Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Zanzibar
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani wakiongozwa na Naibu Msajili ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Joyce Mkhoi na Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bw. Nestory Mujunangoma wamefanya ziara ya kitalii visiwani Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita ikiwa ni ziara ya kujifunza pamoja na kuburudika na kufurahi kwa pamoja ili kujiweka sawa kiroho, kimwili na kiakili baada ya kazi.
Akizungumza baada ya kuhitimisha utalii huo, Mhe. Mkhoi alisema anatumaini kila mtumishi amefurahia utalii huo na kwamba baada ya hapo deni lililobaki ni kwa watumishi pindi warudipo katika Vituoni kufanya kazi kwa bidii na kwa ari mpya.
Naye Mtendaji wa Mahakama Pwani, Bw. Mujunangoma alisema dhumuni la ziara hiyo ni kupumzisha akili kutokana na kazi na vilevile kujifunza historia mbalimbali Visiwani humo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Watumishi wote, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Mkuranga, Mhe. Sameera Suleiman alisema wamefurahia utalii huo maana imewapa fursa nzuri ya kufahamiana Wilaya moja na nyingine lakini pia wamepata fursa ya kutengeneza kumbukumbu kubwa katika maisha.
Ziara hiyo ilijumuisha maeneo ya Msitu wa Jozani (Jozani Forest) ambapo watumishi hao walipata wasaa wa kubadilisha mandhari ya mjini na msituni ambapo waliweza kuona ngedere wekundu na pia kuona uwekezaji katika msitu huo.
Hali kadhalika waliweza kutembelea Shamba la Viungo (Spice Farm) ambapo walijifunza namna viungo vinavyotumika pamoja na ulimwaji, utunzwaji hadi kuvunwa kwake.
Pia walitembelea sehemu maarufu ya Forodhani na kushuhudia mandhari nzuri ya Bahari, kuzama kwa jua (Sun Set) na Mchezo maarufu wa Makachu.
Aidha, katika utalii huo walitembelea Mji maarufu wa Nungwi na kufanya utalii wa ndani ya maji kwa kutumia Jahazi linaloongozwa na upepo na pia kutembelea Makazi ya Kasa na kupata wasaa wa kuwalisha Kasa hao, pia kupata historia ya kuzaliwa, ukuaji wao na namna ya kuwatunza.
Ziara hiyo ya siku tatu ilianza tarehe 26-28 Juni, 2026 ikihusisha
Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mahakama za Wilaya za Kibaha, Kisarawe,
Mkuranga, Mafia na Rufiji. 
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (katikati) akiwa na baadhi ya watumishi wa Mahakama Pwani wakiwa katika Ziara ya Utalii Visiwani Zanzibar.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni