Alhamisi, 2 Aprili 2026

NAIBU MSAJILI MBEYA AONGOZA KIKAO CHA KUSUKUMA MASHAURI YA JINAI

Na. MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama Mbeya

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya imefanya kikao cha kusukuma mashauri ya jinai kilichoongozwa na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Aziza Temu kwa lengo la kuimarisha usimamizi na ufanisi wa utoaji haki kwa wakati mapema ipasavyo.

Akizungumza katika kikao hicho Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, alibainisha kuwa azimio la kuhakikisha mashauri ya mlundikano hayavuki Desemba 2025 limefanikiwa kwa kiasi kikubwa, huku juhudi za kupunguza vielelezo mahakamani hasa dawa za kulevya, zikiendelea kwa kushirikiana na vyombo husika ili kuharakisha uteketezaji wake.

Akiwasilisha taarifa ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Aziza Temu alieleza kuwa, kwa sasa hakuna mashauri ya mlundikano kwa Mahakama Kuu Mbeya na kwa Mahakama za chini ni machache ambayo yamebaki kwa sababu maalumu ambapo mengine yanasubiri maamuzi ya Mahakama ya Rufani. Aliongeza kuwa, Mahakama Kuu imeweka rekodi mpya kwa kumaliza mashauri yote ya mlundikano.

Kikao pia kilipokea taarifa ya ujio wa Wahe. Majaji na watumishi wengine wa Mahakama ya Rufani mwezi Aprili 2026, pamoja na kuanza kwa vikao vya kesi za mauaji Mahakama Kuu Mbeya kuanzia tarehe 13 Aprili 2026.

Aidha, ilibainishwa kuwa, kutokana na kujitenga kwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mkoa wa Songwe, kutasaidia kupunguza mzigo wa mashauri katika Kanda ya Mbeya na idadi ya wafungwa na mahabusu katika Gereza Kuu la Ruanda Mbeya.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer, akiwasilisha taarifa ya Mahakama Mkoa wa Mbeya, alizungumzia kuhusu jitihada za Mahakama kusimamia utoaji wa haki mapema ipasavyo:

“Kufuatia maelekezo ya Jaji Mkuu, mashauri yanapaswa kumalizika ndani ya miezi sita kwa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya na miezi mitatu kwa Mahakama za Mwanzo. Sote tushirikiane kuhakikisha kwamba ukomo huu unazingatiwa” alisema Mhe. Laizer

Vilevile, Mhe. Laizer alisisitiza umuhimu wa taarifa za Wafungwa na Mahabusu hususan utoro wa Mahabusu na wafungwa walio chini ya ulinzi halali, kufikishwa mapema mahakamani ili kuisaidia Mahakama katika kuandaa usikilizwaji wa mashauri mbalimbali.

Katika maazimio ya kikao hicho ilikubaliwa kuwa, taarifa muhimu za wafungwa, ikiwemo utoro, vifo, msamaha wa Rais au kumaliza kifungo, ziwasilishwe kwa wakati mahakamani ili kusaidia katika upangaji wa Vikao vya kusikiliza mashauri, ili mashauri yote yamalizika ndani ya miezi sita tangu kusajiliwa kwake na yaliyovuka muda huo yapewe kipaumbele yakamilike kabla au ifikapo Juni 2026.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau wa mnyororo ya haki jinai wakiwemo Wahe. Mahakimu Mkoa wa Mbeya, Magereza, Polisi, Ofisi ya Upelelezi, Ofisi ya Mdhibiti Mali za Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Mbeya (NPS), Ustawi wa Jamii, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitengemea (TLS), Idara ya Marekebisho ya Tabia na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu (kushoto), akiendesha kikao hicho wakati wa kuwasilisha taarifa ya Mahakama Kuu Mbeya.

Mwakilishi wa Mkuu wa Gereza Kuu Ruanda Afisa Magereza akizungumza jambo katika kikao hicho.

Sehemu ya wadau walioshiriki kikao hicho.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer, akiwakilisha taarifa ya Mkoa wa Mbeya ikijumuisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mahakama za Wilaya na Mahakama zake za Mwanzo.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni