- Wajumbe wadhamiria mifumo ya Mahakama, Wadau kusomana kupunguza udanganyifu
Na
HIGHNESS TERRY-Kituo Jumuishi cha Masuala Familia,Temeke
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Ndoa na Familia
Temeke, Mhe. Sara Mwaipopo, hivi karibuni aliwaongoza Mahakimu na Wadau
mbalimbali wa Mahakama katika kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai.
Kikao
hicho (Bench Bar Meeting) kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano katika kituo
hicho na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbalimbali wa Mahakama, akiwemo Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Frank Moshi, aliyekuwa
Katibu wa Kikao.
Wengine
ni Mtendaji wa Mahakama Kituo Jumuisgi Temeke, Bw. Samson Mashalla, Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mahakama ya Watoto, Mhe. Mwamini Kazema, Hakimu Mkazi Mfawidhi
Mahakama ya Wilaya, Mhe. John Msafiri na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Mwanzo, Mhe. Upendo Kapama.
Walikuwepo
pia Wajumbe wa Sekretarieti kutoka IJC Temeke pamoja na Wadau mbalimbali wa
huduma za kimahakama kutoka PSSSF, RITA, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Msajili wa
Hati, Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Mwakilishi kutoka Benki ya CRDB na
wawakilishi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Akizungumza
katika ufunguzi wa Kikao hicho, Mhe. Mwaipopo alisema kuwa ni jukumu la Mahakama
kushirikiana kwa karibu na Wadau katika utekelezaji wa majukumu.
“Katika
kusimamia mpango mkakati wake wa kumaliza mashauri ya mlundikano, Mahakama katika
Kituo Jumuishi Temeke inatambua umuhimu mkubwa wa Wadau kwenye utekelezaji wa
majukumu yetu. Tunawaalika Wahusika na Wadau wote ambao majukumu yao yanaathiri
utendaji wa kazi tushirikiane ili kupunguza au kumaliza kabisa mashauri
mlundikano,” aliongeza Mhe. Mwaipopo.
Aidha,
katika kikao hicho, Wadau walipata taarifa katik ya robo ya tatu ya mwaka iliyowasilishwa
na Katibu, ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Frank Moshi, na
kuona takwimu za hali ya mashauri kutoka Mahakama Kuu, Mahakama ya Watoto,
Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo.
Wakati
wa wasilisho hilo, wajumbe pia waliweza kufahamu sababu zilizochangia
kutokumalizika kwa wakati mashauri katika Mahakama zote na walipata nafasi ya
kutoa maoni yao.
Naibu
Msajili alieleza changamoto kubwa upande wa mirathi kuwa na muda mrefu wa
kufuatilia mashauri hayo pamoja na kuchelewa kufunga mirathi kwa wakati.
Aidha,
alieleza changamoto kubwa ya utekelezaji kuwa ni muda mrefu wa upatikanaji wa
wanunuzi wa mali za ndoa pamoja na utathimini wa thamani wa mali husika.
Wajumbe
wa kikao walijadili mambo mbalimbali, ikiwemo tatizo la uhamishaji wa hati za
umiliki kwenda kwa warithi pamoja na uhamishaji wa hisa na vipande kutoka
kwenye Taasisi za Waadau.
Suluhisho
lililotolewa ni kuomba uboreshaji wa mifumo ya Mahakama na Wadau wake kusomana,
lakini pia kuongeza uelewa kwa wateja wanohudumiwa juu ya ufuatiliaji wa stahiki hizo.
Pia
kulikuwepo na majadiliano kuhusu kuchelewa kufunga mashauri kutoka Mahakama ya
Watoto, ambapo sababu iliyobainishwa ni kuchelewa kwa majibu ya vinasaba (DNA)
kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, huku upande wa Mahakama Kuu, sababu
iliyotolewa ni kuwepo kwa amri ya Mahakama ya kufungua shauri upya baada ya
makosa kufanyika.
Kulikuwepo
pia na changamoto ya suala la
kubadilisha majina ya umiliki wa ardhi iliyobainishwa, jambo linalosababisha
kupita muda wa kusikiliza mashauri uliowekwa kwenye kadi kipimo, ambayo ni siku
60 kwa Mahakama ya Mwanzo na Watoto, Siku 90 kwa Mahakama ya Wilaya na Siku 120
kwa Mahakama Kuu.
Ofisa
Sheria kutoka RITA, Bi.Janeth Mandawa, aliongeza kuwa kuna changamoto ya wateja
kuvutana juu ya nani kupata mali zisizohamishika na zinazoamishika kutokana na
usheleweshaji katika uhamishaji wa umilik wa ardhi.
Alisisitiza
kuwa ni muhimu ujumbe wa vikao kama hivyo kufika katika ofisi zote zinazohusika
na taratibu za uhamishaji wa umiliki wa ardhi.
Hakukuwepo
na mjumbe kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu ili kuleta majibu katika hoja ya miongozo
inayohitajika kwa ajili ya upimaji wa vinasaba (DNA) kutokana na udhuru wa
kuomba muda kwa ajili ya taratibu ya kuandaa orodha itakayotumika kwa nchi
nzima.
Akijibu hoja hiyo, Mjumbe wa Halmashauri ya
Kigamboni alieleza kuwa ,“Sisi bado tupo kwenye majadiliano na pia tumeanzisha
mradi wa kutengeneza hati miliki kwa awamu na kuendelea na zoezi la upimaji wa
ardhi kwa maeneo ambayo hayajapimwa.
“…tumewasiliana
na Ofisi ya Ardhi na tayari hoja hii imepelekwa katika Baraza la Madiwani ili
kujadili namna bora ya kutoa uhakiki wa taarifa maalum za umiliki ili kutatua
changamoto hii.”
Mjumbe huyo aliongeza kuwa ni muhimu kuwepo na mfumo unaosomana ili kuwezesha kesi zilizopo mahakamani na zenye kuhitaji uhamishaji wa umiliki ardhi zitumwe na Mahakama katika mfumo husika ili kufanyiwa kazi kwa haraka na kuepusha mashauri kukaa muda mrefu bila kumalizika.
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Ndoa na
Familia Temeke, Mhe. Sara Mwaipopo, akitoa neno la ufunguzi wa Kikao cha
Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai kilichofanyika hivi karibuni. Kulia ni Katibu
wa Kikao na Naibu Msajili, Mhe. Frank Moshi na kushoto ni Mtendaji, Bw. Samson
Mashalla.
Katibu
wa Kikao na Naibu Msajili, Mhe. Frank Moshi, akitoo ufafanuzi katika kikao cha
Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai.
Ofisa kutoka Banki Kuu ya Tanzania akitoa ufafanunuzi juu ya orodha ya mahitaji ili
kuhamisha umiliki wa hisa au vipande kutoka kwa marehemu kuja kwa warithi.
Wajumbe
wa Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai ambao ni wadau wa Mahakama
kutoka Taasisi mbalimbali wakisikiliza kwa makini wasilisho kutoka kwa Naibu
Msajili na Katibu wa Kikao, Mhe. Frank Moshi (hayupo pichani).
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni