Jumatano, 1 Julai 2026

WADAU WA HAKI JINAI SONGWE WAKUTANA KUPANGA MIKAKATI YA UONDOSHAJI MASHAURI

Na. ELIUD KIWANGA – Mahakama, Songwe

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe, hivi karibuni ilifanya kikao cha kusukuma Mashauri ya Jinai, kikilenga kutathimni na kuimarisha usimamizi na ufanisi wa utoaji wa haki katika Masjala ya Songwe.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe na kuongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Abubakar Mrisha na kuhudhuriwa na wadau wa Haki Jinai kutoka Taasisi mbalimbali Mkoa wa Songwe.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde alisoma taarifa ya mwenendo wa Mashauri ya Haki Jinai Masjala ya Songwe kuanzia tarehe 30, Machi, 2026 mpaka tarehe 26 Juni, 2026 kwa kuainisha mashauri yote yaliyofunguliwa, mashauri yaliyomalizika na mashauri yaliyoendelea kusikilizwa.

Mhe. Minde aliaainisha changamoto zinazoathiri usikilizwa wa mashauri ya jinai na baadae zilipatiwa ufumbuzi. “Tunaomba ushirikiano wa wenu kwa Mahakama na sisi tunajitahidi kadri tunavyoweza ili kuhakikisha mashauri aliyosalia yanamalizika kwa wakati,” alisistiza.

Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Malata alisisitiza kwamba, kikao hicho kinajikita katika mikakati ya kuhakikisha mashauri ya jinai kwa ngazi ya Mahakama Kuu yanasikilizwa haraka ili kuepuka mlundikano wa Mashauri huku tukiendelea kuwahimiza wadau kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake katika mnyororo wa haki jinai ili kusaidia Mahakama kutekeleza jukumu lake la msingi ipasavyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Tawi la Songwe, Bw. Moses Mwampashi amesema, idadi ya Mawakili mkoani Songwe haitoshi ukilinganisha na uhitaji wa wananchi katika uwakilishi wa Mawakili mahakamani Songwe, aliendelea kubainisha kuwa uhitaji wa Mawakili ni mkubwa ukilinganisha na idadi ya mashauri yaliyopo mkoani humo.

Wakili huyo, ameliomba jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Songwe kusaidia ongezeko la Mawakili ili kutoa huduma ya kisheria na uwakilishi mzuri wa wananchi mahakamani kwa wakati, hatua hiyo itaiwezesha Mahakama kumaliza mashauri mapema ipasavyo.

Katika kikao hicho, Wadau wa Haki Jinai pamoja Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe waliazimia kuwa Wafungwa na Mahabusu wafikishwe kwa wakati, Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea wafike mahakamani saa moja kabla ya muda ulioandikwa kwenye Summons, kujiridhisha kwa kina juu ya mashahidi wanaofika kutoa ushahidi mahakamani.

Vilevile, wadau waliazimia kwamba, ikiwa wakili atashindwa kuendelea kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake arudishe doc brief ili wakili mwingine aweze kupangiwa shauri hilo, pia uongozi wa TLS uwakumbushe mawakili majukumu yao kisheria ikiwemo kuwatembelea mahabusu kabla ya kuletwa mahakamani, Mawakili wa Serikali na wa kujitegemea kujiandaa ipasavyo kabla ya kuingia mahakamani. Vyombo vya haki jinai kuzingatia taratibu za kisheria zinazosimamia masuala yote ya haki jinai.

Mhe. Malata aliwashukuru wadau wote waliofika katika kikao hicho na kuwasisitiza kutimiza na kutekeleza maazimio yote waliyokubaliana kwa kuzingatia sheria za haki jinai zinavyotaka, aliomba ushirikiano ili kuboresha utoaji wa haki jinai kwa wananchi.

Kikao hicho cha Wadau wa Haki Jinai Songwe kilihudhuriwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Magereza, Polisi, Ofisi ya Upelelezi Mkoa, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Ustawi wa Jamii, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Ofisi ya Uangalizi Mkoa wa Songwe na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala, Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata (katikati), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Abubakar Mrisha (kushoto) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde (kulia) wakiwa kwenye kikao cha kusukuma mashauri ya jinai.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe Mhe. Stephano Minja akifuatilia kikao hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata (katikati), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Abubakar Mrisha (kushoto) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Mahakama mara baada ya kuhitimisha kikao cha kusukuma mashauri ya jinai.

Sehemu ya wawakilishi wa baadhi ya Taasisi zilizoalikwa za haki jinai mkoani Songwe.

Kaimu Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Bw. Mohamed Kimungu Rajabu akifuatilia kikao hicho.

Sehemu ya Wadau wa Mahakama waliohudhuria kikao hicho akiwemo Bi.Tea Mshana, Bi. Maria Sanga kutoka NPS-Songwe pamoja na Bi. Geladina Theobard kutoka Ofisi ya Uangalizi-Songwe.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni