Na AMANI MTINANGI, Mahkama-Tabora
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imeikumbusha jamii juu ya
thamani ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya Usuluhishi ikiwa ni kuashiria kuanza
kwa Wiki ya Usuluhishi nchini.
Uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi kwa upande wa Tabora ulifanyika tarehe 09
Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora na kuongozwa na
Naibu Msajili wa Kanda hiyo, Mhe. Rhoda Ngimilanga, ambaye alisisitiza kuwa,
usuluhishi si njia dhaifu ya haki, bali ni njia iliyopevuka inayorejesha utu na
uhusiano kati ya pande zinazozozana.
Hotuba kutoka kwa Wawakilishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi
ya Mashtaka ya Taifa, pamoja na Ofisi ya Mawakili wa Kujitegemea Tabora
zilijenga hoja kwamba jamii inayochagua usuluhishi hujijenga yenyewe kwa sababu huweka mbele maelewano kuliko mashindano.
Mwanafalsafa wa kale Socrates aliwahi kusema, “Si kushinda hoja ndiko
kunakomfanya mtu awe na haki, bali kuelewa ukweli.” Kauli hii inapata uhai
wake katika dhana ya usuluhishi—ambapo lengo si kumuangusha mwenzako, bali kumuinua
pamoja nawe, sawa na Aristotle
alitufundisha kuwa, “Haki ni usawa uliopimwa kwa busara.” Katika
muktadha huu, usuluhishi huwa mizani inayosawazisha pande mbili bila
kupendelea, bali kwa kuzingatia utu na
ridhiko la wadaawa.
Hata katika mila za Kiafrika, kuna msemo unaosema: “Mti hauanguki kwa
kelele, bali kwa shoka la kimya.” Hii ni taswira ya usuluhishi nguvu yake iko katika utulivu wake wa kina wa pande zote unaoakisi lengo la kujenda pamoja palipovunjika. Ni katika mantiki hiyo ndipo Wiki ya Usuluhishi inapata uzito wake. Sio
tu jukwaa la kusikiliza mashauribali ni darasa la jamii kujifunza kuwa,
migogoro si mwisho wa uhusiano bali ni mwanzo wa kuelewana.
Hafla hiyo ya uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi Mahakama Kanda ya Tabora ilihudhuriwa pia na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel Munda na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, Mhe. Gabriel Ngaeje, ujumbe mmoja ulijitokeza wazi: haki haipaswi kuwa safari ya mateso, bali mchakato wa uponyaji.
Wiki ya Usuluhishi itaendelea hadi tarehe 17 Aprili, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Tabora. Lakini kwa wanaotafakari kwa kina, somo lake linaweza kudumu zaidi ya wiki moja kama alivyowahi kusema Confucius, “Amani ya kweli haiji kwa ukosefu wa migogoro, bali kwa uwezo wa kuisimamia kwa hekima.”
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Rhoda Ngimilanga akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi Tabora iliyofanyika tarehe 09 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, Mhe. Gabriel Ngaeje akielezea kuhusu mwelekeo wa usuluhishi na umuhimu wake katika kuleta amani na haki kwa jamii wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi Tabora uliofanyika tarehe 09 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora.
Washiriki waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi wakisikiliza kwa makini hotuba mbalimbali za Viongozi waliozungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika tarehe 09 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel Munda akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi Tabora.
Mwakilishi kutoka Baraza Usuluhishi na Uamuzi, Mhe. Magreth Shimbi akitoa neno.
Mwakilishi wa Ofisi ya Wakili wa Serikali, Wakili Samwel Mahuma akizungumza kuhusu umuhimu wa usuluhishi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi Mahakama Kanda ya Tabora iliyofanyika hivi karibuni.
Wakili Flavia Fransis, Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) akizungumzia kuhusu nafasi na umuhimu wa Usuluhishi katika kutatua migogoro wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi Tabora.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni