Jumatano, 1 Julai 2026

JESHI LA MAGEREZA LAIPONGEZA MAHAKAMA PWANI KWA KUFANYA KAZI KWA BIDII

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Jeshi la Magereza Mkoa wa Pwani wameipongeza Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani humo pamoja na Mahakama ya Wilaya Kibaha kwa kufanya kazi kwa bidii na kuondoa msongamano gerezani.

Akitoa pongezi hizo wakati wa Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama Pwani tarehe 30 Juni, 2026, Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Basili Kiwone amesema wamebakiwa na Mahabusu 21 tu tofauti na kipindi cha nyuma ambapo Mahabusu walikuwa wengi kuliko wafungwa.

Katika kikao hicho cha kusukuma mashauri kilichoongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi amesema kwa sasa Mahakama ya Hakimu Mkazi inayo mashauri mawili tu na bado hayazidi miezi sita na Mashahidi wanakuja.

Kikao hicho kimeazimia kwamba upande wa Mashtaka kuhakikisha Mashahidi wanafika Mahakamani kwa wakati, hilo ni azimio endelevu na pia kuhakikisha upelelezi unakamilika mapema ipasavyo. 

Aidha, Mhe. Mkhoi amesisitiza kuwa, upande wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mashahidi wafike kwa wakati ili mashauri hayo yasivuke miezi sita.

Akizungumza wakati wa kuwakaribisha Wadau wa Haki Jinai, Kaimu Mkuu wa Gereza la Mkuza, Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Eliatosha Yamakili alisema, siku ya jana (tarehe 30 Juni, 2026) walikuwa na Mahabusu 21 tu na Wafungwa 54 wa Kitanzania na Wafungwa Raia wa Burundi watatu, mfungwa mmoja Raia wa Ethiopia na Mzuiwa mmoja Raia wa Ethiopia, hivyo jumla yao wote wako 80 ingawa Gereza hilo lina uwezo wa kubeba Wahalifu 140.

Akieleza utekelezaji Mrakibu Msaidizi, Yamakili amesema kwa sasa wanaendelea na ujenzi wa jiko la kisasa ambalo litatumika kuandaa chakula cha Wahalifu na kwa sasa mfumo wa gesi umeshafungwa kilichobaki ni hatua ya umaliziaji tu.

Vilevile, ameeleza kwamba, Gereza hilo linafanya ukarabati wa Selo za Kike ambapo wameanza kwa kuweka sakafu mpya na kupaka rangi kwenye Selo moja, kujenga sehemu ya chakula na kupumzika.

Katika hatua ya kutekeleza dhana nzima ya urekebu Gereza hilo la Mahabusu Mkuza lilipokea ugeni wa Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Mashariki kwa madhumuni ya kuona shughuli zote za kujifunza na kuona namna bora ya kuandaa upimaji wa Wanafunzi kwa lengo la kutoa vyeti kwa watakaohitimu na kufaulu.

Naye, Mahabusu Simon Marekani akisoma risala kwa niaba ya Mahabusu na Wafungwa wenzake amewashukuru Wadau wa Haki Jinai kwa maboresho wanayoyafanya gerezani hapo licha ya kuwa zipo changamoto mbalimbali ambazo waliomba kuwasilisha kwa timu hiyo ambazo ni pamoja na upande wa mashtaka  kutopeleka mashahidi kwa wakati mpaka wapate msukumo wa Hakimu ndipo walete Mashahidi na wakati mwingine hawafiki kwa wakati ukizingatia mashauri mengi mashahidi ni Askari Polisi wa Mkoa wa Pwani.

Changamoto nyingine walizielekeza kwa Jeshi la Polisi kwa Watuhumiwa kukaa muda mrefu Kituo cha Polisi zaidi ya mwezi mmoja bila kufikishwa Mahakamani, Watuhumiwa kubadilishiwa vielelezo,  kulazimishwa kuweka saini kwa Dole Gumba kwenye maelezo wasiyoyatambua na pia Watuhumiwa kudhulumiwa mali zao hasa wakiwa Kituo cha Polisi mfano Simu, Pesa, Viatu na vitu vingine.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Haki Jinai mara baada ya kukagua Gereza la Mkuza. Wa pili kushoto ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha Mhe.  Emmael Lukumai, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mkuza, Mhe. Leah Mkono, wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mlandizi na wa pili kulia ni Mrakibu Msaidizi wa Magereza,Eliatosha Yamakili.



Wadau wa Haki Jinai wakiendelea na Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika tarehe 30 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani.

 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (kushoto) akiongoza Kikao cha Kusukuma Mashauri. Kulia ni Katibu wa kikao hicho ambaye ni Wakili wa Serikali, Bi. Laura Kimaro.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni