Na. SHARIFU MOKIWA - Mahakama, Sumbawanga
Mahakama Kuu, Kanda ya
Sumbawanga imefanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi tarehe 10 Aprili, 2026 kwa
lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Uongozi na watumishi, kuboresha
utendaji kazi na utoaji wa huduma za kimahakama.
Kikao cha Baraza hilo
kilifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Frederick
Manyanda na kuhimiza mshikamano na uwajibikaji miongoni mwa watumishi kwa
kutumia kaulimbiu ikiwemo, Mshikamano Daima (Solidarity Forever) Kazi na Utu
Tunasonga Mbele pamoja ile ya Mahakama ya Tanzania ya Uadilifu, Uweledi na Uwajibikaji.
Baraza hilo, lilitumia
kikao hicho kufanya uchaguzi wa Katibu na Katibu Msaidizi wa Baraza la
wafanyakazi ambao watachukua nafasi zilizoachwa wazi na viongozi waliopita
ambao mmoja alihama na mwengine alikuwa anatokea Mkoa wa Katavi ambako
kumeanzishwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo.
Katika uchaguzi huo, kuliwasilishwa majina mawili ya wajumbe
yaliyopendekezwa na Menejimenti ili yaweze kupigiwa kura na wajumbe wa kikao na
baada ya zoezi la uchaguzi Bw. Fredrick Mahava alichaguliwa kuwa Katibu wa Baraza
la wafanyakazi huku Bi. Bupe John akichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi wa Baraza
la wafanyakazi.
Akizungumza baada ya
kuchaguliwa Katibu wa Baraza la wafanyakazi Bw. Fredrick Mahava aliwashukuru
wajumbe kwa imani waliyoionesha kwake. “Asanteni kwa kutuchagua kuwa Katibu na
Katibu Msaidizi. Tunaahidi kushirikiana na Mwenyekiti katika kutekeleza
majukumu yetu na kuhakikisha tunatimiza majukumu tuliyopewa,” alisema.
Katika hatua nyingine,
Katibu huyo alikabidhiwa Mkataba wa Baraza la wafanyakzi kati ya Mahakama ya
Tanzania na Chama cha wafanyakazi Serikalini na afya Tanzania (TUGHE) mbele ya
wajumbe wa kikao hicho.
Aidha, zoezi hilo
lilienda sambamba na uteuzi wa Kamati Tendaji ya Baraza la wafanyakazi ambayo
inaundwa na Menejimenti yote, Mwenyekiti wa TUGHE, Katibu wa TUGHE na wajumbe
kutoka kwa wawakilishi wa wafanyakazi ambapo wajumbe hao walichaguliwa kwa
kupigiwa kura ambao walikuwa ni Bi. Veronika Garikunga kutoka Mahakama ya Wilaya
Sumbawanga, Bw. Damian Mlowezi Kutoka Mahakama ya Wilaya Kalambo, Bi. Jenifeva
Mwakanema kutoka Wilaya ya Nkasi na Bi. Atupelile Konga kutoka Mahakama Kuu,
Kanda ya Sumbawanga.
Akitolea ufafanuzi
kuhusu Baraza hilo, Afisa kazi Mkoa wa Rukwa Bw. Curthbelth Kumburu alisema
kuwa, Baraza la wafanyakazi ni chombo cha ushirikishwaji kinachomkutanisha
mwajiri na mwajiliwa kwa lengo la kupanga mipango mbalimbali na kushughulikia
changamoto zinazojitokeza mahali pa kazi.
Bw. Kumburu aliongeza
kuwa, lengo Kuu la Baraza hilo ni kuhakikisha Taasisi inasonga mbele kwa
kuwashirikisha watumishi katika kutoa maoni chanya yanayochangia maendeleo ya Taasisi.
Aidha, alibainisha
kuwa, Baraza hilo linaendeshwa kwa mujibu wa sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya
utumishi wa umma, sheria ya ajira na mahusiano kazini pamoja na sheria ya
taasisi ya kazi namba 7 ya mwaka 2024 na mkataba wa kuanzishwa kwa Baraza
husika.
Vilevile, Mtendaji wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba aliwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa majukumu 2025/2026 kwa wajumbe ikionyesha hali ya raslimali
watu, maendeleo ya kiutendaji pamoja na utekelezaji wa majukumu mbalimbali
Baraza hilo, liliwasilisha hoja mbalimbali za wafanyakazi na kujadiliwa kwa pamoja, zile ambazo zilikuwa ndani ya uwezo wa Viongozi wa Kanda zilipata majibu papopapo na zile zilizo nje ya uwezo wa viongozi wa Kanda zilipokelewa kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye Baraza Kuu litakalofanyika Makao Makuu ya Mahakama hivi karibuni.
Kikao
hicho cha Baraza la wafanyakazi kilihitimishwa kwa msisitizo wa kuendelea
kudumisha mshikamano, ushirikiano na uwajibikaji miongoni mwa watumishi ili
kuhakikisha Mahakama inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Jaji Mfawidhi Mahakama
ya Sumbawanga Mhe, Frederick Manyanda akifungua kikao cha Baraza la wafanyakazi
Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu
Essaba akiwasilisha taarifa ya utekelezaji 2025/2026 majukumu ya Mahakama.
Katibu wa Baraza la wafanyakazi Bw. Fredrick Mahava (kulia) akikabidhiwa Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi baada kuchaguliwa kuwa Katibu wa Baraza hilo na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba (kushoto)
Wajumbe wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wakiimba wimbo kuonesha
umoja na mshikamno.
Afisa kazi kutoka Mkoa wa Rukwa Bw. Curthbelth Kumburu akitoa ufafanuzi
kuhusu Baraza la Wafanyakazi.
Wajumbe wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wakiimba wimbo kuonesha
umoja na mshikamno.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni