Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Obadia Bwegoge ameongoza
Kikao cha awali cha usikilizaji wa mashauri ya mauaji na uhujumu uchumi lengo
likiwa ni kuharakisha uendeshaji wa mashauri kwa makosa yanayoweza kusikilizwa
na Mahakama Kuu.
Kikao
hicho kilifanyika tarehe 22 Mei, 2026 katika ukumbi wa Mahakama Kuu Njombe ambapo,
Mhe. Bwegoge alikutana na Wadau wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe wakiwemo wa
upande wa Mashtaka na upande wa Utetezi na kukubaliana mambo mbalimbali yunayohusu
mashauri ya mauaji na uhujumu uchumi.
Awali,
Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe.Isack Mlowe alifungua
kikao hicho na kumkaribisha Jaji Bwegoge ili aweze kuzungumza na wadau wa
Mahakama Njombe na kuwaeleza lengo la kikao hicho.
Aliwaeleza
kuwa, kikao hicho kilikuwa kinahusiana na maandalizi ya usikilizwaji wa mashauri ya kikao cha usikilizaji
wa mashauri ya mauaji na uhujumu uchumi kitakachoanza tarehe 15 Juni, 2026 mpaka tarehe 12 Julai, 2026
Mahakama ya Mwanzo Makambako iliyopo katika Halmashauri ya Mji Mdogo wa Makambako.
Mhe. Bwegoge alijadiliana na wadau wa Mahakama
mkoani Njombe kuhusu mambo mbalimbali pamoja na kupeana ushauri wa changamoto
ambazo huwa zinajitokeza katika usikilizwaji wa mashauri.
Katika
kikao hicho, alisema vikao vya mashauri hasa yanayosikilizwa mfululizo huwa kunakuwa na changamoto kama vile
uchelewaji wa mahabusu kufika Mahakamani, kupatikana kwa mashahidi ambao hutoa
ushahidi wa shauri zaidi ya moja.
Aidha, Jaji Bwegoge alitoa ushauri wa hoja
mbalimbali ambazo ziliibuka ikiwemo adha ya usafiri kutoka Njombe Mjini mpaka
Halmashauri ya Mji Mdogo wa Makambako.
Nao
upande wa Gereza Njombe na Polisi Njombe, walitoa ombi la mahabusu ambao mashauri yao
yatasikilizwa kwa siku zaidi ya moja mfululizo waweze kukaa Mahabusu zilizopo Mji
wa Makambako wakae huko na siyo kurudi mkoani Njombe ili kupunguza gharama kutokana
na aza ya mafuta kupanda bei ambapo Mhe. Bwegoge aliridhia ombi hilo.
Kwa
upande wa mashtaka pamoja na upande wa utetezi walibaini mambo ya msingi katika
usikilizwaji wa mashauri ambapo Mhe. Bwegoge aliwakumbusha Wadau Mahakama kuwa
uendeshaji wa vikao hivyo hufuata Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA)
na Kanuni za Makosa ya Uhujumu Uchumi.
Wakati wa kufunga kikao hicho, Mhe. Mlowe aliwashukuru wadau waliohudhuria kwenye kikao hicho ambao ni wadau wa Mahakama Njombe wakiwemo upande wa Mashtaka (NPS), Ofisi ya Upelelezi Polisi Mkoa (RCO), Magereza Njombe na Mawakili wa Kujitegemea upande wa Utetezi pamoja na Ustawi wa Jamii Mkoa wa Njombe.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Obadia Bwegoge (aliyeketi katikati) akiongoza Kikao cha awali cha usikilizaji wa mashauri ya mauaji na uhujumu uchumi. Aliyeketi kushoto Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Isack Mlowe na kulia ni Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Njombe, Bi. Lucia Mpepo wakiwa katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 22 Mei, 2026 mahakamani hapo.
Wadau mbalimbali wa Mahakama Kuu Njombe wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri katika Kikao cha awali cha usikilizaji wa mashauri ya mauaji na uhujumu uchumi. Aliyesimama ni Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Isack Mlowe akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Obadia Bwegoge akizungumza na Wadau wa Mahakama (hawapo katika picha) tarehe 22 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama hiyo.
Wadau mbalimbali wa Mahakama Njombe walioshiriki katika kikao hicho wakichangia jambo wakati wa majadiliano.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni