Jumatatu, 29 Juni 2026

MENEJIMENTI MASJALA NDOGO MBEYA YAFANYA TATHMINI YA UTENDAJI KAZI ROBO YA NNE

Na. MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Menejimenti ya Mahakama Masjala Ndogo ya Mbeya hivi karibuni ilifanya kikao cha tathmini ya utendaji kazi kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, kwa lengo la kupitia utekelezaji wa majukumu ya kimahakama, kiutawala pamoja na kuweka mikakati ya kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Kikao hicho kiliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, na kuwakutanisha Majaji, viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya za Masjala Ndogo ya Mbeya pamoja na Maafisa mbalimbali kutoka katika Mahakama hizo.

Aidha, kila Mahakama iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake kwa robo ya nne, zikijumuisha usimamizi wa rasilimali watu, matumizi ya fedha, manunuzi na ugavi, hali ya mashauri, upimaji wa utendaji kazi pamoja na utoaji wa motisha kwa watumishi.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Mtulya alisisitiza umuhimu wa kuzingatia usawa katika kuwathamini watumishi ili kuongeza ari ya kazi na kuimarisha utendaji katika Mahakama zote za Masjala hiyo.

“Katika kuboresha utendaji kazi, nasisitiza kuwepo na usawa wa utoaji wa stahiki na motisha kwa watumishi wa mahakama zote katika Masjala nzima ya Mbeya, kuanzia Mahakama Kuu hadi Mahakama za Mwanzo,” alisema Mhe. Mtulya.

Taarifa zilizowasilishwa zilionesha mafanikio mbalimbali mathalani kusikiliza na umalizaji wa mashauri yaliyopangwa, matumizi bora ya fedha kwa kuzingatia vipaumbele vya ofisi, kupunguza msongamano wa wafungwa na Mahabusu magerezani kupitia usikilizaji wa mashauri na kuendelea kudumisha ushirikiano mzuri na wadau wa Mahakama,

Aidha, kikao hicho pia kilibaini changamoto mbalimbali zinazohitaji kufanyiwa kazi, miongoni mwa changamoto hizo ni uchakavu wa vyombo vya usafiri unaosababisha kuongezeka kwa gharama za matengenezo, uchakavu wa majengo hususan Mahakama za Mwanzo, ufinyu wa bajeti pamoja na upungufu wa watumishi.

Mwenyekiti alisisitiza umuhimu wa kuendeleza usimamizi madhubuti wa rasilimali zilizopo, kuimarisha uwajibikaji na kuendelea kushirikiana katika kutafuta suluhisho la changamoto zilizojitokeza ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za Mahakama na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiongoza kikao hicho cha menejimenti, wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo (kulia) na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bi. Mavis Fransis Miti.

Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer akiwasilisha taarifa ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya.

Sehemu ya washiriki katika kikao hicho wakimfuatilia kwa makini Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani).

Sehemu ya washiriki katika kikao hicho wakimfuatilia kwa makini Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani).

Sehemu ya washiriki katika kikao hicho wakimfuatilia kwa makini Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani).

Sehemu ya washiriki katika kikao hicho wakimfuatilia kwa makini Mwenyekiti wa kikao hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani).

Afisa Utumishi Mahakama ya Wilaya Mbeya Bi. Odilia Mapunda (katikati) akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi kwa Mahakama ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo. 






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni