Na FRANCISCA SWAI – Mahakama Musoma.
Mahakama Kanda ya
Musoma hivi karibuni, imefanya mkutano wa Baraza la Wafanayaka kwa mwaka 2026
na kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji.
Akifungua Baraza
hilo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mhe. Fahamu Mtulya, aliwasisitiza wajumbe wote kuwa
huru kueleza changamoto zao.
Mhe. Mtulya
alisema kuwa sehemu ya kutatua changamoto zilizo ndani ya uwezo wa Kanda ni
katika Baraza hilo na zile zilizo nje ya uwezo wa Kanda zichukuliwe na
kuwasilishwa kwa Mwajiri.
Alisema Baraza la
Wafanyakazi ndio sehemu muhimu ambayo Watumishi wanapata nafasi ya kuongea na Mwajiri
pamoja na Wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi, yaani TUGHE, ili kupata
ufumbuzi wa changamoto wanazokutana nazo lakini pia kujua nini Mwajiri na
Serikali kwa pamoja wanafanya ili kuboresha mazingira ya kazi.
Naye katibu wa
TUGHE Mkoa wa Mara, Bw. Hamis Mwisa, alipata wasaa wa kuelezea na kutoa elimu
juu ya mkataba mpya wa Baraza la Wafanyakazi na kutoa pongezi kwa namna
ulivyoweza kuainisha wajumbe ambao wanabeba uwakilishi mzuri wa Watumishi,
jambo litakaloongeza ufanisi na uwazi katika Mabaraza ya Wafanyakazi.
Aidha, Mjumbe wa
Baraza Kuu Serikalini anayeteuliwa na TUGHE Makao Makuu, Dkt. John Bomani, alimpongeza
Mwenyekiti wa Baraza kwa namna anavyoliendesha kwa kuzingatia kanuni za
demokrasia na kuruhusu uhuru wa maoni.
Alisema kuwa mwenendo
huo wa uwazi ni kiashiria cha mahusiano mazuri kati ya Viongozi na Watumishi,
jambo ambalo linasaidia katika kuweka mazingira bora na rafiki ya kazi.
Katika mkutano wa
Baraza hilo, wajumbe walipata nafasi ya kuelezwa kilichojiri katika Baraza la
mwaka 2025 pamoja na matokeo ya hoja zilizowasilishwa. Pia walieleza hoja
mbalimbali ambazo zilikubalika zichukuliwe na kuwasilishwa kwa Mwajiri katika Mkutano
Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania.
Pamoja na hayo,
katika Baraza hilo wajumbe walipitishwa katika taarifa mbalimbali za kiutendaji,
ikiwemo taarifa ya bajeti inayoendelea ya mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na
makisio ya bajeti ijayo ya mwaka 2026/2027, huku majukumu yaliyopangwa
kutekelezwa kwa kila ngazi ya Mahakama ndani ya Kanda yakianishwa.
Vilevile, wajumbe
wa Baraza hilo walipata nafasi ya kupendekeza na kuchagua mtumishi hodari wa
Mahakama Kanda ya Musoma, zoezi lililosimamiwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo.
Akihitimisha Baraza hilo, Mwenyekiti aliwashukuru na kuwapongeza Watumishi kwa namna walivyowasilisha hoja zao, pamoja na Viongozi wa TUGHE Mkoa wa Mara, hususan Katibu, Bw. Hamis Mwisa, kwa namna anavyojitoa kushiriki katika vikao na kutoa elimu kwa wajumbe juu ya masuala mbalimbali, ikiwemo elimu ya Mabaraza ya Wafanyakazi.
Viongozi na
wajumbe wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi, Kanda ya Musoma, wakiimba kwa
pamoja wimbo wa mshikamano daima wakati wa ufunguzi.
Katibu wa Baraza
la Wafanyakazi Musoma, Bw. Kandana Lucas, akisema neno wakati wa ufunguzi wa
mkutano huo uliofanyika hivi karibuni.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza
la Wafanyakazi Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, akisisitiza jambo wakati wa
mkutano huo.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza
la Wafanyakazi Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati), Katibu wa Baraza
la Wafanyakazi Musoma, Bw. Kandana Lucas (kushoto) pamoja na Katibu Msaidizi wa
Baraza la Wafanyakazi Musoma, Bi. Teckla Patrick, wakihesabu kura za wajumbe
wakati wa zoezi la kuchagua mtumishi hodari wa Kanda ya Musoma.
Mjumbe wa Baraza
la Wafanyakazi, Bw. Simo Lubili (aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya kikao cha
Baraza la Wafanyakazi la mwaka 2025 pamoja na majibu ya hoja zilizowasilishwa
mwaka huo.
Katibu wa TUGHE
Mkoa wa Mara, Bw. Hamis Mwisa (aliyesimama) akifafanua mkataba mpya wa Baraza
la Wafanyakazi wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma.
Mjumbe wa Baraza
Kuu Serikalini, Dkt. John Bomani, akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa mkutano
wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni