Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Jaji
wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji
na Tathmini, Mhe. Barke Sehel hivi karibuni alifanya ziara ya kikazi Mahakama Kuu
Masjala Ndogo ya Njombe lengo likiwa ni kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa
shughuli za Mahakama.
Mhe.
Sehel ambaye pia ni na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake
Tanzania (TAWJA) alianza ziara yake tarehe 07 Mei, 2026 ambapo alipokelewa na
mwenyeji wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya
Njombe, Mhe. Victoria Nongwa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa TAWJA pamoja na
Viongozi na watumishi watumishi wa Mahakama Njombe.
Jaji
Sehel alipata wasaa wa kuzungumza na watumishi wa Mahakama Njombe ambapo
alisikiliza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwemo ukosefu wa huduma
ya usafiri wa basi la Mahakama linaloweza kuwapeleka ofisini kutokana na umbali
mkubwa wa kutoka maeneo wanayoishi mpaka mahali pa kazi.
Aidha, Mwenyekiti huyo alipata fursa ya
kutembelea jengo la Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Njombe (IJC) ambalo lipo kwenye
hatua za mwisho kwa asilimia 97 na baadhi ya viongozi na watumishi tayari
wameanza kuhamia kwenye jengo hilo.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti alifanya ukaguzi
wa shughuli za kimahakama katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mahakama ya Wilaya
ya Njombe na Makete pamoja na Mahakama ya Mwanzo Njombe.
Vilevile,
katika ziara hiyo Mhe. Sehel alipata fursa ya kuzungumza mambo mbalimbali ya TAWJA
Njombe katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake pamoja na kuhuisha
uanachama wa TAWJA na IAWJ.
Akiendelea na kikao hicho huku wanachama
wengine wakishiriki kwa njia ya mkutano mtandao (Video Conference) walio nje ya
Wilaya ya Njombe, Mhe. Sehel alisisitiza
mshikamano pamoja na kushirikiana kikamilifu katika shughuli za Chama hicho, Tawi
la Njombe ikiwa ni pamoja na kujitolea katika majukumu mbalimbali bila kujali
malipo pamoja na kutoa elimu na kuhudhuria mikutano ya ndani.
Mwenyekiti huyo wa TAWJA alisisitiza kuwa Chama
hicho ni jukwaa linalowawezesha kung’ara kitaifa na kimataifa kwa kazi zinazofanyika,
ambapo aliwatakia wanachama wa TAWJA Njombe majukumu mema ya ujenzi wa Taifa
huku akisisitiza uadilifu, weledi na uwajibikaji kama ambavyo Kaulimbiu ya
Mahakama inasema.
Mhe, Sehel pamoja na wanachama wa TAWJA Njombe
walipata fursa ya kukata keki na kufungua champeni pamoja na Makamu Mwenyekiti
Mhe. Victoria Nongwa kama ishara ya mwanzo mpya wa TAWJA mkoani Njombe.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Jaji Mkuu ya Ufuatiliaji na Tathmini, Mhe. Barke Sehel akipatiwa maelezo na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Njombe, Bw. Richard Mbambe (wa kwanza kushoto). Wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa TAWJA akizungumza hivi karibuni na baadhi ya Wanachama wa Chama hicho wa mkoani Njombe.
Jaji Sehel akiwa katika maandalizi ya kukata keki maalum ikiwa ni ishara ya kuanza kwa Tawi mpya la TAWJA Mahakama Njombe.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni