Jumanne, 14 Aprili 2026

JAJI MFAWIDHI TANGA AONGOZA KIKAO CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI

Na MUSSA MWINJUMA-Mahakama, Tanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Mteule, jana tarehe 13 Aprili, 2026 aliongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi lililofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Tanga.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali ndani ya Kanda pamoja na wajumbe wengine waalikwa, wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Messe Chaba na Mhe. Happiness Ndesamburo.

Akifungua kikao hicho, Mhe. Mteule aliwashukuru wajumbe wote kwa kufika pamoja na changamoto za mvua na kuharibika kwa mindombinu ya barabara. Aidha alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwenye kikao na kila Wilaya kupata uwakilishi.

“Baraza hili lipo kwa mujibu wa sheria na ni maelekezo ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Baraza ni sauti na ni lazima Watumishi wapate eneo au vikao rasmi kama hivi ili kutoa maoni ,ushauri na hata mapendekezo ya namna gani Taasisi yao inaweza kuendeshwa ili kuleta tija na matokeo Chanya,” alisema.

Aidha, Jaji Mfawidhi alisisitiza umuhimu wa Baraza kuwa ni kikao mahsusi kinachotoa fursa kwa Watumishi kujenga hoja za kiutendaji, kujua sera na mipango kupitia taarifa mbalimbali zitakazowasilishwa.

“Nawasihi sana kutoa maoni yenu kwa uhuru na maoni ya mnaowawakilisha hapa; usitoe maoni yako binafsi ukaacha ya wale unaowawakilisha, na ni vyema baada ya kikao hiki twende tukawape mrejesho wale wenzetu ambao hawapo hapa, hii itatusaidia kujenga mshikamano ,” alisisistiza Jaji Mteule.

Akizungumza Katika Baraza hilo, Ofisa Kazi Mwandamizi kutoka Idara ya Kazi jijini Tanga, Bi Diana Chacha, aliwaasa wajumbe juu ya usiri wa taarifa za Baraza na taarifa binafsi ndani ya kikao.

“Usiri wa Baraza ni muhimu sana kwa taarifa za Taasisi na taarifa binafsi, usitoe siri za Baraza kwani kinachoamuliwa kinabaki kuwa maazimo ya kikao,” alisema.

Taarifa mbalimbai za mashauri na kiutendaji ziliwasilishwa na wajumbe walipata fursa ya kujua hali ya mashauri pamoja na mipango ya baadaye ya Kanda kwenye masuala ya miundombinu, maslahi, afya za Watumishi na michezo.

Akifunga kikao hicho, Mhe. Mteule aliwashukuru wajumbe kwa michango yao mizuri yenye kujenga, lakini alitoa rai juu ya kujenga utamaduni wa kusikiliza hotuba za Viongozi wa Taasisi. Alisema kuwa ndani ya hotuba hizo kuna majibu ya maswali mengi ambayo huwa wanajiuliza bila kupata majibu.

“Najua mambo ni mengi, lakini nawaomba Watumishi tujenge utamaduni wa kusikiliza hotuba za Viongozi wetu ili kujua maboresho mbalimbali yanayofanywa kwa maslahi yetu kama Taasisi,” alisema.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Mteule, akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi.

Wajumbe waalikwa, Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Messe Chaba na Mhe. Hapiness Ndesamburo.

Ofisa Kazi Mwandamizi kutoka Idara ya Kazi Tanga, Bi. Diana Chacha, akiwasilisha mada ndani ya kikao cha Baraza.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Bw. Jumanne Msuta akiwasilisha taarifa ya utendaji mbele ya wajumbe wa Baraza.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Tanga, Mhe. Hudi Majid Hudi, akiwasilisha taarifa ya mashauri mbele ya wajumbe wa Baraza.


Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Baraza wakimsikilzia Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Mteule (hayupo pichani).

 Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni