Ijumaa, 1 Mei 2026

SERIKALI ITAENDELEA KUBORESHA MASLAHI, MAZINGIRA YA KAZI KWA WAFANYAKAZI; MHE. SENYAMULE

Na. INNOCENT KANSHA & JAMES BUSANYA - Mahakama

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu jijini Dodoma leo tarehe Mosi Mei, 2026 wameungana na wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi kuadhimisha Siku ya wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) katika Kiwanja cha michezo cha Jamhuri jijini Dodoma.

Maadhimisho hayo yalianza kwa Taasisi mbalimbali kushiriki kwenye maandamano huku wakiwa wamebeba Mabango yenye kaulimbiu ya maadhimisho hayo isemayo “Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050” matembezi hayo yaliyoanzia kwenye viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuhitimishwa kiwanjani Jamhuri na kupokelewa na Mgeni Rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amelishukuru Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi TUCTA kwa kumualika kushiriki katika kilele cha maadhimisho hayo, huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuhimiza uwajibikaji na bidii kazini miongoni mwa wafanyakazi.

Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi nchini ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kufikia malengo ya maendeleo ya Dira ya Taifa ifikapo mwaka 2050.

Mhe. Senyamule amesema kuwa, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Serikali imefanikiwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi, huku ikiendelea kuboresha miundombinu muhimu ya kurahisisha mfanyakazi kutoa huduma bora kwa jamii kama vile upatikanaji wa umeme, ujenzi wa miundombinu ya majengo pamoja na kuimarisha mawasiliano ya simu na intaneti.

“Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya kazi ili kuwasaidia wafanyakazi kufanya kazi kwa urahisi na ufanisi zaidi ili kuongeza tabasamu kwa wananchi,” alisema Mkuu wa Mkoa huyo.

Aidha, alitoa wito kwa wafanyakazi kushirikiana na Serikali kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, huku akisisitiza umuhimu wa Sekta binafsi kufuata taratibu na sheria zilizowekwa ili kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Mhe. Senyamule akigusia maelekezo ya Rais Samia amesema kuwa, alielekeza kuwapa tabasamu wananchi nanyi Viongozi muwape tabasamu watumishi ili wafanyaka wawape tabasamu wananchi wanaowahudumia kuendelea kuimarisha ustawi wa wananchi kwa kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa usawa na kuepuka rushwa.

Aidha, Mhe. Senyamule amesema kwamba, Mkoa wa Dodoma umetajwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayonufaika na uwekezaji wa Serikali hususan Vyuo vya elimu ya Juu. Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wafanyazi kujiendeleza kielimu kutokana na fursa hiyo.

Katika hatua nyingine, wafanyakazi wametakiwa kuepuka vitendo vya rushwa na badala yake kuzingatia uadilifu katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Pia wamehimizwa kutenga siku maalum za kusikiliza kero za wananchi ili kuboresha huduma.

Mkuu wa Mkoa huyo aliwatakia wafanyakazi wote mkoani Dodoma maadhimisho mema ya Siku ya Wafanyakazi Duniani na kuwataka kuendelea kushirikiana kwa ngazi zote kitaasisi katika kujenga Taifa lenye maendeleo na ustawi.

Kwa upande wake, Katibu wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi Mkoa wa Dodoma Bw. Albert Stanslaus akisoma risala ya wafanyakazi mbele ya Mgeni rasmi amesema kuwa, licha ya juhudi za Serikali kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini, bado kuna changamoto zinazoikumba Sekta ya ajira ambazo zimeendelea kujitokeza, hususan katika sekta binafsi, ambapo wafanyakazi wanalalamikia ukiukwaji wa haki zao za msingi.

Risala hiyo ya wafanyakazi imebainisha mambo mbalimbali yaliyotajwa na wadau kwamba licha ya hatua stahiki zilizochukuliwa na Serikali kutatua changamoto za wafanyakazi lakini bado kuna matatizo yanayohitaji ufumbuzi wa haraka.

Bw. Stanslaus ameongeza kuwa, kupitia risala hiyo wafanyakazi wanakumbwa na ucheleweshaji wa malipo ya malimbikizo mbalimbali kama vile likizo, kupanda madaraja, huku wengine wakidai kutokuwa na mikataba rasmi ya ajira, hali inayowafanya kukosa uhakika wa ajira zao. Aidha, ilibainika kuwa kuna waajiri wanaolipa mishahara midogo isiyokidhi viwango vinavyokubalika kisheria.

Changamoto nyingine iliyotajwa ni kutowasilishwa kwa michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati, jambo linalosababisha usumbufu mkubwa wanapohitaji mafao yao pindi wanapostaafu au wanapopata matatizo.

Pamoja na hayo, washiriki wa maadhimisho hayo walitoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake katika kuboresha mazingira ya kazi, ikiwa ni pamoja na kupandisha mishahara kwa mwaka 2025, kupandisha watumishi madaraja na kulipa madeni ya muda mrefu ya wafanyakazi.

Kupitia risala hiyo Katibu huyo alisisitiza kuwa juhudi zaidi zinahitajika ili kuhakikisha haki za wafanyakazi zinalindwa kikamilifu, hasa kwa kuimarisha usimamizi wa sheria za kazi na kuwawajibisha waajiri wanaokiuka taratibu.


Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akihutubia alaiki ya wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali wa Serikali na Sekta Binafsi katika Siku ya Maadhimisho ya Wafanyakazi Duniani leo tarehe Mei, Mosi, 2026 katika kiwanja cha michezo cha Jamhuri jijini Dodoma.




Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu jijini Dodoma wakiwa tayari kwa ajili ya matembezi ya kuadhimisha Siku ya Wanyakazi Duniani leo tarehe Mosi Mei, 2026 katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu jijini Dodoma wakiwa tayari kwa ajili ya matembezi ya kuadhimisha Siku ya Wanyakazi Duniani leo tarehe Mosi Mei, 2026 katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu jijini Dodoma wakiwa wanashiriki matembezi na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi ikiwa ni ishara ya kuadhimisha Siku ya Wanyakazi Duniani
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu jijini Dodoma wakiwa wanashiriki matembezi na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi ikiwa ni ishara ya kuadhimisha Siku ya Wanyakazi Duniani.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu jijini Dodoma wakiwa wanashiriki matembezi na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi ikiwa ni ishara ya kuadhimisha Siku ya Wanyakazi Duniani
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu jijini Dodoma wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kuhitimisha matembezi 

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu jijini Dodoma wakiwa wanapita mbele ya Mgeni Rasmi kwa mbwembwe na bashasha wakati wanaingia uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni