Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Veronica John ametoa elimu kwa wananchi kuhusu kutumia njia ya usuluhishi katika utatuzi wa migogoro mingi inayojitokeza katika jamii akieleza kuwa inaleta amani, utengamano wa kijamii na kudumisha udugu miongoni mwa jamii.
Bi. Veronica amesisitiza hayo hivi karibuni wakati akitoa elimu kwa wananchi waliokuwa wakisubiri kupata huduma mbalimbali Mahakama Kuu Kigoma.
Aidha, aliwajulisha wananchi hao kuwa, zipo njia nyingi za kutatua migogoro katika jamii ikiwemo njia ya Usuluhishi, amesema, “njia hii inapendelewa kwa kuwa inaleta maridhiano ya pamoja kwa amani bila kuathiri haki ya mtu katika mgogoro husika.”
Bi. Veronica amewaeleza wananchi hao kuwa, njia ya usuluhishi ina faida nyingi kuliko njia nyingine za utatuzi wa migogoro katika jamii, ambapo amesema kuwa, usuluhishi unadumisha udugu na ushirikiano wa jamii kuliko njia nyingine, upatikanaji haki kwa njia ya kirafiki na kucheka na kuendelea kushirikiana kwenye mambo kadhaa, kupunguza gharama za wananchi katika kuendesha mashauri Mahakamani kwakuwa usuluhishi hauhitaji Wakili wala gharama za vikao kwa msuluhishi kwani Mahakama inao utajiri wa wasuluhishi kutoka ndani na nje ya Mahakama.
Kwa upande wake Bw. Bakari Abdallah Mfaume, Mkazi wa Gungu, ameishauri Mahakama kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wananchi kufahamu zaidi faida za usuluhishi ili kuleta amani zaidi katika migogoro ya Ardhi, ikiwa ni pamoja na kuona eneo la mgogoro ili kuweza kung’amua kiini cha mgogoro na kuutatua kwa njia ya amani.
Elimu ya usuluhishi iliyoanza tarehe 13, Aprili 2026 hadi tarehe 17 Aprili, 2026 ilitolewa vema katika Vituo vya Mahakama Kuu Kigoma, Mahakama za Wilaya Kigoma, Kibondo, Kasulu, Uvinza, Kakonko na Buhigwe ikienda na sambamba na utoaji elimu kupitia Redio ambapo Wilaya hizo zilishiriki kuwahabarisha wananchi kuhusu Wiki ya Usuluhishi iliyofanyika katika Mahakam azote nchini.
Mwanachama wa Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS) Bi. Veronica John akifafanua jambo hivi karibuni alipokuwa akitoa elimu ya Usuluhishi kwa wananchi Mahakama Kuu Kigoma.
Mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bi. Veronica John akisisitiza jambo
alipokuwa akitoa elimu ya usuluhishi kwa wananchi Mahakama Kuu Kigoma hivi karibuni.
Sehemu ya wananchi wakisikiliza
kwa makini elimu iliyokuwa ikitolewa na Wakili Veronica John,
Mahakama Kuu Kigoma.
Mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bi. Veronica John akisikiliza kwa makini swali alilokuwa akiulizwa na mmoja wa wananchi wakati alipokuwa akitoa elimu ya usuluhishi kwa wananchi hao hivi karibuni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni