Jumatatu, 29 Juni 2026

KAMPENI YA KUPANDA MITI YASHIKA KASI MAHAKAMA ZA MWANZO KIGOMA

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa hivi karibuni aliwaongoza watumishi wa Masjala hiyo na Mahakama ya Mwanzo Bangwe kupanda miti ya kivuli na matunda katika maeneo ya wazi yaliyopo katika Mahakama hiyo mpya iliyofunguliwa na kuanza kazi.

Upandaji miti huo ni Kampeni inayosimamiwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, ambaye mara kadhaa katika ziara zake amekuwa akipanda miti katika Mahakama husika anapotembelea, hata hivyo amekuwa akisisitiza kuwa miti hutunza uoto wa asili, kutunza miundombinu ya majengo ya Mahakama pamoja na kulinda mipaka ya maeneo ya Mahakama hizo sambamba na kuvutia kwa mandhari nzuri iliyopambwa na miti hiyo.

Aidha, Mhe. Rwizile amenukuliwa mara kadha katika vikao vya watumishi akisema, “tumekuwa na maeneo ya Mahakama zetu ambayo yapo wazi sana, hivyo tusipoweka mikakati ya makusudi ya  kuyalinda maeneo hayo, basi tunaweza kuyapoteza kwa watu wengine kuyatumia, maana hatuna alama zinazolinda maeneo hayo, ni rai yangu Uongozi wa Mahakama za Wilaya zote, kuandaa utaratibu wa kupanda miti katika maeneo hayo kuanzia Mahakama za Mwanzo sambamba na viwanja vipya vya Mahakama za Kata na nyumba za Mahakimu, hasa ambavyo vimepatikana na upimaji umefanyika na kukabidhiwa viwanja hivyo.”

Vilevile, watumishi wametumia muda wa asubuhi kabla ya shughuli za Mahakama kuanza, ili kutekeleza jukumu hilo, ambapo wamepanda miti hiyo na kuahidi kuitunza hususan katika kipindi hiki cha kiangazi ambapo miti hiyo inahitaji maji ya kutosha ili kustawi vizuri.

Kampeni hiyo pia ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ikiwa ni pamoja na maelekezo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050, inayotaka kuwa na Tanzania ya kijani, hivyo, Mahakama Kuu Kigoma imeendelea kuhakikisha maeneo yote ya Mahakama yanavutia kwa miti mizuri inayopandwa kwa mpangilio mzuri na wenye kuleta mvuto wa mazingira ya Mahakama zote Mkoani humo.

Zoezi hilo la kupanda miti lilihudhuriwa na Viongozi wa Mahakama Kigoma akiwemo Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bw. Yusuph Kasuka, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya mwanzo Bangwe, Mhe. Florence Ikorongo pamoja na Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Valerian Msola, Ofisa Utumishi Mwandamizi, Bw. Festo Sanga na Watumishi wa Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma na Mahakama ya Mwanzo Bangwe.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya  Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akipanda Mti wa Mpapai katika eneo la wazi lililoandaliwa kupandwa miti Mahakama ya Mwanzo Bangwe.

Mtendaji  wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya  Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akipanda mti wa kivuli katika eneo la Mahakama ya Mwanzo Bangwe.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Bangwe, Mhe. Florence Ikorongo akipanda Mti wa Kivuli katika eneo la Mahakama ya Mwanzo Bangwe.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya  Kigoma,  Mhe. Valerian Msola akipanda Mti wa Mpapai katika eneo la wazi liloandaliwa kupandwa miti Mahakama ya Mwanzo Bangwe.

Ofisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Festo Sanga akipanda Mti wa Kivuli katika eneo la wazi liloandaliwa kupandwa miti Mahakama ya Mwanzo Bangwe.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kigoma walioshiriki kupanda miti hivi karibuni katika eneo la wazi liloandaliwa kupandwa miti katika Mahakama ya Mwanzo Bangwe.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni