Jumanne, 14 Aprili 2026

MAHAKAMA DODOMA YAANZA MAADHIMISHO YA WIKI YA USULUHISHI

Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama Kuu, Dodoma

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, imeanza rasmi maadhimisho ya Wiki ya Usuluhishi yanayoendelea kuanzia tarehe 13 hadi 17 Aprili, 2026, sambamba na Kanda nyingine nchini.

Maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kaulimbiu isemayo, “Kutumia Njia Mbadala ya Utatuzi wa Migogoro kama Mbinu Inayopendelewa ya Kutatua Migogoro nchini Tanzania.”

Katika kipindi hiki, uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, ukiongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt.Juliana Masabo, umejipanga kuhakikisha Wananchi wanapata huduma kwa urahisi zaidi kwa kupokea na kusajili migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi, ndoa na madai ya kawaida. Migogoro hiyo inapatiwa ufumbuzi kupitia Wasuluhishi waliobobea katika mbinu za usuluhishi.

Kwa upande mwingine, dawati maalumu la huduma limeanzishwa katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma kwa ajili ya kupokea malalamiko na kutoa mwongozo kwa Wananchi, huku mazingira maalumu yakiandaliwa ili kuhakikisha usuluhishi unafanyika kwa ufanisi na faragha.

Katika kuifikia jamii kwa upana zaidi, Mahakama pia imeendesha kampeni ya utoaji elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, ikiwemo Radio Mwangaza na Radio Family FM, ambapo Wananchi wameelimishwa juu ya umuhimu wa kuchagua usuluhishi kama njia ya haraka, nafuu na yenye tija katika kutatua migogoro.

Wananchi waliojitokeza kushiriki maadhimisho hayo wamepata nafasi ya kujifunza kwa kina kuhusu dhana ya usuluhishi, kuuliza maswali na kupata majibu ya kitaalamu kuhusu masuala ya kisheria yanayohusu utatuzi wa migogoro nje ya mfumo wa kawaida wa Mahakama.

Kwa ujumla, Wiki ya Usuluhishi siyo tu jukwaa la kutoa elimu, bali ni fursa muhimu kwa jamii kubadili mtazamo kuhusu namna bora ya kushughulikia migogoro yao. Kupitia njia ya usuluhishi, Wananchi wanahimizwa kuchagua amani, maelewano na suluhisho la haraka badala ya migogoro mirefu inayoweza kuleta madhara kwa pande zote.

Mahakama ina matarajio kuwa Wananchi wataendelea kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hii adhimu, siyo tu wakati wa maadhimisho haya, bali hata baada yake, kwa lengo la kujenga jamii yenye mshikamano, haki na ustawi wa kudumu.

Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiwa katika picha ya pamoja pamoja na Viongozi wa Dodoma baada ya kutembelea dawati maalumu lililowekwa kwa ajili ya Maadhimisho ya Wiki ya Usuluhishi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.  Katikati ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rehema Kirefu, anaefuatia kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe Abraham Mwampashi, anaefuatia wa kwanza kulia kwake Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe Mustafa Ismail, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo, wa tatu kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan, wa tatu kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Agatha Chugulu na wa nne kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Upendo Ngitili.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Dodoma, Mhe. Judith Baligenge akiwa katika studio za Radio Mwangaza iliyopo Jijini Dodoma akitoa elimu kuhusu usuluhishi.

 Wakili wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Mwita Mohere, akiwa katika studio za Radio Mwangaza iliyopo Jijini Dodoma akitoa elimu kuhusu usuluhishi.


 

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kongwa, Mhe. Sarah Mwalilino (wa kwanza kulia) akiwa ameambatana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Wizara ya Katiba na Sheria, Bi Zerafina Gotora wakiwa katika Studio za Family Fm zilizopo Ilazo Jijini Dodoma wakitoa elimu kuhusu usuluhishi.

 

Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan (katikati) na kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Mhe. Zabibu Mpangule na kushoto kwake ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Dodoma, Mhe. Thurston Kombe, wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Wiki ya usuluhishi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni