· Awataka Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kusimama ipasavyo katika utendaji kazi wao
Na
MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amekemea vikali
vitendo vya baadhi ya Viongozi wa Serikali na wa Kisiasa kuingilia utendaji wa
shughuli za Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kwa kisingizio kwamba wao
ni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya.
Mhe.
Masaju ameyasema hayo leo tarehe 30 Juni, 2026 alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu
wa Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Tanzania uliofanyika
kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini
Dodoma.
“Hizo
sheria zinazowapa madaraka hazikuwapa mamlaka ya kuingilia utekelezaji wa amri
na maamuzi ya Mahakama. Wachukulieni hatua. Haiwezekani Mahakama imeshatoa amri
halafu mtu mwingine anazuia, hiyo inakuwa ni Mahakama au ni kitu gani? Ni
lazima tutofautishe shughuli za kisiasa na shughuli za kutoa haki zinazofanywa
na Mahakama,” amesema Jaji Mkuu.
Akizungumzia
kuhusu Changamoto na Usimamizi wa Sheria, Jaji Mkuu amewaeleza, Madalali na
Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kuwa nao wana changamoto ndio maana wanaruhusu
wanasiasa kuingilia utendaji kazi wao bila kuwachukulia hatua.
“Hakuna
mtu ambaye yuko juu ya sheria na hata mimi Jaji Mkuu siko juu ya sheria. Na
kwanza hata mimi kwa kiapo changu na Majaji wote hapa na Mahakimu wote, na hata
Wasajili tunaapa tunapotekeleza majukumu yetu kuzingatia Katiba, mila na
desturi, na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila hofu, upendeleo,
wala chuki,” amesema Mhe. Masaju.
Aidha,
Jaji Mkuu amewataka Madalali na Wanasheria wao kuchukua hatua kali za kisheria,
ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kinyume cha sheria (false imprisonment) au uzuiaji
wa utekelezaji wa amri halali, Maofisa wa Polisi au Viongozi wanaokiuka Sheria
kwa majina yao binafsi, kwani Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameshafafanua kuwa
wavunja Sheria watagharamia makosa yao wenyewe.
Mhe.
Masaju amesema kuwa, katika kipindi hiki ambacho Tanzania inatekeleza Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2050, msingi Mkuu wa Dira hiyo inahusu Utawala Bora na Haki,
hivyo, hakuwezi kuwa na ‘Utawala Bora na Haki’ kama maamuzi ya Mahakama
yanaingiliwa na watu wengine bila sababu za msingi.
Amesisitiza
kuwa Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka wazi
kuwa, kila mtu ana wajibu wa kuitii Sheria za pamoja na haki ya kulinda na
kusimamia Katiba.
“Ili
kufikia malengo haya, Mhimili wa Mahakama lazima ubaki na hadhi na heshima yake
na pande zote zitekeleze wajibu wao kwa usafi na uadilifu ili kuzuia mianya ya
kuingiliwa,” amesisitiza Mhe. Masaju.
Aidha,
Jaji Mkuu amewakumbusha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kuwa, kama
wanataka wasiingiliwe nao wanapaswa kuwa wasafi kwa kutekeleza wajibu wao kwa
mujibu wa Katiba, Sheria, Maadili na Kanuni zilizowekwa ili kutotoa fursa kwa
watu wengine kuwaingilia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kadhalika,
amewataka wadau hao muhimu wa Mahakama kuwa na uwezo wa kumudu majukumu yao kwa
ufanisi unaotakiwa. Akiwasisitizia jambo hilo, ameeleza: “Mmeshukuru hapa
kwamba Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kinatoa mafunzo
yanayowasaidia; lakini moja ya masharti ya kupewa kazi hizi ni kuwa na uwezo wa
kumudu majukumu husika. Masharti yanasema wazi kuwa mnatakiwa muwe watu mnaojua
taratibu za mambo mnayoyasimamia. Sasa kama mlikuwa hamyajui, mlipataje hizi
nafasi ? Tutawanyang’anya hizi leseni.”
“Mmewekewa
utaratibu ambao lazima ninyi wenyewe muuheshimu mnapokuwa mnatekeleza majukumu
yenu, utaratibu huu umetajwa katika Sheria, yale maadili yenu, ningependa
niwarejeshe hapa katika hayo maadili myazingatie, haya yatawafanya basi
mkiyatekeleza na kuyaishi muwe na sifa sasa ya kuwa Maofisa wa Mahakama.
Mkishindwa kuyaishi haya na kuyatekeleza hata kama sisi nia yetu ingetaka ninyi
muwe Maofisa wa Mahakama,” amesema Jaji Mkuu.
Mhe.
Masaju amebainisha kuwa, Misingi ya kimaadili kwa Madalali na Wasambaza Nyaraka
imebainishwa katika Nyongeza ya Pili na ya Tatu, mtawalia ya Kanuni za Madalali
na Wasambaza Nyaraka (Uteuzi, Malipo na Nidhamu), Tangazo la Serikali Na. 363
la 2017 kama ilivyorekebishwa na Tangazo la Serikali Na. 106 la 2019.
Aidha,
ametaja sifa za Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kuwa ni pamoja na
Uadilifu ambapo amesema suala la kuwa na uadilifu ni jambo la msingi na
wanatakiwa kulidumisha.
“Mtakuwa
Waadilifu kwa kutekeleza Sheria za Nchi na Katiba, lakini mtakuwa waadilifu
kuyaishi maadili ya utumishi wenu na mtakuwa waadilifu wakati wa kutekeleza
majukumu yenu, myatekeleze kwa uadilifu ipasavyo,” amesisitiza.
Jaji
Mkuu ametaja sifa nyingine wanayopaswa kuwa nayo kuwa ni kuwa Waaminifu kwa
kile ambacho wanakifanya kwa kutekeleza sheria kwa uaminifu bila kutumia vibaya
mamlaka yao sambamba na kufanya kila hatua kwa uaminifu.
“Tulianza
shughuli hii kwa dua na sala, Mungu hadhihakiwi unachopanda ndicho unachovuna,
hatuwezi kutumia fursa hii kujinufaisha na kuonea watu, kimsingi wanaotumia hii
vibaya watawajibishwa na Mungu, nendeni msome Zaburi 37 muone inasema nini.
Hatuwezi kuwa wakati wote tunalitaja jina la Mungu, lazima tuishi hilo kauli
Mungu hadhihakiwi, huwezi kulichukulia jina la Mwenyezi Mungu bure kama jina
langu mimi. Kuna amri inasema usilitaje jina la Mungu wako bure yaani
unalichukulia poa na unamchukulia poa,” amesema.
Mhe.
Masaju amesema, Mahakama haipaswi kuwa na sifa mbaya na kwamba ikiwa na sifa
mbaya, itakosa uhalali wa kuwa Mahakama ya kufanya maamuzi, hivyo amewataka
kutoshiriki kuchafua sifa ya Mhimili huo.
Ameongeza
kwa kusema kuwa, kama Mahakama imeamua sahihi, halafu wao wanapofanya tofauti
na kilichoamriwa wanakosea na maana yake ni kupotosha uamuzi wa Mahakama hali
inayosababisha Mahakama iwe na sifa mbaya.
Aidha,
amewataka Wadau hao muhimu wa Mahakama kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu na
wawe na uwezo wa kumudu majukumu yao kwa ufanisi ipasavyo. Amesema, kutokufanya
hivyo kutaleta migogoro isiyoisha Mahakamani.
Ameongeza
kuwa, sifa nyingine ni pamoja na Usiri (Confidentiality), kutovujisha siri za
mchakato wa maamuzi ya Mahakama kabla hayajatamkwa rasmi na kutoa Huduma Bora
(Quality Service) zenye viwango vinavyoacha picha chanya kwa jamii.
Kadhalika,
Mhe. Masaju amesema Madalali ni Nguzo Muhimu ya Haki, ambapo amewatambua kama
Maofisa muhimu wanaotekeleza majukumu ya ukamilishwaji wa maamuzi ya kisheria.
"Ninyi
ni watu muhimu sana. Vinginevyo, kwenye mashauri ya madai, maamuzi ya Mahakama
yasingekuwa yanatekelezwa. Na kama maamuzi hayatekelezwi, Mahakama itadhulika,
na hatma yake ni uvunjifu wa amani na kupotea kwa uhuru wa Mahakama,"
amesema Mhe. Masaju.
Aidha,
amewakumbusha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kuhusu kuwa na hofu ya
Mungu, Jaji Mkuu amewataka kusoma Zaburi ya 37 na kuacha tabia ya kulitaja jina
la Mungu bure huku matendo yao yakiwa ya kidhalimu.
“Sheria
inawataka Madalali kutambua makundi maalum yenye uhitaji na kutoa huduma kwa
uangalifu mkubwa bila kuwaletea fedheha au majonzi zaidi. Makundi hayo ni
pamoja na Watu wazima, Walemavu, Wagonjwa sana, Waliogubikwa na majonzi ya
kufiwa, Wanawake wajawazito,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Ameongeza
kuwa, kila Dalali wa Mahakama ana wajibu wa kuheshimu utu, faragha na staha ya
mwanamke. Ambapo amesisitiza, hawa watu wengine ni wajane, msiende
kuwanyang'anya mali zao na kuwaongezea majonzi."
Kanuni
ya 7 ya Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka zinabainisha jukumu kuu la
Madalali wa Mahakama kuwa ni kutekeleza amri au maamuzi ya Mahakama zilizo
ndani ya mamlaka yake, na itajumuisha majukumu mengine kama; kukamata na kuuza
mali ya mdaiwa kwa ajili ya kutekeleza amri au maamuzi ya Mahakama kama
ilivyoelekezwa kwenye Amri ya 21 ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai na
Sheria Nyinginezo Pamoja na kutekeleza amri za kuwaondoa/kufukuza wadaiwa
(eviction orders).
Majukumu
mengine ni kutekeleza amri nyingine yoyote iliyotolewa na Mahakama;kuandaa na
kuwasilisha Mahakamani taarifa au mrejesho namna utekelezaji ulivyofanyika; na
kutekeleza maelekezo mengine yoyote yaliyotolewa na Mahakama.
Aidha,
Kanuni ya 8 ya Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka zinabainisha jukumu kuu
la Wasambaza Nyaraka kuwa ni kufikisha nyaraka za kimahakama na zile zisizo za
kimahakama, na itajumuisha kufikisha; Wito wa Mahakamani (summonses), notisi,
nakala za hukumu, uamuzi (rulings), amri za Mahakama (decree or orders), notisi
za uteuzi kwa madalali wa Mahakama na nyaraka nyingine zozote zinazotolewa na
Mahakama.
Kwa mujibu wa Orodha ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kwa mwaka 2026/2027 iliyotolewa na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa idadi yao ni 99.
Baadhi ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Tanzania walioshiriki katika Mkutano Mkuu wakimsikiliza na kufuatilia hotuba ya Jaji Mkuu (hayupo katika) alipokuwa akifungua Mkutano huo leo tarehe 30 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.











Hakuna maoni:
Chapisha Maoni