Jumatano, 13 Mei 2026

MAHAKAMA YAENDELEA KUIMARISHA UTOAJI HAKI

  • Yataja mafanikio ya utumishi, TEHAMA na Miradi ya Ujenzi
  • Mtendaji Mkuu aeleza mafanikio ya ajira, ustawi wa Watumishi

Na HALIMA MNETE- Mahakama, Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, amesema kuwa Mahakama inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za haki nchini kupitia maboresho mbalimbali ya kiutumishi, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa majengo katika maeneo tofauti ya nchini.

Prof. Ole Gabriel amesema hayo leo tarehe 13 Mei, 2026 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya mwaka wa fedha 2025/2026 katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania 2026 unaofanyika katika ukumbi wa PSSSF Makole, chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju.

Akizungumza katika mkutano huo utakaohitimishwa kesho tarehe 14 Mei, 2026, Prof. Ole Gabriel amesema Mahakama imeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wake wenye lengo la kuendeleza maboresho ya utoaji huduma, huku mafanikio yaliyopatikana yakitokana na juhudi za Watumishi wa Mahakama nchini kote.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Mahakama imefanikiwa kuajiri Watumishi wapya 1,121, wakiwemo Mahakimu 173, hatua ambayo imeongeza nguvu kazi katika utoaji wa huduma za haki nchini. Hata hivyo, amesema bado Mahakama inakabiliwa na upungufu wa Watumishi ambapo hadi Aprili 30, 2026 idadi ya watumishi waliopo ni 6,976 dhidi ya mahitaji ya watumishi 12,121.

“Tumekuwa na kikao kizuri na Viongozi wa TUGHE Mahakama, ambapo hoja nyingi zimejadiliwa na baadhi yake zimepatiwa ufumbuzi,” amesema Prof. Ole Gabriel.

Katika masuala ya ustawi wa watumishi, amesema Mahakama imetenga zaidi ya shilingi milioni 900 kwa ajili ya kuanzisha kifurushi maalum cha bima ya afya kwa Watumishi wake ili kusaidia huduma za ziada za matibabu.

Kuhusu miundombinu. Prof. Gabriel amesema Mahakama inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi, ikiwemo ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama Dodoma ambao umefikia asilimia 99.

Amesema pia Mahakama imeendelea kujenga na kukarabati majengo ya Mahakama katika Mikoa mbalimbali, huku baadhi ya majengo mapya ya Mahakama Kuu yanayoitwa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki tayari yakianza kutumika katika Mikoa mbalimbali.

Kwa upande wa TEHAMA, Prof. Ole Gabriel amesema Mahakama itaendelea kuimarisha mifumo mbalimbali pamoja na mfumo wa Mahakama Mtandao (Virtual Court) ili kuongeza ufanisi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa Wananchi.

Amesisitiza kuwa matumizi ya TEHAMA yanapaswa kuendelea kuwa sehemu ya utamaduni wa Mahakama ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Katika hitimisho lake, Prof. Ole Gabriel ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuipa Mahakama kipaumbele katika utoaji wa bajeti na kuwataka Watumishi kuendelea kushirikiana katika kuimarisha utoaji wa haki nchini.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Wafanyakazi Mahakama ya Tanzania 2026. Picha chini ni sehemu ya wajumbe kutoka Masjala mbalimbali wanaohudhuria Mkutano huo.












Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni