Na. CHRISTOPHER MSAGATI–Mahakama, Manyara
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Ilvin
Claud Mugeta, amewaongoza wajumbe wa Chama Cha Mahakimu na Majaji Tanzania
kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo hiyo katika Mafunzo yaliyofanyika kuanzia
tarehe 20 mpaka 23 Mwezi Mei, 2026 katika Hifadhi ya Taifa ya Wanyama Serengeti.
Akizungumza
na wajumbe hao kwa nyakati tofauti wakati wa maandalizi na hitimisho la ziara hiyo,
Mhe. Mugeta alieleleza lengo la ziara hiyo ni kuwawezesha Majaji na Mahakimu kutoka
Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara kuendelea kujinoa na kuongeza ujuzi
katika utendaji kazi wa kila siku ili kuleta tija na ufanisi wa utoaji huduma
ya Utoaji Haki kwa wananchi kwa wakati mapema ipasavyo.
“Suala
zima la utoaji haki kwa wakati mapema ipasavyo, linaenda sambamba na utoaji wa
mafunzo mbalimbali kwa wahusika wote ambao wanahusika katika mnyororo huu wa
Utoaji Haki…
…Kwa
sasa tumeanza na Waheshimiwa Majaji na Mahakimu kwa kupitia Chama chetu cha
TMJA lakini baadae tutaona namna ya kufikisha mafunzo haya kwa watumishi
wengine. Lengo la mafunzo haya ni kuendelea kunoa maarifa na ujuzi wetu tulio
nao kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma,” alisema Mhe. Mugeta.
Kwa
upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Devotha
Kamuzora ambaye pia ni Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Manyara aliwapongeza
watumishi wote waliofanikiwa kushiriki ziara hiyo ya mafunzo na kuwashauri
watumishi kuendelea kujisomea na kujiongezea ujuzi na maarifa ili kuwa imara
katika maamuzi na utendaji kazi wa kila Siku.
“Nawapongeza
watumishi wote (Watalii wenzangu) mliofanikiwa kusafiri kwa ajili ya mafunzo
haya na ninawashauri siku nyingine tuendelee kupenda kujisomea kwa ajili ya
kuboresha maarifa yetu ya kila siku hususan uandishi wa Hukumu zenye tija na
zinazoeleweka vizuri kwa jamii,” alisema Mhe. Kamuzora.
Baadhi
ya mada zilizotolewa katika mafunzo hayo ni pamoja na Uendeshaji wa mashauri ya
Mirathi katika Mahakama za Mwanzo, Utekelezaji wa Hukumu katika Mahakama za
Wilaya na Mahakama za Mwanzo na pia Usimamizi na Uondoshaji wa vielelezo
vinavyopokelewa Mahakamani.
Katika
hatua nyingine, Wanachama hao wa TMJA Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara
walitumia muda wao wa baada ya mafunzo katika kufanya ziara ya Utalii wa kuona
wanyama wa aina mbalimbali katika Hifadhi hiyo ya taifa ya Serengeti.
Akizungumza
kwa niaba ya wanachama wengine wa TMJA Manyara, Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo
Bassotu Mhe. Sabato Mwangwa, aliushukuru uongozi wa TMJA Manyara pamoja na
Uongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara kwa kuwezesha mafunzo hayo
kufanyika katika Hifadhi ya Serengeti kwa sababu pamoja na mafunzo, pia
wanachama wamepata muda wa kuburudisha akili na miili yao kwa kuweza kufanya
utalii huo wa ndani.
“Tunashukuru
sana viongozi wetu kwa kutuwezesha kufanya mafunzo haya huku mbugani, Pamoja na
maarifa tuliyoyapata tumeweza kuburudika kwa kuona Wanyama wa aina mbalimbali.
Tunaomba uongozi uone uwezekano wa kufanya mafunzo zaidi na ikiwezekana
yaratibiwe katika maeneo kama haya,” alisema Mhe. Mwangwa.
Jumla
ya wanachama 47 wa TMJA Manyara wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo
ya Manyara, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara, Mahakimu
Wakazi wafawidhi wa Wilaya zilizopo katika Masjala Ndogo hiyo na pia Mahakimu
wengine waliweza kushiriki ziara hiyo ya mafunzo.
Wengine
waliokuwa kwenye ziara hiyo ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya
Manyara, Maafisa Rasilimaliwatu na Maafisa Tawala wa Mahakama wa Masjala Ndogo
hiyo walishiriki ziara hiyo ikiwa ni muendelezo wa kuendelea kutambua vivutio
vya asili vilivyo ndani na nje ya Mkoa wa Manyara.
Sehemu
ya Wajumbe wa Tawi la TMJA Manyara wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa
zikitolewa wakati wa mafunzo ya Wajumbe wa Tawi la TMJA Manyara yaliyofanyika
katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Hakimu
wa Mahakama ya Mwanzo Dongobesh Mhe. Mgusi Masinde iliyopo wilayani Mbulu
akitoa mada ya Uendeshaji wa mashauri ya Mirathi wakati wa mafunzo ya Wajumbe
wa Tawi la TMJA Manyara yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Mnyama
aina ya Nyati akiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama alivyoonekana na
wajumbe wa TMJA-Manyara katika ziara ya mafunzo na Utalii iliyofanyika
Hifadhini hapo.
Wanyama
aina ya Swala wakiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama walivyoonekana
na wajumbe wa TMJA-Manyara katika ziara ya mafunzo na Utalii iliyofanyika
Hifadhini hapo.
Mnyama
aina ya Twiga akiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama alivyoonekana na
wajumbe wa TMJA-Manyara katika ziara ya mafunzo na Utalii iliyofanyika
Hifadhini hapo.
Mnyama
aina ya Fisi akiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama alivyoonekana na
wajumbe wa TMJA-Manyara katika ziara ya mafunzo na Utalii iliyofanyika
Hifadhini hapo.
Wanyama aina ya Pundamilia wakiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama walivyoonekana na wajumbe wa TMJA-Manyara katika ziara ya mafunzo na Utalii iliyofanyika Hifadhini hapo.
Wajumbe
wa Tawi la TMJA Manyara wakiwa katika picha ya Pamoja kabla ya kuanza kwa
mafunzo yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Majaji
wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Ilvin Mugeta (mwenye fulana ya
mistari ya rangi nyekundu na nyeupe) pamoja na Mhe. Devotha Kamuzora (mwenye
kofia ya rangi nyeusi) wakiwaongoza wajumbe wa TMJA-Manyara kumsikiliza mmoja
wapo wa watumishi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti mara baada ya kuwasili
Hifadhini hapo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo akitoa Neno la Salamu wakati wa mafunzo ya Wajumbe wa Tawi la TMJA Manyara yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni