Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa amekutana na wadau wa Mahakama Taasisi
mbalimbali zinazotoa huduma kwa wananchi ndani ya Kanda hiyo ili kuteta nao juu
ya uanzishwaji wa shughuli za Mahakama Kuu Njombe
Akizungumza na wadau hao tarehe
30 Machi, 2026 aliwaeleza kuwa, Mahakama Kuu Kanda ya Njombe imeanza
kufanya kazi Jumatatu tarehe 30 Machi, 2026.
Aidha, Mhe. Nongwa alisema
kuwa, kuanza kazi kwa Mahakama hiyo kulianza kwa kufunguliwa kwa dirisha la
kusajili mashauri. Hivyo, aliwaeleza Wadau wa Mahakama kuwa, lengo la kikao
hicho ni kuzungumza kwa pamoja na kupeana ushauri katika kukabiliana na changamoto
mbalimbali.
Pamoja na kushauriana na kufafanua zaidi pale
penye changamoto za usikilizwaji mashauri kwa njia ya kieletroniki wakati yanapokatiwa
rufaa, Jaji Nongwa ameomba ushirikiano wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) hasa
kwa mashauri ya mauaji.
Kuhusu Baraza la Kata la
Nyumba na Ardhi, Mhe. Nongwa amewasisitiza kuhusu mfumo wao ambao bado
haujaungana na Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) hivyo, Baraza
hilo litatakiwa kuwa na nakala laini pindi zinapohitajika mahakamani.
Kwa upande wa Madalali wa
Mahakama, Jaji Mfawidhi huyo amewataka kufuata sheria kwenye mashauri
yanayokaziwa hukumu kwa kuwa mashauri hayo yana hatua mbalimbali.
Alielezea jinsi ya ufunguaji
wa mashauri kwa njia ya kieletroniki ya kutotumia karatasi (paperless) kwenye
dirisha dogo la ufunguaji wa mashauri kupitia Mfumo wa Kieletroniki wa Usimamizi
wa Mashauri (e-CMS) la Masjala ndogo ya Mahakama Kuu Kanda ya Njombe iliyoanza
kutoa huduma zake kuanzia Siku ya Jumatatu tarehe 30 Machi, 2026.
Kwa upande mwingine Jaji
Nongwa alisisitiza umoja na mshikamano kwa Mawakili na kwa Taasisi nyingine za Haki Jinai ili waweze
kutoa huduma kwa wateja ambao ni wananchi kwa weledi na ufanisi hasa kwa kutoa
kipaumbele kwa wateja walio kwenye makundi maalum mfano kwa akinamama
wajawazito, wazee na akina Mama wenye watoto wadogo.
Naye Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama na Mtendaji
wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe, Bw. Richard Mbambe kwa pamoja waliwashukuru
Wadau wa Mahakama Kwa utayari wa kufika kwa ajili ya kumsikiliza Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa na kuhaidi kuendeleza ushirikiano.
Wadau walioshirikiki katika kikao hicho ni Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Njombe, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa Njombe (RCO), Baraza La Nyumba na Ardhi, Mawakili wa Kujitegemea pamoja na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali kutoka Mkoa wa Njombe ambao walichangia hoja mbalimbali kwa pamoja juu ya uendeshaji wa Masjala ndogo ya Mahakama Kuu Njombe.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa akizungumza na Wadau wa mkoani Njombe. (hawapo katika picha) tarehe 30 Machi, 2026.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano akizungumza na Wadau na Mawakili wa Mkoa wa Njombe (hawapo katika picha).
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa Njombe Mhe. Liadi Chamshamu akitoa neno la shukrani kwa Wadau (hawapo katika picha) walioshiriki katika kikao.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Njombe, Bw. Richard Mbambe akitoa neno la shukrani kwa wadau wa Mkoa wa Njombe. Nyuma yake ni Ofisa Utumishi, Bi. Happy Merere pamoja na wadau wengine waliohudhuria katika kikao hicho.
Wadau wa Mahakama pamoja wakifuatilia kinachojiri katika kikao.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni