Jumanne, 30 Juni 2026

MADALALI, WASAMBAZA NYARAKA WA MAHAKAMA WAASWA KUWA WAADILIFU

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma amewaasa Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka   kufanya kazi zao kwa kuzingatia Uadilifu wa hali ya juu na Sheria.

Mhe. Mruma ametoa rai hiyo leo tarehe 30 Juni, 2026 alipokuwa akitoa neno kwa niaba ya Jaji Kiongozi, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Tanzania uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

"Mkikosa uadilifu katika hilo, mnatengeneza mazingira rahisi kwa watu wa Mihimili mingine kuingilia Mhimili wa Mahakama na kuhalalisha uingiliaji wao," amesema Jaji Mruma.

Akizungumza kwa niaba ya Jaji Kiongozi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama, Mhe. Mruma amebainisha kuwa, utekelezaji wa hukumu za madai unategemea kwa kiasi kikubwa utendaji wa Madalali hao, na kwamba bila wao, mnyororo wa utoaji haki unakuwa haujakamilika.

Jaji Mruma amesema, katika miaka ya karibuni, kumeonekana kuwepo kwa changamoto kubwa ya Viongozi wa Kisiasa—hasa wanaotumia nyadhifa zao kama Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama—kuingilia utekelezaji wa amri za Mahakama.

Akieleza jinsi ya kukabiliana na hali hiyo, amewataka Madalali kujiamini na kutumia sheria kuchukua hatua dhidi ya yeyote anayewakwamisha.

"Sheria inawaruhusu kuwachukulia hatua watu wanaoingilia utendaji wenu kwa njia ya dharau kwa Mahakama (contempt of court). Kumzuia Ofisa yeyote wa Mahakama kutekeleza amri halali ni kosa, na tunategemea mchukue hatua za kisheria ili kukomesha hali hii mara moja na kwa mara zote," amesisitiza.

Pamoja na kuwataka Madalali hao kuwa wajasiri, Mhe. Mruma ameeleza kuwa, uhuru wao wa kufanya kazi na ulinzi wa kisheria unaweza tu kulindwa ikiwa wao wenyewe wataonesha uadilifu wa hali ya juu.

Ametaja maeneo yanayolalamikiwa zaidi kuwa ni pamoja na: Ukamataji na Uhifadhi wa Mali ambapo Mali kukamatwa na kutofikishwa kwenye yadi za Madalali, na wakati mwingine kupotea.

Kaimu Jaji Kiongozi huyo ametaja eneo lingine linalolalamikiwa kuwa ni Uuzaji wa Mali chini ya Kiwango: Mali kuuzwa kwa bei isiyo ya soko au isiyozingatia tathmini halisi.

“Ukiukwaji wa Taratibu za Uondoaji, baadhi ya madalali wasio waadilifu kufunga nyumba au kutoa watu nje bila kuwa na amri maalum ya uondoaji badala ya kuweka tu tangazo la zuio la Mahakama,” amesema.

Ameongeza kuwa, ili kuimarisha usalama na hadhi ya Madalali hao, Mahakama inaangalia uwezekano wa Kisheria wa kuwatambua rasmi watendaji hao kama Maofisa kamili wa Mahakama ili wapate ulinzi thabiti wa kisheria wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma akitoa neno wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Tanzania uliofanyika leo tarehe 30 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.



Baadhi ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama wakimsikiliza Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa neno wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho leo tarehe 30 Juni, 2026 Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)






 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni