Jumanne, 28 Aprili 2026

WAJUMBE BARAZA LA WAFANYAKAZI KIGOMA KUWAJIBIKA IPASAVYO

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutumia kikao hicho kama jukwaa muhimu la majadiliano ya wazi ili kuimarisha uwajibikaji, uwazi na ushirikishwaji wa waatumishi katika masuala ya kiutumishi.

Mhe. Rwizile aliyasema hayo hivi karibuni kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma wakati akiongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Kigoma kilicholenga kujadili ustawi wa Watumishi, tathmini ya utekelezaji wa maazimio yaliyopita na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi wa Taasisi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Jaji Rwizile alisisitiza umuhimu wa Baraza kama chombo cha kushauri na kuimarisha mahusiano kazini kwa kuzingatia mkataba mpya unaolenga kuboresha maslahi ya mwajiri na watumishi wake.

Jaji Mfawidhi huyo alieleza kuwa, “Baraza hili lipo kisheria na mkataba mpya umejikita katika kujenga Taasisi yetu kwa pamoja, hivyo mawazo yenu ni msingi wa maboresho tunayoyahitaji katika usimamizi wa shughuli za usimamizi wa usikilizwaji mashauri katika Mahakama zetu.”

Hata hivyo, aliwajulisha wajumbe kuwa, kupitia kikao hicho kulikuwa na ajenda ya uchaguzi wa Viongozi wapya wa Baraza kwa mujibu wa mkataba mpya wa Baraza la Wafanyakazi, hivyo aliwashukuru na kuwaaga Viongozi wa Baraza waliopita amba oni Mhe.  Victor Kagina, aliyekuwa Katibu na Bi. Naomi Chawe aliyekuwa Katibu Msaidizi wa Baraza hilo.

Zoezi la uchaguzi liliongozwa na Ofisa Kazi, Bw. Frank Kimaro ambaye alisisitiza taratibu za uchaguzi kuwa wazi na shirikishi kwa wajumbe wote kwa  mujibu wa Mkataba.  

Baada ya zoezi la kupiga kura kukamilia, Msaidizi wa Kumbukumbu, Bw. Julius Manyanya alichaguliwa kuwa Katibu mpya wa Baraza hilo na  Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Mburalina Maira aliteuliwa kuwa Katibu Msaidizi na Bi. Naomi Chawe alichaguliwa kuwa Mwakilishi TUGHE Baraza la Wafanyakazi Taifa.

Katika tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita, Baraza liliridhishwa kubaini kuwepo kwa hatua kadhaa zenye tija zinazoonesha juhudi za uongozi katika kuboresha ustawi wa watumishi na ufanisi wa utendaji kazi.

Aidha, Watumishi waliibua hoja ya kuchelewa kupandishwa madaraja, hususan kwa wale walio kwenye ajira za muda mrefu. Katika mjadala, ilisisitizwa kuwa, watumishi wanapaswa pia kujitahidi kujiendeleza kielimu ili kukidhi vigezo.

Wajumbe wa Baraza hilo wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka 2025/2026, huku wakichukua hatua za haraka na za kimkakati kushughulikia mara tu changamoto zilizobainika ili kutatuliwa.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akitoa neno la ufunguzi wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kigoma kilichofanyika hivi karibuni.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala  Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (kulia) akimkabidhi Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi Katibu wa Baraza mpya, Bw. Julius Manyanya mara baada ya kuibuka mshindi katika nafasi hiyo kwa kupata kura nyingi za kishindo kutoka kwa wajumbe.


Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Mahakama Kigoma wakifuatilia kwa makini mjadala ulikuwa ukiendelea wakati wa kikao cha Baraza hilo.


Ofisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanznaia Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Festo Sanga akiwasilisha taarifa ya utendaji wa shughuli za kimahakama kwa mwaka 2025/2026.

Ofisa Kazi, Bw. Frank Kimaro akitoa ufafanuzi juu ya utaratibu wa uchaguzi wa Viongozi wapya wa Baraza la Wafanyakazi wa  Mahakama Kigoma.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni