Alhamisi, 21 Mei 2026

MAHAKAMA YAOKOA ZAIDI YA BILIONI TATU

Na HABIBA MBARUKU na JAMES BUSANYA - Mahakama Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, amesema kuwa Mahakama ya Tanzania, kwa kipindi cha mwaka Jnuari, 2021 hadi Aprili, 2026 imeokoa jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 3.6 wakati ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ishara ya kuwa imara katika matumizi na usimamizi wa fedha za Umma.

Prof. Ole Gabriel ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi ya Mahakama mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyofanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Jijini Dodoma tarehe 20 Mei, 2026 ili kupata uzoefu wa Mhimili wa Mahakama katika kusimamia miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani na za Nje.

Akizungumza wakati wa wasilisho lake, Prof. Ole Gabriel ameeleza kuwa Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kusimamia matumizi ya fedha kwa ufanisi, ambapo kwa kipindi kilichotajwa zaidi ya miradi ya ujenzi wenye thamani ya Tsh Biliopni 460 ilitekelezwa.

Aidha, Mtendaji Mkuu amefafanua kuwa katika hatua ya kwanza Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kujenga majengo ya kwanza ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita katika Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mwanza pamoja na Arusha vilivyogharimu zaidi ya bilioni 51.

Katika hatua nyingine, Prof. Ole Gabriel ameeleza kuwa Mahakama imepiga hatua kubwa katika mapinduzi ya kidigitali ambayo yameokoa gharama na kupunguza matumizi ya fedha, huku maboresho katika majengo, hasa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki ambavyo vimeongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma pamoja na taarifa. Akitolea mfano wa Kitumo Jumuishi ambapo Mahakama za ngazi zote zinapatikana katika jengo moja.

Mtendaji MKuu alibainisha kuwa hii inamfanya mwananchi kukata rufaa kwenye Mahakama ya ngazi ya juu ambayo ipo kwneye jengo hilohilo sekafu inayofuatia. Ifahamike kuwa kwenye Kitua Jumuishi, Mahakam ya mwanzo inakuwa sakafu ya chini, Mahakama ya Wilaya Sakafu ya kwanza, Mahakama ya Hakimu Mkazi Sakafu ya Pili, Mahakama Kuu sakafu ya Tatu.

Kadhalika, Prof. Ole Gabriel ameainisha miradi iliyokamilika ni Pamoja na vituo vingine Jumuish 9 na kwamba kwa kujumlisha na zile 6 za awali sasa kunakuwa na vituo jumuishi 15 Nchini kikiwepo cha Pemba, Zanzibar.

Sambamba na hilo, amesema kuwa Mahakama inazidi kusogeza huduma karibu na mwananchi kwa kuendelea kujenga miundombinu ya majengo katika maeneo mbalimbali nchini, na kwamba katika Wilaya 139 Nchini tayari kuna Mahakama za Wilaya katika Wilaya 137.

Prof. Ole Gabriel ameweka wazi kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Mihimili mingine ya Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali, hususan TAMISEMI ili kutimiza azma ya kujenga Mahakama katika kila kata nchini ambapo kwa sasa Tanzania ina Kata 3,956.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Mashimba Ndaki (MB) ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga katika maendeleo, hususan katika matumizi ya TEHAMA.

Mhe. Ndaki amesema, Mhimili wa Mahakama ni mfano wa kuigwa katika usimamizi za rasilimali za Umma na pia Matumizi ya TEHAMA kwa viwango vya kimataifa.

Aidha Mwenyekiti amesisitiza kuwa ni vyema Taasisi nyingine za Umma zifike Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania kujifunza jinsi ambavyo mifumo ya TEHAMA ya Mahakama inasomana vizuri ambapo hata yeye aliweza kuona hali ya jengo la Mahakam ya Mwanzo kwenye jimbo lake akiwa ndani ya chumba cha TEHEMA Jumuishi (Judiciary Situation Room).

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi ya Mahakama mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyofanya ziara yake ya kikazi Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jana tarehe 20 Mei, 2026.


Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakisikiliza wasilisho la Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel, katika ziara yao ya kikazi waliyoifanya jana tarehe 20 Mei, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.


Sehemu nyingine ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakisikiliza wasilisho la Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel, katika ziara yao ya kikazi waliyoifanya jana tarehe 20 Mei, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakifuatilia maelezo ya Chumba Maalumu cha Mifumo ya Utoaji Taariza za Mahakama (Judicial Situation Room).

Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mashimba Ndaki (aliyeshika kisemeo, MB) katika Chumba Maalumu cha Mifumo ya Utoaji Taarifa za Mahakama (Judicial Situation Room).

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati wanawasili Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jana tarehe 20 Mei, 2026 kwa ziara ya kikazi.



Picha ya pamoja baada ya ziara hiyo.








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni