·
Asisitiza Ushirikiano na Ubunifu katika Utoaji Haki
Na HALIMA MNETE, Mahakama-Dodoma
Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John
Anthony Jingu, amesema atahakikisha anaendeleza mafanikio yaliyofikiwa na
Mahakama ya Tanzania sambamba na kuleta ubunifu mpya utakaozidi kuimarisha
utoaji wa haki nchini.
Dkt. Jingu ametoa kauli hiyo jana tarehe 24 Juni, 2026 katika kikao maalum cha Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha
rasmi Mtendaji Mkuu huyo mpya wa Mahakama na kumuaga kwa heshima Mtendaji Mkuu
mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel baada ya kuhitimisha utumishi wake wakati wa
hafla ya makabidhiano ya ofisi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Jaji Mkuu, Makao
Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Jingu amemshukuru Mhe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani
kubwa aliyomuwekea kwa kumteua kushika nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama,
akisema uteuzi huo ni heshima kubwa kwake na dhamana nzito inayohitaji
kujituma, uadilifu na unyenyekevu wa hali ya juu.
Amesema amepokea dhamana hiyo kwa heshima kubwa akitambua
uzito wa majukumu yanayoambatana na nafasi hiyo, huku akiahidi kuyatekeleza kwa
bidii na kwa moyo wa kuitumikia nchi.
“Ninapokea dhamana hii kwa heshima kubwa na unyenyekevu.
Ninafahamu uzito wa jukumu hili na matarajio makubwa yaliyopo. Kwangu,
utekelezaji wa nafasi hii si wajibu wa kawaida bali ni ibada na huduma kwa
taifa,” alisema Dkt. Jingu.
Aidha, alisema mwelekeo wa uongozi wa Serikali chini ya Rais
Samia umejikita katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, usalama na
ustawi wa wananchi, huku taasisi za umma zikiendelea kuwahudumia wananchi kwa
ufanisi na uwajibikaji. Alisisitiza kuwa Mahakama kama mhimili muhimu wa dola
ina nafasi ya kipekee katika kufanikisha maelekezo hayo kupitia utoaji wa haki
wenye usawa, weledi na uadilifu.
Dkt. Jingu amesema atayapokea na kuyafanyia kazi maelekezo
ya Rais kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha Mahakama inaendelea kuwa taasisi
imara inayojenga imani kwa wananchi.
“Maelekezo ya Mhe. Rais ni dira muhimu katika utekelezaji wa
majukumu yetu. Tutahakikisha Mahakama inaendelea kutimiza wajibu wake kwa
viwango vinavyotarajiwa na wananchi wa Tanzania,” ameongeza.
Pamoja na hayo, Dkt. Jingu amempongeza Mtendaji Mkuu Mstaafu
wa Mahakama, Prof. Ole Gabriel, kwa uongozi wake wa mafanikio na mchango mkubwa
alioutoa katika kuimarisha utendaji wa Mahakama kwa kipindi chote cha utumishi
wake.
Amesema Prof. Gabriel ameacha alama kubwa ndani ya Mahakama
kupitia uongozi wake uliosaidia kusukuma mbele mageuzi mbalimbali ya kimfumo na
kiutendaji yaliyoongeza ufanisi katika utoaji haki.
Dkt. Jingu pia amempongeza Prof. Gabriel kwa kustaafu akiwa
na afya njema, akieleza kuwa hali hiyo ni ushahidi wa maisha yenye nidhamu
pamoja na umuhimu wa kuwa na familia bora inayotoa upendo, utulivu na msaada wa
karibu.
“Tumeshuhudia Prof. Gabriel akihitimisha utumishi wake akiwa
mwenye afya njema, jambo ambalo ni la kujivunia. Hii inaonesha umuhimu wa kuwa
na familia bora na mazingira mazuri ya maisha yanayompa mtu utulivu na nguvu ya
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” ameeleza.
Aidha, alisema nasaha na hekima zilizotolewa na Prof.
Gabriel wakati wa makabidhiano hazitapuuzwa, badala yake zitafanyiwa kazi kwa
vitendo ili kuendeleza misingi mizuri iliyoachwa.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya taasisi hayawezi kupatikana
kwa juhudi za mtu mmoja pekee bali yanahitaji ushirikiano wa viongozi na
watumishi wote.
“Ujenzi wa Taasisi imara si kazi ya mtu mmoja. Tunahitaji
kushirikiana, kusaidiana na kujengana ili tuweze kufikia malengo yetu ya
pamoja,” amesema.
Dkt. Jingu amewahimiza Viongozi na watumishi wa Mahakama
kuendelea kumpa ushirikiano pamoja na kumwelekeza pale inapohitajika, akisema
bado yupo katika mchakato wa kujifunza na yuko tayari kupokea maarifa mapya
kutoka kwa wote wenye uzoefu.
“Tutaendeleza yote mazuri tuliyoyakuta, lakini pia tutaleta
mawazo mapya, ubunifu mpya na mifumo mipya itakayozidi kuimarisha utendaji wa
Mahakama,” amesema.
Aliongeza kuwa, Mahakama haipaswi kujikita katika tafsiri ya sheria pekee, bali pia katika kuzingatia utu, maadili na ubinadamu katika utoaji wa huduma kwa wananchi, ili haki itolewe kwa namna inayolinda hadhi ya kila mmoja.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu akitoa neno wakati wa kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu huyo na kumuaga Mtendaji Mkuu Mstaafu, Prof. Elisante Ole Gabriel kilichofanyika tarehe 24 Juni, 2026 kwenye Ukumbi wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu wakati wa kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu huyo mpya wa Mahakama na kumuaga kwa heshima Mtendaji Mkuu mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel kilichofanyika tarehe 24 Juni, 2026 kwenye Ukumbi wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni