- Waweka mikakati kuboresha utoaji haki kwenye mashauri ya mirathi, madai ya fidia
Na
MWANDISHI WETU-Mahakama, Temeke
Mahakama Kituo Jumuishi cha
Masuala ya Familia Temeke hivi karibuni kilishiriki mafunzo ya kubadilishana
uzoefu na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ili kuongeza ufanisi katika
kuwahudumia wananchi, hasa katika utoaji wa haki zinazohusu fidia katika mashauri
ya mirathi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika
katika ukumbi wa Destiny Hall ulioko Kibaha katika Mkoa wa Pwani yalifunguliwa
rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa.
Katika hotuba yake ya ufunguzi,
Mhe. Mwanabaraka alisisitiza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kutatua changamoto
za ucheleweshaji wa haki kwa warithi na kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji
kati ya Taasisi hizo mbili.
Katika Kikao hicho, mada
ziliwasilishwa kuhusu Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Taratibu na changamoto
za madai ya fidia kwa wafanyakazi pamoja na taratibu za ufunguaji na uendeshaji
wa mashauri ya mirathi.
Bw. Deo Victor Ngowi kutoka
Idara ya Huduma za Sheria WCF, akiwasilisha mada kuhusu sheria inayoongoza
fidia kazini, alitoa ufafanuzi kuwa fidia hutolewa na WCF kutokana na ajali au
vifo kazini na hivyo haiwezi kudaiwa kama sehemu ya mirathi na wasimamizi wa
mirathi.
Alieleza pia kuwa fedha
hizo hazilipwi kwenye akaunti ya mirathi, bali huenda moja kwa moja kwenye
akaunti binafsi za wanufaika sahihi. Bw.
Ngowi alichambua makundi muhimu yanayolipwa na WCF ambayo ni wenza na watoto
wenye umri chini ya miaka 18.
Aidha, alieleza kuwa madai
yote ya fidia ni lazima yawasilishwe WCF ndani ya miezi 12 tangu kutokea kwa
ajali au kifo kwa mnufaika wa WCF.
Bw. Ngowi aliwaelimisha washiriki
pia juu ya nani hufaa kuwa wanafaika wa WCF kwa kusema kuwa, “WCF haihusiki na
wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi kama mikataba ya chini ya siku 30, wafanyakazi
wa kujitolea, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama.”
Meneja Msimamizi wa Ulipaji
Fidia, Bi. Rehema Mwakabongo, alipokuwa akiwasilisha mada, alieleza faida
mbalimbali zitolewazo na mfuko huo, ikiwemo gharama za matibabu ya ulemavu wa
muda au wa kudumu, msaada wa matibabu nje ya nchi, na fao la mazishi.
Alieleza changamoto
zinazojitokeza katika ulipaji wa fidia kama udanganyifu kutoka kwa wanufaika,
ikiwemo uwepo wa nyaraka zaidi ya moja ya cheti cha kifo, changamoto ya
utofauti wa majina ya walipwaji, hivyo kusababisha uwepo wa ‘deed poll’ za udanganyifu.
Bi. Rehema alielezea pia changamoto
ya waajiri na waajiriwa kuchelewa kuwasilisha nyaraka muhimu kwa ajili ya
malipo ya fidia kwa wakati, hivyo kuomba ushirikiano mkubwa na Mahakama pale
inapohitajika.
Katika kikao hicho, mada kuhusu
utaratibu wa ufunguaji mashauri ya mirathi, uendeshaji hadi kufungwa zilitolewa
na Mahakimu, Mhe. Stephanie Kagaruki Hakimu
Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Mwanzo, kwa kushirikiana na Mhe. Mhangwa Yunge,
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya.
Mahakimu hao walifafanua
mada juu ya taratibu za ufunguaji na uendeshaji wa mashauri ya mirathi, taratibu na mamlaka za Mahakama
kulingana na ngazi zake.
Mahakama za Mwanzo husikiliza
mirathi ya kiislamu na ile ya mila na desturi, Mahakama za Wilaya na Mahakama Kuu
husikiliza mirathi ya kikristo na asili ya kiasia.
Pia watoa mada walieleza
juu ya nyaraka zinazoweza kutumika ili WCF itoe malipo, nyaraka za Mahakama
kama vile fomu namba 80 kwa Mahakama Kuu na Wilaya pamoja na Fomu No.5 kwa
Mhakama ya Mwanzo zinazoonyesha orodha ya mali za marehemu.
Fomu No.81 kwa Mahakama
Kuu na Wilaya pamoja na Fomu No. 6 kwa Mahakama ya Mwanzo zinazoonyesha hesabu
za mali ya marehemu ikiwaonyesha wanufaika na walichopewa.
Watoa mada walisema muhtasari
wa kikao cha familia sio takwa la kisheria bali hutumika kama utaratibu wa
kujiridhisha. Walieleza pia hukumu inaweza kuwa nyaraka muhimu, lakini sio inayowataja
warithi halisi, hivyo ni muhimu kuthibitisha wanaostahili kulipwa.
Watoa mada walieleza kuwa
hakuna haja ya msimamizi wa mirathi kuagizwa hati ya kiapo cha uthibitisho kwa
kuwa hati ya usimamizi wa mirathi kutoka mahakamani ni uthibitisho tosha kuwa
ameteuliwa na Mahakama.
Washiriki wa mafunzo hayo
walipata nafasi ya kujadili juu ya mada zilizowasilishwa na kuibua maswali
muhimu kama vile stahiki za watoto waliozidi miaka 18 wenye changamoto maalumu
za kuwafanya kuwa chini ya uangalizi wa wazazi wao.
Mfuko wa WCF uliahidi
kuifanyia kazi changamoto hiyo kwa kuwa kwa sasa watoto wa kuanzio umri huo sio
wanufaika wa mfuko.
Kuhusu maboresho ya sheria, washiriki
waliishauri WCF kuona namna ya kurahisisha michakato, ikiwemo kuheshimu nyaraka
za Mahakama bila kuweka ulazima mkubwa wa cheti cha kifo pale ambapo Mahakama
imeshathibitisha vifo hivyo.
Kikao kazi hicho kilifungwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Gladys Barthy, ambaye aliishukuru WCF kwa fursa hiyo ya kujengeana uwezo. Ili kuhakikisha makubaliano hayo yanafanyiwa kazi kwa vitendo, Mahakama imeahidi kuteua mtu maalum (focal person) atakayekuwa kiunganishi cha haraka kati ya Mahakama Kituo Jumuishi Temeke na WCF ili kuharakisha huduma kwa wananchi.
Jaji Mfawidhiwa Mahakama Kituo Jumuishi cha
Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, akifungua mafunzo ya
kubadilishana ujuzi katika ukumbi wa Destiny Hall Kibaha Pwani.
Washiriki wa mafunzo hayo wakisikiliza
hotuba kutoka kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Wa WCF, Bw. Abrahamu Siyovelwa.
Majaji Kutoka Mahakama Kuu Kituo Jumuishi
Temeke walioshiriki katika kikao mafunzo wakifuatilia mada zilizokuwa
zinawasilishwa.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Mhe.
Stephani Kagaruki, akitoa mada juu ya
taratibu za ufunguaji wa mirathi Mahakama za Mwanzo katika kutoa haki kwa wananchi.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Mhangwa
Yunge, akitoa ufafanuzi juu ya mada za Usimamizi wa mashauri ya mirathi katika
Mahakama ya Wilaya na Mahakama Kuu Temeke.
Meneja Malipo toka WCF, Bi Rehema Kabongo, akitoa mada kuhusu taratibu za fidia kwa wafanyakazi.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Singida.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni