Jumanne, 21 Aprili 2026

JAJI MANYANDA ASISITIZA UTOAJI HAKI USIYOTONESHA MAJERAHA YA UKATILI WA KIJINSIA

Na. SHARIFU MOKIWA-Mahakama, Sumbawanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Kapela Manyanda amewataka washiriki wa Mafunzo ya kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia ambao ni Mahakimu wa Mahakama za Wilaya, Waendesha Mashtaka wa Serikali pamoja na Maafisa wa Ustawi wa Jamii kutoka mikoa ya Rukwa na Katavi kuongeza umakini wanaposhughulikia mashauri ya aina hiyo ili kuwajengea imani waathirika wanapofika mahakamani.

Mhe. Manyanda alisema hayo wakati akifungua Mafunzo ya siku tatu kuhusu namna ya kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia (Sexual and Gender Based Violance-SGBV) Mafunzo hayo yameanza jana tarehe 20 Aprili, 2026 katika ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Sumbawanga.

Mhe. Manyanda ameongeza kuwa, mafunzo hayo yanalenga kuwasaidia washiriki kuhakikisha wanaepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Mafunzo haya yakatumike kuhakikisha kuwa tunaepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, tutumie lugha ya staha, tuzingatie weledi na tujenge mazingira ambayo waathirika wanaweza kuwa huru kutoa ushahidi bila kuathiri kumbukumbu zao,” alisema Mhe. Manyanda

Aidha, Jaji Manyanda aliongeza kuwa, utoaji wa haki unapaswa kuzingatia utu, usalama na mazingira rafiki kwa waathirika ili kusaidia upatikanaji wa haki bila kuongeza maumivu ya kihisia na kisaikolojia.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa  Irishi Rule of Law International pamoja na kushirikiana na Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Sumbawanga.

Vilevile, Mafunzo hayo yanawezeshwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga, Mhe. Pamela Mazengo kwa kushirikiana na Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Wilaya Momba, Mhe. Raymond Kaswaga.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 22 Aprili, 2026 huku yakilenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa haki na kuimalisha ulinzi kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia katika jamii.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Kapela Manyanda akifungua mafunzo ya kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia

Sehemu ya washiriki wa Mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini mada mbalimbali zinazoendelea kutolewa na wawezeshaji

Washiriki wa Mafunzo hayo wakiwa kwenye majadiliano ya pamoja wakati wa Mafunzo 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga, Mhe. Pamela Mazengo (aliyesimama) akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo. 

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Kapela Manyanda (katikati) wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo hayo. 

Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Wilaya Momba, Mhe. Raymond Kaswaga (aliyesimama) akiwasilisha mada wakati wa mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Sumbawanga



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni