Na SOJO STEPHEN-Mahakama, Mtwara
Mahakama za Mwanzo tatu
zilizokuwa zinajengwa ndani ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara,
zimezinduliwa katika jitihada za kusogeza huduma za haki karibu zaidi na
Wananchi, hasa waliopo katika maeneo ya vijijini.
Uzinduzi huo wa pamoja
ulifanyika tarehe 27 Machi, 2026 katika Mahakama ya Mwanzo Chikundi kwa niaba
ya Mahakama nyingine za Mwanzo Kitangari na Newala Mjini na kuhudhuriwa na
Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Wadau wa sekta ya sheria.
Mgeni rasmi katika hafla
hiyo alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin
Kakolaki, akiwa ameambatana na Naibu Msajili, Mhe. Seraphine Nsana na Mtendaji
wa Mahakama ya Mtwara, Bw. Yusuph Msawana.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Mhe. Kakolaki alisema kuwa kuanzishwa kwa Mahakama hizo kutasaidia
kupunguza msongamano wa mashauri na kuharakisha utoaji wa haki kwa Wananchi.
Alisisitiza kuwa hatua
hiyo ni sehemu ya juhudi za Mahakama na Serikali kuhakikisha kila Mwananchi
anapata haki kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Aidha, aliwahimiza
Wananchi kutumia Mahakama kama njia sahihi ya kutafuta haki, badala ya kutumia
mbinu au sheria zisizo sahihi ambazo zinaweza kusababisha migogoro zaidi.
Vilevile, aliwasihi
Wananchi na Watendaji wa Mahakama kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha shughuli za Mahakama, kuharakisha utoaji
wa huduma na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mashauri.
Mhe. Kakolaki
aliwashukuru Wananchi, Viongozi wa Serikali pamoja na Wadau mbalimbali wa
kijamii kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki uzinduzi wa Mahakama hizo
zilizozinduliwa katika maeneo ya Chikundi, Kitangari na Newala Mjini.
“Napenda kuwashukuru
Wananchi, Viongozi na Wadau wote kwa kushiriki uzinduzi huu wa Mahakama za
Mwanzo za Chikundi, Kitangari na Newala Mjini. Ushiriki wenu unaonesha namna
ambavyo jamii inathamini uwepo wa huduma za haki karibu na Wananchi,” alisema.
Alieleza kuwa Mahakama ya
Tanzania ina mikakati madhubuti ya kuhakikisha Wananchi wanapata haki bila
kucheleweshwa wala kubaguliwa, na kwamba moja ya mikakati hiyo ni ujenzi wa
Mahakama za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mahakama ya Tanzania
imejipanga kuhakikisha kila Mwananchi anapata huduma ya kisheria kwa wakati na
kwa usawa. Ndiyo maana tunaendelea kujenga Mahakama za Mwanzo ili kusogeza
huduma hizi karibu zaidi na Wananchi,” aliongeza.
Naye Mtendaji wa Mahakama
Mtwara alieleza kuwa Mahakama ina mkakati wa kuendelea kujenga majengo mapya na
bora kwa ajili ya Mahakama mbalimbali nchini ili kuwezesha shughuli zote za
utoaji wa haki kufanyika katika mazingira mazuri na yenye ufanisi.
“Ujenzi wa majengo haya
ni sehemu ya mkakati wa kuboresha mazingira ya kazi kwa Watumishi wa Mahakama
na kuhakikisha Wananchi wanapata huduma za haki katika maeneo yaliyo karibu nao
na yenye miundombinu bora,” alisema.
Aidha, aliipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa juhudi zake za kuboresha miundombinu ya utoaji wa
huduma za kisheria katika jamii, akisema hatua hiyo itaongeza ufanisi na
kuimarisha imani ya Wananchi kwa Taasisi hiyo.
Vilevile, aliwasisitiza
watumishi wa Mahakama kuyatunza majengo hayo na miundombinu mingine iliyojengwa
ili yaweze kudumu na kuendelea kutoa manufaa kwa jamii pamoja na watumishi kwa
ujumla.
Kwa upande wao, baadhi ya
Wananchi waliohudhuria hafla hiyo walieleza kufurahishwa na hatua hiyo,
wakisema itapunguza umbali waliokuwa wakisafiri kufuata huduma za Mahakama.
Mbali na viongozi hao,
hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Fatima
Saidi Kubenea. Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwepo kwa
ushirikiano mzuri kati ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mahakama ili kuhakikisha
huduma za haki zinawafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Mahakama za mwanzo zitakuwa na jukumu la kusikiliza na kuamua kesi ya ngazi ya kwanza, madai kulingana na mamlaka yao kisheria. Wananchi wamehimizwa kutumia vyema fursa hiyo kwa kufuata taratibu za kisheria na kuepuka kujichukulia sheria mkononi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki, akiwasili katika viwanja vya Mahakama ya Mwanzo Chikundi.
Wageni waalikwa
walioshiriki kwenye uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo katika viwanja vya Mahakama
ya Mwanzo Chikundi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (katikati), Jaji wa
Mahakama Kuu Mtwra, Mhe. Said Ding’ohi (kulia) na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya
ya Masasi Fatima Saidi Kubenea pamoja wasikiliza taarifa ya ujenzi wa majengo
ya Mahakama.
Mtendaji wa Mahakama Kanda
ya Mtwara akitoa hotuba yake katika uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo iliyofanyika
Chikundi.
Mwakilishi wa Mkuu wa
Wilaya ya Masasi Fatima Saidi Kubenea akihutubia katika uzinduzi wa Mahakama za
Mwanzo Chikundi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki akitoa hutuba katika uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo eneo la Chikundi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki akikata utepe katika shughuli ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (kushoto,) Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya (katikati) na Jaji wa Mahakama ya Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara (kulia) kwa pamoja wakikagua ukumbumbi wa wazi wa Mahakama ya Mwanzo Chikundi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (katikati), Jaji wa
Mahakama Kuu Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi (wa pili kushoto), Naibu Msajili, Mhe.
Seraphine Nsana (wa kwanza kushoto), Naibu Msajili, Mhe. Elia Mrema (wa kwanza
kulia) na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Masasi Fatima Saidi Kubenea (wa pili
kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Kanda ya
Mtwara.
Habari hii imehaririwa na FAUSSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni