· Awataka watumishi wa Mahakama kuendelea kutekeleza Kaulimbiu ya Siku ya Sheria, 2026
· Ataka mashauri yasikilizwe mapema ipasavyo ili kuchangia ustawi na maendeleo ya Taifa
· Asisitiza ushirikiano, amani na kuthaminiana kwa Watumishi
Na MARY GWERA-Mahakama,
Dodoma
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama, amewataka Viongozi wa Mahakama kuwa wanyenyekevu
sambamba na kufungua milango kwa ajili ya kuwasikiliza Watumishi walio chini
yao ili kutatua changamoto wanazokabiliana nazo bila vikwazo.
Mhe. Masaju ametoa wito
huo leo tarehe 13 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma alipokuwa
akifungua Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania.
“Kadri unavyokuwa na Madaraka
makubwa ni kwa kiwango hicho hicho unakuwa mtumishi wa wote, sisi Viongozi ni
Watumishi wa watu, tuwe na tabia ya kufungua milango tuwasikilize walio chini
yetu, tusifunge milango,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu amesema
Viongozi pia wanawategemea Watumishi walio chini yao ambapo ameeleza kuwa, kwa
kadri Kiongozi anavyozidi kupanda kimadaraka ni kwa kiwango hicho hicho anazidi
kuwa tegemezi kwa watu wengine, na kwamba kadri unavyokuwa na Madaraka makubwa
ni kwa kiwango hicho hicho unapaswa kuwa mnyenyekevu ili uwafikie
wanaokutegemea na wao wakufikie ili ujue changamoto zao na mafanikio yao.
Kadhalika, Mhe. Masaju
amesema kuwa, Viongozi wasiwazuie wajumbe wa Baraza kuzungumza yale yanayowasibu,
badala yake wawaache huru kusema yale wanayokabiliana nayo katika utekelezaji
wa majukumu yao ili kupata ufumbuzi wa utekelezaji mzuri wa majukumu ya
Mahakama.
Ameongeza kuwa, hata
Viongozi wanapotembelea Mahakama mikoani Viongozi wa Mahakama husika wanapaswa
kuwaacha watumishi wazungumze na Viongozi ili wajue Mahakama imepiga hatua gani
katika maendeleo, wajue changamoto zilizopo
ili tutatue changamoto hizo na kupiga hatua ili hatimaye vikao vya Baraza viwe
vya furaha.
Aidha, Jaji Mkuu
amewapongeza watumishi wa Mahakama wa Kada zote kwa utekelezaji mzuri wa
majukumu ya Mhimili huo kwa ufanisi ipasavyo.
“Kwanza natambua mchango
wenu, kila mmoja wetu katika utendaji wa Mahakama ya Tanzania, mmefanya kazi
kubwa sana, miaka iliyopita na mimi tangu nimekuja kushirikiana na ninyi
mmefanya kazi kubwa sana ya kutekeleza majukumu yenu na wakati fulani katika
mazingira magumu mimi naelewa katika utumishi wangu mimi nimeanzia chini sana
nikiwa Wakili wa Serikali Daraja la tatu, kwahiyo ninafahamu na wakati mwingine
Katika upande mwingine,
Mhe. Masaju amewakumbusha Viongozi na watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla kuendelea
na utekelezaji wa Kaulimbiu ya Siku ya Sheria Nchini ya mwaka huu 2026 isemayo;
‘Mchango wa Mahakama ya Tanzania katika Maendeleo na Ustawi na Maendeleo
ya Taifa.’
“Mahakama ina mchango
mkubwa sana, mnaweza kurejea hotuba yangu ya Siku ya Sheria, nimeeleza yote,
hii haiwezi kuwa ni Kaulimbiu ya Siku ya Sheria, hii tunaiishi mwaka huu wote
wa 2026, kwahiyo tunapofanya kazi yatupasa tujue tuna mchango katika ustawi na maendeleo
ya Taifa la Tanzania. Wajibu wetu Mahakama ni kuendelea kutekeleza majukumu
yetu kwa ufanisi ipasavyo na tunapaswa kuendelea kuwa wabunifu,” amesema Jaji Mkuu.
“Kwenye Kanda mtaangalia
mnapopanga mashauri mjue kuna kitu tunafanya, kwahiyo mnatakiwa kuangalia
ustawi na maendeleo ya Taifa, tunahusika hata sisi katika maendeleo kwa sababu
amani ni msingi mkubwa unaoleta ustawi na maendeleo ya Taifa,” amesema Mhe.
Masaju.
Ameeleza kuwa, kwa msingi
huo ndio maana wa mfano kuna mashauri ya jinai, mashauri ya madai, mashauri ya
uchaguzi na kila aina ya mashauri yanashughulikiwa na kumalizika watu wanapiga
hatua mapema.
“Mpaka sasa kwa mfano yale
mashauri ya uchaguzi yaliyofunguliwa, limebaki shauri moja tu, mengine yote
yameshaisha, kuna mashauri ya kila aina ya mirathi, ya ndoa, ya uhujumu uchumi.
Sisi kama Mahakama wajibu wetu ni upi? najua tunazo changamoto pengine hatupati
ushirikiano mzuri sana lakini sisi hatuwezi kukata tamaa ndio wajibu wetu,
tukiharibu tunawajibishwa sisi, sisi ndio tunaosemwa na tunapaswa tuendelee
kuwa wabunifu katika maeneo yetu ya kazi kuhakikisha kwamba mchango wa Mahakama
ya Tanzania katika ustawi na maendeleo ya Taifa unazidi kuimarika,” amesisitiza
Jaji Mkuu.
Amesema, tunaishi katika
nchi inayozingatia Utawala wa Sheria, hivyo, Mahakama ina nafasi kuwa katika
ustawi na maendeleo ya Taifa na kwa sababu ni muhimu mashauri yanapopangwa yapangwe
kimkakati na hayatakiwi kucheleweshwa bila sababu za msingi, lakini pia inabidi
kuwa ni mikakati ya kubaini mashauri yenye kero yanayoleta sintofahamu katika
jamii yashughulikiwe.
“Uchumi ni Ardhi wala
hata sio kitu kingine, kwahiyo tuna mikakati ya kumaliza haya mashauri ya Ardhi
tangu mwaka jana tumekuwa na hiyo mikakati, na Mahakama Kuu wamefanya vizuri
sana kwa sababu mashauri ya ardhi kwa Mahakamani yanaanzia Mahakama Kuu, yanakwenda
Mahakama Rufaa mengine kwenye ‘originial jurisdiction’ tunafanya vizuri japo bado
ni mengi kwa sababu migogoro inazalishwa mingi na sehemu fulani tumeshauri kwa
mfano ukisoma Sheria ya Usajili wa Ardhi (Land Registration Act) kuna mtu pale
anaitwa ‘The Registrar of Titles) ana mamlaka makubwa sana mashauri mengine hata yasingekuwa yanakuja
mahakamani yangekuwa yanaenda pale kama kuna migogoro wakishindwa kutatua
upande ambao hauridhiki unakuja Mahakama ya Rufani,” ameeleza.
Kwa upande wa Mahakama ya
Rufani, Mhe. Masaju amesema kuna mashauri mengi ya jinai, hivyo wameweka
mkakati wa kushughulikia mashauri hayo ambayo walianza kusikiliza katika Vikao
vya Mahakama ya Rufani (COA Session) ya mwezi Februari ambapo walichanganya na
mashauri ya mirathi ili watu wawe na amani kwenye familia zao na wengine wajue
hatma yao.
“Majaji hawa wa Mahakama
ya Rufani wamefanya kazi nyuma, mashauri mengi yameenda, kama wengine hawasema
sisi wenyewe tujisemee, mimi nawapongeza sana Mahakama ya Rufani,” amesema Jaji
Mkuu.
Ameongeza kuwa, Mwezi
Aprili walipanga mashauri ya kazi na ndoa ambayo kikao chake kimekamilika tarehe
08 Mei, 2026 na wengine wanaendelea, jitihada hizo ni katika wajibu wa
kutekeleza mchango wa Mahakama katika maendeleo na ustawi wa Taifa.
Kadhalika, amesema katika
Vikao vinavyofanyika Juni na Agosti, 2026 mashauri ya ardhi yatashughulikiwa
tena ili kuyapunguza. Ameeleza kuwa, katika vikao hivyo wataweka pia mashauri
machache ya jinai na kabla ya Desemba pia watakuwa na mashauri ya jinai.
Amebainisha kuwa, ili
Mahakama ifanikiwe inahitaji ushirikiano kutoka Mihimili mingine ili kutekeleza
jukumu la utoaji haki kwa ufanisi ipasavyo.
Kwa upande wa Mahakama
Kuu, Mhe. Masaju amesema, wamekamilisha vikao vya kusikiliza mashauri ya ardhi
ikiwa ni mwendelezo wa zoezi ambalo lilianza mwaka jana, ambapo amesema kwa
sasa hatatoa takwimu kwakuwa zinaandaliwa na Msajili wa Mahakama Kuu na
zitatangazwa kwa wananchi kile ambacho Mahakama imefanya.
Amesema pia kulikuwa ni shida kubwa za mashauri ya baadhi ya waajiri kutowasilisha michango ya mafao ya watumishi wao katika mifuko ya hifadhi za jamii ambapo amesema wamefanya mabadiliko ya kanuni na kwamba katika usikilizaji wa mashauri hayo Majaji na Mahakimu wamefanya vizuri kwakuwa mashauri hayo mengi yameisha na yameisha kwa njia ya usuluhishi.
“Sisi Mahakama nia yetu ni kwamba wafanyakazi wapate stahili zao sio wanakatwa halafu mwisho wa siku hawapewi stahili zao,” ameeleza.
Kadhalika Jaji Mkuu
amewataka watumishi wote wa Mahakama kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano,
umoja na kuthaminiana katika utekelezaji wa majukumu.
Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Ezra Kyando akizungumza jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama lililofunguliwa leo tarehe 13 Mei, 2026 na Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha).
Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kushoto) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (wa pili kushoto) wakiwa katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama nchini ulioanza leo tarehe 13 Mei, 2026. Mkutano huo unatarajiwa kuhitimishwa kesho tarehe 14 Mei, 2026.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija (wa pili kushoto), Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wa pili kulia), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (wa kwanza kushoto) na Katibu Msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama, Mhe. Christina Mlilwo.
Wimbo wa Mshikamano Daima (Solidarity Forever) ukiimbwa na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania.
(Picha na Mary Gwera-Mahakama)























Hakuna maoni:
Chapisha Maoni