- Chawasilisha
Mapendekezo Saba kwa Jaji Mkuu
Na MARY GWERA,
Mahakama-Dodoma
Chama cha Madalali wa
Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Tanzania kimeiomba Mahakama kusimamia
ipasavyo Sheria na taratibu ili kulinda usalama wao, heshima ya amri za Mahakama
na kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.
Akizungumza mbele ya
Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju
leo tarehe 30 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya
Tanzania jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Chama hicho, Bi. Mwamvua Kigulu amesema
kuwa, Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama ni nguzo muhimu kwani hukumu
haiwezi kufikia lengo lake bila utekelezaji, na mashauri hayawezi kusonga mbele
bila usambazaji sahihi wa nyaraka.
Bi.
Mwamvua ametaja Changamoto na Mapendekezo saba kwa Mahakama ili kuimarisha
utendaji kazi na kulinda hadhi ya Mhimili huo, ambayo ni pamoja na kuomba Ulinzi
wa Polisi Wakati wa Utekelezaji.
Chama
hicho kimeomba Mahakama isimamie utekelezaji wa amri zake kwa kutoa ulinzi wa
Polisi kwa Madalali, kwani katika baadhi ya maeneo amri hizo hazitekelezwi
ipasavyo, jambo linalohatarisha usalama wao.
“Kuingiliwa na Viongozi
wa Kisiasa na Serikali; kufuatia matukio ya kuingiliwa kwa amri halali za Mahakama
kabla na baada ya kutekelezwa, Chama kinaomba Mahakama kutoa Mwongozo thabiti
kuwa hakuna mamlaka inayoruhusiwa kuzuia utekelezaji huo isipokuwa kwa mujibu
wa sheria,” amesema Mwenyekiti huyo.
Kadhalika, Chama hicho kimeomba
kudhibiti Wavamizi wa Kazi ya Usambazaji Nyaraka: ambapo kimesikitishwa na
tabia ya baadhi ya Mawakili na Makarani wa Mahakama kufanya kazi ya usambazaji
nyaraka wakati hawajateuliwa kisheria hivyo wameomba sheria isimamiwe ipasavyo
ili kazi hiyo ifanywe na Wasambaza Nyaraka waliosajiliwa pekee.
Aidha, Bi. Mwamvua
ametaja pendekezo lingine la kuomba kuongezeka kwa Muda wa Kuhuisha Leseni
ambapo Chama hicho kimeomba muda wa kuhuisha leseni zao uongezwe na kuwa miaka
mitatu (3) kwa nyaraka zinazoisha muda wake ili kupunguza gharama, kwa kuwa
wote wapo chini ya sheria moja.
Kuhusu Gharama za
Uhifadhi (Storage), wamependekeza gharama za uhifadhi zilipwe kuanzia siku ya
kwanza mali inapokamatwa, kwa kuwa gharama za maghala, ulinzi na bima hulipiwa
mwaka mzima na usimamizi ukiacha hapo hapo.
Kadhalika, Mwenyekiti
huyo amebainisha juu ya changamoto ya Gharama za Utekelezaji (GN Na. 363 ya
2017) ambapo Chama hicho kimeomba malipo ya utekelezaji yaendelee kulipwa bila
kuwekewa ukomo wa asilimia, bali yalipwe kwa uwazi na haki kama yalivyoainishwa
kwenye Kanuni za Serikali (GN Na. 363 za Mwaka 2017).
Aidha, Bi. Mwamvua
ameishukuru Mahakama ya Tanzania kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa kuwapatia
mafunzo ya mara kwa mara na kuomba mafunzo hayo kuwa endelevu ili kuendelea
kuongeza weledi, uwajibikaji na ubora wa huduma kwa wananchi.
Chama hicho kupitia
Mwenyekiti huyo kimemshukuru Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwa kuwasikiliza na kuahidi
kuendelea kushirikiana bega kwa bega na Mahakama katika kusimamia utawala wa
sheria nchini Tanzania.
Mwenyekiti wa Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Tanzania, Bi. Mwamvua Kigulu akitoa neno la utangulizi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho leo tarehe 30 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akisikiliza neno kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Tanzania, Bi. Mwamvua Kigulu (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa neno la utangulizi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho leo tarehe 30 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni