mwelekeo wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha 2026/2027.

Kikao hicho kilichofanyika tarehe 10 Aprili, 2026 kilianza kwa utaratibu wa kufanya uchaguzi wa Katibu wa Baraza, ambapo Bw. Rojas Rwanyumba alichaguliwa kushika nafasi hiyo baada ya kupata kura nyingi za maoni kutoka kwa wajumbe.

Wakati wa kufungua kikao hicho, Mwenyekiti alieleza matarajio yake kuwa baraza hilo litatoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utendaji kazi wa Mahakama katika Kanda ya Bukoba na kutangaza rasmi kufunguliwa kwa mkutano huo.

Akihutubia Baraza hilo, Mwenyekiti, Jaji Banzi alisisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, weledi na uwajibikaji huku akiwahimiza watumishi kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi licha ya changamoto za bajeti ndogo inayoongezeka kidogo huku majukumu yakiongezeka.

Alieleza kuwa, kikao hicho kina lengo la kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita na kuweka mwelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuboresha utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Katika hotuba yake, Jaji Mfawidhi huyo aliwahimiza watumishi kuwa wabunifu katika kukabiliana na changamoto za kiutendaji, akitoa mfano wa matumizi ya rasilimali zilizopo kama miti ya zamani kutengeneza samani za Mahakama, ikiwa ni njia ya kupunguza gharama na kuongeza ufanisi.

Kwa upande wa utendaji kazi, alibainisha kuwa hali ya uendeshaji wa mashauri kwa ujumla ni nzuri katika Kanda hiyo, ingawa bado kuna changamoto ya mashauri yanayochelewa kukamilika.

Alieleza kwamba, kuna mashauri machache katika ngazi mbalimbali za Mahakama yaliyovuka muda uliopangwa, na kusisitiza kuwepo kwa mikakati madhubuti ya kuhakikisha mashauri hayo yanamalizika mapema ipasavyo ili kufikia lengo la kutokuwa na mlundikano wa mashauri (zero backlog).

Aidha, aliwahimiza watumishi kushirikiana kati ya vituo mbalimbali ili kusaidiana pale ambapo kuna mzigo mkubwa wa mashauri pamoja na kuendelea kuongeza juhudi katika utoaji wa maamuzi kwa wakati.

Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Bw. Edward Mbara, Katibu wa TUGHE Mkoa, Bw. Kitanda pamoja na wajumbe na waalikwa kutoka Wilaya mbalimbali ndani ya Kanda hiyo.

Katika kikao hicho, wajumbe walipata fursa ya kuwasilisha hoja mbalimbali zilizolenga kuboresha ustawi wa watumishi na mazingira ya kazi. Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na Ulipaji wa posho za sare na likizo kwa wakati, kutengwa kwa bajeti maalum ya mafunzo kwa watumishi, Uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama hususan kwa maeneo yanayokumbwa na changamoto kama mafuriko.

Hoja nyingine ni kushughulikia ucheleweshaji wa ada kwa watumishi wanaodhaminiwa masomoni, kuandaliwa kwa semina za afya ya akili kwa watumishi, kuboresha maslahi ya Madereva na Wasaidizi wa Ofisi, kuwepo kwa makazi karibu na vituo vya kazi kwa Mahakimu na kuboresha mfumo wa uhamisho wa watumishi na utoaji wa mikopo kwa watumishi wa kipato cha chini.

Baraza la Wafanyakazi linaendelea kuwa jukwaa muhimu la ushauri na maamuzi katika kuboresha utendaji wa Taasisi za umma nchini.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo, Mhe. Immaculata Banzi (kulia) pamoja na Katibu wa Baraza hilo, Bw. Rojas Rwebugisa Rwanyumba wakiongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Bukoba kilichofanyika  tarehe 10 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama.

 Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo na Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Bukoba, Mhe. Flora Ndale akiwasilisha hoja mbele ya Viongozi, wajumbe na waalikwa wakati wa kikao cha Baraza hilo kilichofanyika tarehe 10 Aprili, 2026.

Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Bi. Monica Kalokola akiwasilisha hoja mbele ya viongozi, wajumbe na waalikwa wakati wa Kikao cha Baraza hilo.

Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba. Kutoka kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Biharamulo, Mhe. Flora Ndale (kushoto), katikati ni Terrysophia Tesha na kulia ni Flora Haule. Walioketi nyuma yao ni wajumbe na waalikwa wa Baraza hilo wakifuatilia na kusikiliza kwa makini  na utulivu hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na wajumbe  wa Baraza.


 (Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

Maoni 1 :