Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani
Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani wamefanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kwa mara ya kwanza likilenga kushughulikia changamoto ambazo zinaweza kutatulika katika ngazi ya Mkoa kabla ya kupeleka katika ngazi ya Kanda.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 10 Aprili, 2026
kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi amesema kikubwa
wanachoangalia kwanza ni utendaji kazi wao kabla ya mengineyo yoyote kwa sababu
utendaji kazi ndio kitu kikubwa ambacho kinasababisha mpaka wanakutana kwa changamoto
hizo.
Aidha, Mhe Mkhoi alisema wanatakiwa kujitathmini katika kikao hicho cha Baraza walipotoka, walipo na wapi wanakwenda. Katika kujitathimini wanaangalia mashauri ya mwaka 2024 ambapo kulikuwa na mashauri 2004 na kubaki na mashauri 268, amesema wakiangalia walikotoka wanaona wamefanya kazi kubwa.
Kupitia kikao hicho walipokea kero au maoni ambayo yatawapa ufanisi katika utendaji kazi wao na pia yatakayowaboreshea maslahi yao katika kazi zao za utumishi wa umma.
Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo, alisema mpaka mwaka jana, 2025 mashauri ya
mlundikano yalikuwa manne pekee na Mahakama kama nne hazikuwa na mashauri ya mlundikano,
Mahakama tatu pekee ndio zilikuwa na mashauri hayo.
Aliongeza kuwa, lengo la kikao hicho pia ni kuangalia utendaji kazi pamoja na kubaini changamoto zinazowakabili na kuona ambazo zinatakiwa kutatuliwa na zile zinazoshindikana zipelekwe mamlaka zinazofuata.
Naye Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Nestory Mujunangoma alisema kutokana na changamoto mbalimbali za kiutumishi Mahakama ya Hakimu Mkazi imeona ni bora kuwa na Baraza la Wafanyakazi la Mkoa ili kupitia hoja zinazotoka kila Wilaya na kuona namna ambavyo zinaweza kutatuliwa kimkoa na zile zinazoshindikana kuwasilishwa katika Kikao cha Baraza cha Kanda na baadae Makao Makuu.
“Hata tusingekuwa na Baraza hilo leo ingetulazimu kukutana siku moja kabla ya Kikao cha Baraza cha Kanda na baadhi ya viongozi ili kujadili changamoto lakini kama Mkoa tumeona kuna njia bora zaidi ya kuchambua changamoto na kuna zile zinazotatulika kwa ngazi ya Mkoa na zingine zinaenda Kanda,” alisema Bw. Mujunangoma.
Aliongeza kuwa, hata changamoto hizo zinapofika ngazi ya Kanda na kama yatahitajika majibu bado ni Mkoa ndio watatakiwa watoe majibu. Hivyo wameona ni bora wakazichakata na kupata hoja ambazo zitawakilishwa katika Baraza la Wafanyakazi Kanda.
Miongoni mwa hoja ambazo zilikuwa ndani ya uwezo wa Mkoa zilipata ufumbuzi na kuwekewa maazimio na utekelezaji kuanza mara moja ikiwemo watumishi wa Kada ya Wasaidizi wa Kumbukumbu kuhudhuria vikao na mafunzo ya Kada yao (TRAMPA) na Waandishi Waendesha Ofisi kuhudhuria vikao na mafunzo ya kada yao (TAPSEA).
Baada ya kikao hicho wajumbe wa Baraza hilo walipata fursa ya kupata mafunzo kuhusu Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF) na kujifunza namna ambavyo wanaweza kujua mafao yao na namna ya kuangalia michango yao na pia namna ya kufungua akaunti kiganjani.
Akizungumza wakati wa semina hiyo Ofisa kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Bi. Fatma Nzowa alitoa rai kwa watumishi kuweka taarifa zao vizuri hasa majina yao na warithi wao ili pindi akifariki warithi wasikutane na taratibu ndefu za kuchelewesha mafao au wakati wa kustaafu kusiwepo usumbufu wa kufuatilia mafao.
Aidha aliwataka wale ambao walikuwa kwenye ndoa na wameachana wafanye haraka kuwatoa wenza hao kuwa miongoni mwa warithi na pia kuwa na hati ya talaka ili kuepusha usumbufu.
Baraza hilo la Mkoa limewahusisha na kuhudhuriwa na wajumbe wanne kutoka kila Wilaya na wajumbe nane kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi.
Wajumbe wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi Pwani
wakifuatilia hotuba ya Mwenyekiti (hayupo katika picha) wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani kilichofanyika tarehe 10 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni