Jumatatu, 29 Juni 2026

MASJALA NDOGO MBEYA YAKUTANA NA WADAU WA HAKI MADAI

 Na. MUKSINI NAKUVAMBA - Mahakama, Mbeya

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Mbeya, hivi karibuni ilifanya kikao cha kusukuma mashauri ya madai (Bench-Bar Meeting) kwa lengo la kutathmini mwenendo wa mashauri ya madai na kuweka mikakati ya kuhakikisha mashauri hayo yanamalizika kwa wakati, kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya.

Kikao hicho kiliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya na kuhudhuriwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Judith Lyimo, Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer pamoja na wadau wengine wa haki madai.

Katika kikao hicho, wajumbe walipokea taarifa kuhusu hali ya mashauri ya madai, ikiwemo mashauri yaliyomalizika, yaliyobaki, mashauri yaliyoitishwa kutoka mabaraza mbalimbali pamoja na mashauri ya mlundikano.

Aidha, wajumbe wa kikao hicho, walijadili mikakati ya kuhakikisha mashauri ya mlundikano na yale yanayokaribia kuwa ya mlundikano yanashughulikiwa na kukamilishwa kwa wakati ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa haki kwa wakati mapema ipasavyo.

Vilevile, miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni changamoto ya baadhi ya mawakili kutokuzingatia ratiba na taratibu zilizowekwa na Mahakama katika uendeshaji wa mashauri, hali inayochangia ucheleweshaji wa usikilizwaji wa baadhi ya mashauri.

Kwa upande wao, Mawakili wa Kujitegemea kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society - TLS) walipendekeza kuwa pale ambapo Jaji au Hakimu hatakuwa na uwezo wa kuendelea na usikilizaji wa shauri kwa siku iliyopangwa, taarifa itolewe mapema kwa mawakili ili kuwawezesha kupanga ratiba zao nyingine na kutumia muda wao kwa ufanisi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Mtulya alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Mahakama na wadau wote wa sekta ya sheria katika kuhakikisha mashauri ya madai yanasikilizwa na kuamuliwa kwa wakati, sambamba na kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (kushoto) akiongoza kikao cha kusukuma Mashauri ya Madai, kulia nia Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Judith Timoth Lyimo.

Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer (kushoto) akiwasilisha taarifa ya mashauri ya haki madai wakati wa kikao hicho.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Mbeya Mhe. Paul Rupia akiwasilisha Taarifa ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya katika kikao hicho.

Sehemu ya washiriki katika kikao hicho wakimfuatilia kwa makini Mwenyekiti wa kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani).

Sehemu ya washiriki katika kikao hicho wakimfuatilia kwa makini Mwenyekiti wa kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani).








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni