Jumatatu, 20 Aprili 2026

'TUMIENI UJUZI WA USULUHISHI MLIOUPATA KUISAIDIA JAMII KUMALIZA MIGOGORO KWA AMANI'

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa amewataka washiriki wa mafunzo ya Usuluhishi ambao ni Mahakimu kutoka Kigoma, Bukoba, Musoma na Mwanza kutumia ujuzi walioupata kuisaidia jamii kumaliza migogoro yao kwa amani na utengamano.

Mhe. Mbelwa aliyasema hayo hivi karibuni mkoani Kigoma wakati akifunga mafunzo ya Usuluhishi yaliyoendeshwa kwa siku tano na kuhudhuriwa na washiriki 16. 

“Tumieni ujuzi huu wa usuluhishi kuisaidia jamii kutatua migogoro kwa njia ya amani ili kuleta utengamano wa kijamii ili kupunguza utitiri wa migogoro katika Mahakama zetu na hii itaboresha upatikanaji haki kwa wananchi,” alisema Mbelwa.

Alibainisha kuwa, mafunzo hayo yamefanikiwa kwani washiriki wamepewa mbinu zote muhimu za usuluhishi, hivyo ni matarajio ya Mahakama na Jamii kwa ujumla wake kuona wanatumia vema ujuzi na weledi walioupata kuleta tija katika utatuzi wa migogoro Mahakamani ili kupunguza mashauri.

Aidha, alifafanua kuwa, mafunzo hayo yamefanyika sambamba na Wiki ya Usuluhishi Kitaifa, huku akitoa pongezi kwa washiriki ambavyo wameshiriki vema Wiki ya Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi, ambapo wametumia weledi walioupata kufanya usuluhishi na umeleta tija kwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma kwa mashauri waliyosimamia ambayo usuluhishi wake umefanikiwa.

Aidha, alimshukuru Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju kukubali mafunzo hayo yafanyike Kigoma na washiriki kutoka maeneo tajwa walioshiriki katika mafunzo hayo.

Vilevile alimshukuru Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo kwa kuridhia Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa kuwa Wawezeshaji wa Mafunzo hayo ya Usuluhishi.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Nyamagana, Mhe. Ramla Shehagilo alitoa shukrani kwa niaba ya washiriki, ambapo aliwashukuru Wakufunzi wa Mafunzo hayo sambamba na Waandaaji wa mafunzo hayo ambao ni Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) pamoja na Mahakama ya Tanzania kwa kuwachagua wao kuwa washiriki wa mafunzo ya usuluhishi katika Wiki ya Kitaifa ya Usuluhishi.

Naye, Hakimu Mkazi na Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Husna Rweikiza akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Chuo IJA, Mhe. Dkt. Kihwelo alibainisha kuwa washiriki wamejifunza mbinu zote za usuluhishi hivyo, malengo ya mafunzo hayo yamefikiwa, na kubainisha kuwa wasuluhishi hao watakuwa na tija katika kuongeza juhudi za kuimarisha ufanisi na upatikanaji wa haki Mahakamani.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ Tanzania).


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akitoa hotuba ya kufunga Mafunzo ya Usuluhishi yaliyofanyika kwa siku tano Mahakama Kuu Kigoma.

Jaji Mfawidhi Mahakama Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akitoa neno kwa washiriki siku ya mwisho wa Mafunzo ya Usuluhishi yaliyofanyika kwa siku tano mkoani Kigoma. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa na kushoto ni Bi. Rose Nyatega kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ Tanzania).

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa  Mahakama ya Wilaya Nyamagana, Mhe. Ramla Shehagilo akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wote wakati wa kufunga Mafunzo ya Usuluhishi yaliyofanyikia Mahakama Kuu Kigoma.

Hakimu Mkazi na Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Husna Rweikiza akitoa neno kwa niaba ya Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto wakati wa kufunga Mafunzo ya Usuluhishi yaliyotolewa kwa washiriki 16 kutoka Mahakama Kigoma, Bukoba, Musoma na Mwanza.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanznaia Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (kulia) akitoa cheti kwa moja ya washiriki wa Mafunzo ya Usuluhishi wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyowahusisha washiriki 16 kutoka 
Kigoma, Bukoba, Musoma na Mwanza.

Picha ya pamoja baada ya kufunga Mafunzo ya Usuluhishi yaliyofanyika Mahakama Kuu Kigoma.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni