Ijumaa, 1 Mei 2026

MSIWE CHANZO CHA MAFARAKANO NA CHUKI KWA JAMII; JAJI SALMA MAGHIMBI

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Msata

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amewataka watumishi wa Mahakama Mkoa wa Pwani kutokuwa chanzo cha mafarakano na chuki kwa jamii.

Mhe. Maghimbi ameyasema hayo jana tarehe 30 Aprili, 2026 alipokuwa akifungua jengo la Mahakama ya Mwanzo Msata lililopo Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani.

Akizungumza wakati akitoa hotuba yake Jaji Maghimbi amesema jengo hilo ni nyumba ya haki na kuleta amani kwenye jamii hivyo watumishi wasiwe chanzo cha mafarakano na chuki kwenye jamii.

“Tumekabidhiwa kwa Mwenyezi Mungu sisi na jengo, hivyo; tujue anatuangalia na kutuonya tabia na matendo yetu mema na mabaya yatawekwa kwenye mizani, tutende yaliyo mema na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.

Katika hotuba yake, Mhe. Maghimbi ameeleza kuwa, katika Wilaya ya Bagamoyo kuna Mahakama za Mwanzo saba ikiwemo Mahakama ya Mwanzo Msoga- Lugoba ambayo siku za hivi karibuni jengo lake lote liliungua kwa moto, hivyo upelelezi unaenddelea kubaini chanzo cha moto huo.

Kupitia ufunguzi wa jengo hilo pia, Mhe. Maghimbi amewaarifu na kuwatangazia wananchi wote  kuwa, huduma za Mahakama ya Wilaya Bagamoyo zilizokuwa zikisogezwa na kutolewa katika jengo la Mahakama ya Mwanzo Lugoba/Msoga zitaanza kutolewa katika jengo la Mahakama ya Mwanzo Msata.

Aidha, Mhe. Maghimbi amesema kujengwa kwa jengo hilo la Mahakama ya Mwanzo Msata siyo kwa bahati mbaya bali ni utekelezaji wa programu ya maboresho inayofanywa na Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake ulioanza awamu ya kwanza mwaka 2015 hadi 2016 na awamu ya pili 2020 hadi 2025.

“Mpango Mkakati huu wa Mahakama unaongozwa na nguzo tatu za Utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, upatikanaji wa haki kwa wakati na uimarishaji wa imani ya wananchi kwa Mahakama pamoja na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama,” ameeleza Jaji Maghimbi.

Mhe. Maghimbi amesema Mahakama hiyo itahudumia wananchi wa maeneo ya Kata za Mbwewe, Kibindu, Msata, Mandesa na Kimange. Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022 ujenzi huo umeboresha huduma za Mahakama kwa wakazi zaidi ya 92,890 wanaoishi katika Kata hizo tano.

Kadhalika amewakumbusha wananchi kuwa, haki ndio msingi wa ustawi wa Taifa kwa kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuongeza kwamba, ili shughuli yoyote ya kiuchumi iweze kufanyika  kwa ufanisi, inahitaji mazingira ya amani, utulivu, utawala bora, utawala wa sheria na mfumo rafiki wa utatuzi wa migogoro inapotokea. Kwa mantiki hiyo haki huinua Taifa.

Amesema pia kujenga jengo kama hilo ni jambo adhimu, lakini pia kulitumia jengo hilo katika kutoa huduma bora na zinazomlenga mwananchi ni jambo lingine.

Ametumia fursa hiyo, kuwajulisha kuwa, maboresho ya huduma za Mahakama hayajalenga tu majengo bali pia yamelenga kubadili mitazamo ya watumishi wa Mahakama katika kutoa huduma za haki kwa mtazamo wa zamani wa Mahakama inayotisha na sasa kutoa huduma za kimahakama zinazomlenga Mwananchi.

Katika hotuba yake amesema programu ya maboresho ya Mahakama imeleta utamaduni mpya wa utoaji huduma wenye mitazamo ya utoaji haki kwa haraka, weledi, uwazi, ufanisi na unaomjali mwananchi (Citizen Centric Justice Delivery) ili mwananchi atumie muda wake mwingi kwenye uzalishaji wa mal ibadala ya kupoteza muda katika kutatua migogoro Mahakamani.

Amesema katika kuyafikia hayo watajipima kwenye Dira ya Mahaklama ya Tanzania isemayo “Utoaji Haki kwa Wote Mapema ipasavyo.’

Jaji Mfawidhi ametoa maelekezo muhimu kwa watumishi wa Mahakama kulilinda na kulitunza jengo hilo ili lidumu kwa muda mrefu na utunzaji huo uende sambamba na upandaji miti, jengo litumike katika kutoa huduma bora zinazoendana na utekelezaji wa maboresho yanayozingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo.

Ameongeza kuwa, Kituo hicho kinapaswa kuongezewa watumishi ili kiendane na kasi ya kuwahudumia wananchi pamoja na vitendea kazi vingine ikiwemo vifaa vya TEHAMA sambamba na kuimarisha weledi, uadilifu, uwazi, umoja na maelewano baina ya watumishi na wateja.

Kadhalika, Mhe. Maghimbi amewataka Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea kuhakikisha hawatakuwa kikwazo katika utoaji huduma za Mahakama hiyo kwa kuchelewesha haki bila sababu ya msingi ili kusaidia Mahakama kutoa huduma bora, kulinda na kutunza heshima na uhuru wa Mahakama.

Vilevile, Jaji Mfawidhi huyo ametoa rai kwa Viongozi wa Serikali  kusaidia kutoa huduma bora kwa kuweka mazingira wezeshi ua ulinzi na usalama katika jengo la Mahakama, kuisaidia Mahakama kupata maeneo mengine ya kujenga Mahakama mpya hususan katika Kata ambazo hazina Mahakama, kuwafikishia taarifa wananchi wa Kata zingine kuhusu kuanza kwa huduma za Mahakama ya Mwanzo Msata ili waitumie.

Kwa upande wa wananchi, Mhe. Maghimbi amewaomba kufikisha mahakamani migogoro yote inayohitaji kushughulikiwa  na Mahakama sambamba na kusaidia ulinzi wa jengo  hilo na mali za Mahakama ili zitumike kwa manufaa ya umma wa Watanzania.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo ametoa mwelekeo wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ya kuwa shughuli za utoaji haki za Kanda hiyo inasimamia Mikoa miwili ya Dar es salaam na Pwani na inasimamaia Mahakama za Hakimu Mkazi nne na Mahakama za Wilaya 12 na Mahakama za Mwanzo 54.

Pamoja na uzinduzi huo, mwezi uliopita Mhe. Maghimbi alizindua Mahakama mpya ya Wilaya ya Kigamboni inayoketi Somangila  iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam, majengo mapya matatu ya Mahakama za Mwanzo ambazo ni Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Temeke inayoketi Mbagala, Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Mkuranga inayoketi Kimanzichana na Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Kibiti inayoketi Bungu. 

Amesema pia iko safari ya kufikisha huduma za Mahakama Mkoa wa Pwani na Mahakama za Mwanzo katika Kata za Talawanda, Pera, Vigwaza, Ubena Zomozi, Kimange, Mbwewe, Kibindu, Mandera, Mkange, Makurunge, Fukayosi, Mapinga, Yombo, Kiromo, Zinga, Nianjema, Kisutu, Lugoba na Magomeni. 

Naye Mhandisi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhandisi Francis Deogratius Upendo akitoa taarifa ya Mradi wa Mahakama ya Mwanzo Msata amesema, usanifu wa mradi wa Mahakama ya Mwanzo Msata umezingatia mazingira bora ya kufanyia kazi katika ofisi mbalimbali, urahisi wa kufikika na miundombinu wezeshi kwa makundi maalum.

Pia matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma na uendeshaji wa shughuli za Mahakama, ulinzi na usalama kwa watumiaji wa jengo pamoja na muonekano na taswira pekee ya Mahakama.

Akitoa salamu za Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Jesca  Samson amesema Mkuu huyo ametuma salamu za pongezi kwa Mhimili wa Mahakama kwa kuboresha maeneo ya kutolea haki wananchi wa Msata wamefurahi sana.

Baada ya ufunguzi wa Jengo la Mahakama hiyo, Jaji Mfawidhi Maghimbi pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian Mkeha, Jaji wa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam, Mhe. Hamidu Mwanga, Mtendaji wa Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Sumera Manoti, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Nestor Mujunangoma, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe. Yasinta Kingwala walipata wasaa wa kupanda miti katika eneo la Mahakama hiyo.

  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam akihutubia watumishi wa Mahakama, Wadau kutoka Taasisi mbalimbali na wananchi walioshiriki katika sherehe za uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Msata-Bagamoyo iliyofanyika jana tarehe 30 Aprili, 2026.


Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati). wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu divisheni ya Biashara Mhe. Cyprian Mkeha, wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hamidu Mwanga, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mhakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Livin Lyakinana na wa pili kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Jesca  Samson.

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Livin Lyakinana akitoa utambulisho wa wageni waliohudhuria Sherehe ya Ufunguzi wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Bagamoyo inayoketi Msata.

Mhandisi wa Majengo wa Mahakama Kuu, Bw. Francis Deogratius Upendo akitoa taarifa ya mradi huo wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Msata lililopo Wilaya ya Bagamoyo.

Kikundi cha Hamasa cha Watumishi wa Mahakama Pwani wakitumbuiza wakati wa sherehe hizo.

Kwaya ya Mahakama ya Tanzania (Ng’aring’ari Quir one) wakiimba katika sherehe za ufunguzi wa Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Bagamoyo inayoketi Msata. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Dar es Salaam Mhe. Salma Maghimbi akikata utepe kuashiria ufunguzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Msata.


Jengo la Mahakama ya Mwanzo Msata lililozinduliwa.

Kikundi cha Ngoma cha Tosuba kutoka Bagamoyo wakitumbuiza katika sherehe ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Msata-Bagamoyo.

Meza kuu katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi waliohudhuria sherehe za ufunguzi wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Msata.


Meza kuu aktika picha ya pamoja na Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama Dar es Salaam na Pwani. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu divisheni ya Biashara Mhe. Cyprian Mkeha, wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hamidu Mwanga, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mhakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Livin Lyakinana na wa pili kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Jesca  Samson.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



 

  


 

 


 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni