Alhamisi, 14 Mei 2026

MAHAKAMA YA TANZANIA YAJIDHATITI KUBORESHA HUDUMA YA UTOAJI HAKI MAPEMA IPASAVYO

Na MARY GWERA-Mahakama, Dodoma

Mahakama ya Tanzania imetunga jumla ya kanuni mpya tano (5) na kufanyia marekebisho kanuni nane (8) na hivyo kufanya uwepo wa jumla ya kanuni 13 za uendeshaji wa mashauri, lengo likiwa ni kurahisisha mchakato wa usikilizaji mashauri ili haki iweze kupatikana mapema ipasavyo.

Hayo yamebainishwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, alipokuwa akiwasilisha Taarifa kuhusu Kazi za Kimahakama za mwaka 2025 katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama lililofunguliwa jana tarehe 13 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.

Mhe. Nkya ametaja Kanuni hizo kuwa ni pamoja na The Primary Courts-Administration of Estates) (Amendment) Rules 2025 GN No.  428 published on 11th July, 2025, The Civil Procedure Code (Amendment of the First Schedule) Rules, 2025 GN No. 569 published on 12th September, 2025.

Nyingine ni Judicature and Application of Laws (Electronic Filing) (Amendment) Rules, 2025 GN No. 39 published on 17th October, 2025, Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Madiwani za Mwaka 2025 Tangazo la Serikali Na.433 la tarehe 11 Julai, 2025, Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka 2025 Tangazo la Serikali Na.431 la tarehe 11 Julai, 2025, Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi za Mwaka 2025 Tangazo la Serikali Na. 430 la tarehe 11 Julai, 2025.

Kanuni za Marekebisho ya Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka 2025, Tangazo la Serikali Na 610 la tarehe 17 Oktoba, 2025, The Judiciary Administration Regulations (The Judiciary Administration (Judiciary Flag) (Amendment) Regulations, 2025, GN 608/2025 na nyingine.

Akizungumzia kuhusu mafanikio ya Mahakama yaliyopatikana, Msajili Mkuu ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la usikilizaji mashauri kwa asilimia tatu sambamba na kupungua kwa wastani wa mzigo wa kazi toka 227 hadi 222.

Kadhalika, Msajili Mkuu ameeleza kuwa, kumekuwa na kasi ya kupungua kwa wastani wa muda wa kumaliza shauri kutoka siku 78 hadi 66.

Kadhalika, amebainisha kwamba, Mahakama imefanikiwa kufikia malengo ya kiashiria cha kiwango cha mashauri ya mlundikano kwa asilimia tano na usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (lengo lilikuwa 18,500 - 62,041).

“Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kuanzishwa kwa Masjala ndogo tano za Mahakama Kuu, kuanzishwa kwa Vituo vya Mahakama ya Mwanzo 15,” amesema Mhe. Nkya.

Kwa upande wa kiwango cha ukaguzi wa Mahakama na Magereza, Mahakama imefanikiwa kwa asilimia 1.6 na 11.6 mtawalia na kusababisha kupungua kwa mahabusu na wafungwa gerezani, huku Mahakama za Mwanzo kukiwa hakuna mahabusu.

Kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, Mhe. Nkya amebainisha kuwa, zilikaguliwa kwa 100.

“Kuhusu ushughulikiaji wa mrejesho ulikuwa asilimia 99.9 ambapo jumla ya mirejesho 3,144 kati ya 3,149 (ikiwepo mitano “5” iliyobaki mwaka 2024) ilishughulikiwa,” ameeleza.

Amebainisha kuwa, kati ya mirejesho hiyo ushughulikiaji wa malalamiko ulikuwa ni asilimia 99.8 ambapo jumla ya malalamiko 1,609 kati ya 1,611 yaliyokuwepo (yakiwepo matano “5” yaliyobaki mwaka 2024) yalishughulikiwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni