Alhamisi, 2 Julai 2026

“OSHA ENDELEENI KUFANYA UKAGUZI WA MIUNDOMBINU MAHALI PA KAZI; NI TAKWA LA KISHERIA”

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju ametoa rai kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuendelea kufanya ukaguzi katika miundombinu yote ya maeneo ya kazi ili kuhakikisha usalama mahali pa kazi sambamba na kutekeleza takwa la Sheria ya Afya na Usalama Kazini.

Mhe. Masaju ametoa rai hiyo leo tarehe 02 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma alipokuwa akifungua Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

“Ushauri wangu kwenu ni kwamba endeleeni kufanya ukaguzi katika miundombinu yote kama ilivyotajwa katika Sheria ya Afya na Usalama Kazini, na ikiwemo miundombinu ya Mahakama. Sababu hii ya kwenu sio utashi, ni maelekezo ya sheria. Sheria lazima itekelezwe tu," amesema Jaji Mkuu na kuongeza:

"Na Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mwaka 1988, alipokuwa anafunga mkutano wa ALAT, alisema hivi, 'Serikali ni Sheria.' Hakuna kitu kinaitwa Serikali bila sheria, na sheria zikishatungwa lazima zifuatwe.”

Mhe. Masaju aliongezea, “Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweka msingi wa Utawala wa Sheria na inamtaka kila mtu kuitii Katiba hii na Sheria za Jamhuri ya Muungano, na kwamba kila mtu ana haki ya kuchukua hatua kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa kuhakikisha hifadhi ya Katiba na Sheria za Nchi.”

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu ameipongeza OSHA, chini ya Mtendaji Mkuu Bi. Khadija Mwenda, kwa kwenda mbali zaidi ya kusimamia Sheria, kufanya mafunzo na kutoa vitendea kazi vinavyozingatia mifumo ya kiorganomia (ergonomics) ili kuwakinga watumishi na magonjwa yatokanayo na mazingira ya kazi.

Ameongeza kuwa, haki ya kuishi imewekwa katika ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nayo inasema hivi, "Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria." Amesema Sheria ya Afya na Usalama Kazini, msingi wake ni huo: watu kuishi. “Kazi hizi zisifanye tukafa, ndio maana inasisitiza... sasa ukishakufa una maana gani? Na... ukishakufa unaishia pale.”

Amesema, msingi mwingine wa Sheria ya Afya na Usalama Kazini ni Ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inayosema kwamba kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. 

“Na sasa sisi Taifa hili lina kaulimbiu inayosema, "Kazi na Utu". Tufanye hizi kazi lakini tukiwa tumezingatia utu ikiwa ni pamoja na kuzingatia ustawi wetu, kwamba hizi kazi zisifanye tukafa mapema halafu kuwepo kwetu kukawa hakuna maana yoyote,” amesema Jaji Mkuu.

Amesema, suala hilo limehusishwa moja kwa moja na Ibara ya 14 ya Katiba inayofafanua haki ya kuishi, pamoja na Ibara ya 12 inayosisitiza heshima na utu wa binadamu, ikizingatiwa Kaulimbiu ya sasa ya Taifa ya "Kazi na Utu."

"Maendeleo yanapangwa na binadamu na ni kwa ajili yao; hayawezi kupangwa na mashine wala wanyama. Ndio maana uwekezaji katika afya zao ni muhimu. Kadri mtu anavyofanikiwa, ndivyo anavyotaka kuendelea kuishi ili atoe mchango kwa Taifa lake," amesisitiza Mhe. Masaju huku akiongeza kuwa mafunzo hayo yanaendana na Nguzo ya Pili ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 inayolenga kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, motisha na ubunifu na Kipaumbele cha kwanza cha Dira hiyo kinachohusu Utawala Bora na Haki.

Jaji Mkuu ameeleza kuwa, Taifa hili linastahili ustawi wa binadamu wote, wakiwemo Wakulima kwa wafanyakazi na wafanyabiashara na kila mmoja. Amesema, “Na sisi tunaofanya kazi, wawe Mahakimu au Waamuzi kama tulivyo sisi, na kila mmoja wetu anahitaji ustawi. Mafunzo haya pia yanatupeleka kwenye utekelezwaji wa hiyo Dira kwenye ustawi, lakini imeandamana na kitu cha msingi sana: haki, hivyo Mahakama itaendelea kusimamia utoaji haki ipasavyo.”

Ameongeza kuwa, Taifa jumuishi lenye ustawi ni Taifa ambalo halimwachi mtu nyuma, huku akirejea na kupongeza mafunzo ambayo OSHA wameshatoa kwa makundi mbalimbali ya watu. 

Katika hatua nyingine; Jaji Mkuu amemshukuru Rais Samia kwa Uteuzi wa Majaji tisa wa Mahakama ya Rufani kwa jitihada zake za makusudi za kuendelea kuimarisha Mhimili huo kupitia rasilimali watu na vitendeakazi.

“Ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha Mhimili huu wa Mahakama kwa rasilimaliwatu, vitendeakazi na rasilimali nyingine ili Mhimili huu uweze kuendelea kutekeleza jukumu lake la utoaji haki kwa ufanisi zaidi. Na kwa sababu hiyo, ninamshukuru kwa uteuzi huu alioufanya mwezi uliopita na akawaapisha hawa Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani tisa kwa wakati mmoja; hilo ni kazi kubwa sana amefanya. Mheshimiwa Rais namshukuru sana sio kazi ndogo,” amesema Mhe. Masaju.

Ameongeza kuwa, “Unapomteua Jaji, umeteua watu wengine tisa nyuma yake, kwa uchache. Kwa hiyo, anapoteua ni kwamba amedhamiria kwa dhati kabisa. Na hii inaonesha utayari wake wa kuendelea kuimarisha Mhimili huu kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ipasavyo ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninamshukuru sana.”

Jaji Mkuu amesema, uamuzi wa hivi karibuni wa Mkuu wa Nchi wa kuteua na kuwaapisha Majaji tisa wa Mahakama ya Rufani kwa wakati mmoja umetajwa kama uthibitisho wa utayari wake wa dhati wa kuhakikisha haki inatendeka kwa ufanisi mkubwa nchini. 

Aidha, Jaji Mkuu amewapongeza Majaji walioteuliwa hivi karibuni, ambapo amesema, “Ninakutana nanyi mara ya kwanza katika tukio hili rasmi. Niwapongeze sana kwa mwenendo wenu mwema, kuwa na sifa za kuweza kuteuliwa hata kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani. Na Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki sana katika maisha yenu, katika utumishi wenu, na katika shughuli zenu.”

Kadhalika Mhe. Masaju amempongeza Jaji Mlyambina aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama kwa kuwa na ushirikiano mzuri na Wadau wa Haki Kazi ambapo umeiwezesha Mahakama kunufaika na mambo mengi ikiwemo mafunzo kwa Watumishi wake wakiwemo Majaji, Naibu Wasajili, Mahakimu, Madereva na kadhalika.

Viongozi wengine wakuu waliohudhuria tukio hilo ni pamoja na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe.Dkt. Paul Faustine Kihwelo, Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu, baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania, Watumishi wa OSHA, watumishi wengine wa Mahakama.

Wengine waliohudhuria ni pamoja na Wataalamu Wabobezi/Madaktari na Wauguzi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Muhimbili (MUHAS) na Taasisi ya Mifupa (MOI).

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akifungua Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 02 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Sehemu ya Majaji na Viongozi wengine wa Mahakama na OSHA wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 02 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 02 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akitoa neno wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 02 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda akitoa neno wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 02 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (kushoto) pamoja na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Victor Kategere wakiwa katika hafla ya ufunguzi wa Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 02 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu-Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick (kulia) pamoja na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bw. Victor Kategere wakifuatilia kinachojiri katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akimpatia zawadi ya saa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda baada ya hafla ufunguzi wa Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 02 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (kulia) akimpatia zawadi Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju ya Vifaa tiba vya huduma ya kwanza (First Aid Tool Box) baada ya hafla ufunguzi wa Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 02 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Majaji wapya Mahakama ya Rufani (waliosimama) wanaopatiwa mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa Kazi yanayotolewa na OSHA. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma (aliyesimama). Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania (waliosimama). Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa OSHA (waliosimama). Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda.

Meza Kuu katika picha ya pamoja na Wataalamu wa Afya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI.

Meza Kuu katika picha ya pamoja na Wawezeshaji wa Mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa Kazi yanayotolewa na Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda.

(Picha na MARY GWERA & JEREMIA LUBANGO, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni