·
Asema Rais Samia anasimamia kwa dhati
kauli yake ya kuitaka Mahakama ya Tanzania kuwa Mhimili wenye hadhi Duniani
·
Amshukuru pia kwa Uteuzi wa Mtendaji
Mkuu mpya
·
Awataka watumishi wote wa Mahakama
kumpa ushirikiano Mtendaji huyo
·
Ampongeza Prof. Ole Gabriel kwa kazi
nzuri na kustaafu kwa heshima
·
Awakumbusha watumishi wa Mahakama
kuzingatia Utii na Bidii katika Utumishi
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kuuimarisha Mhimili wa Mahakama nchini kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo uteuzi wa Majaji, ongezeko la bajeti na masuala mengine.
Mhe. Masaju aliyasema haya jana tarehe 24 Juni, 2026 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma wakati wa kikao maalum kati yake na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha Kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Antony Jingu na kumuaga kwa heshima Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel.
“Sisi tuna wajibu wa kumshukuru Mhe. Rais kwa nia yake ya dhati ya kabisa kuona kwamba Mhimili huu unatekeleza wajibu wake wa kutoa haki kwa ufanisi ipasavyo ili kusogeza mbele ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa,” alisema Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amesema kuwa, Rais Mhe.
Dkt. Samia anaendelea kuiishi kauli yake ya kuiwezesha Mahakama ili kuhakikisha
Mhimili huo unakuwa moja kati ya Mihimili yenye hadhi duniani kauli jambo
ambalo alimuelekeza Jaji Mkuu kulisimamia alipomuapisha tarehe 15 Juni, 2025 na
vilevile kulisisitiza alipomuapisha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama tarehe 19
Juni, 2026.
Ameongeza, kwa kumshukuru Mhe. Dkt.
Samia kwa kuendelea kuongeza bajeti ya Mahakama hata katika mazingira magumu,
kuendelea kuiwezesha Mahakama kwenye rasilimaliwatu, vitendea kazi.
“Mwaka uliopita, tumeona na
tumeshuhudia kwa mfano ukiacha majengo ambayo ni kitendea kazi kikubwa sana,
magari, uteuzi wa Majaji, ongezeko la nafasi za ajira, Huduma ya
Bima ya Afya kwa Watumishi mambo
ambayo yanaongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi,” amesema.
“Namshukuru pia Mhe. Rais kwa
kumteua Dkt. Jingu kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Dkt. Jingu wewe unakuwa wa
nne, namba nne ina maana kubwa sana kiroho, bahati ndio unarithi kwa Mtendaji
Mkuu Mstaafu ambaye amefanya vizuri ambaye mmekuwa na mahusiano mazuri,
anakurithisha na timu nzuri hii ya Menejimenti tuna kila sababu ya kuendelea
kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwangu mimi ni faraja kubwa sana kwamba Mhe. Rais
alikuona ndio maana namshukuru kwa kukuteua,” amesisitiza Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu ameeleza kuwa, “kadri
unavyokuwa na madaraka makubwa ndivyo unavyozidi kuwa tegemezi kwa watu wengine
zaidi na kwa kadri hiyo hiyo ndivyo unavyopasawa kuwa mnyenyekevu ili hao
unaowategemea wakufanyie kazi zao wakufikie na wewe wakufikie ujue changamoto
zao ili wakusaidie ili muende.”
Ameongeza kuwa, “kadri unavyokuwa na
madaraka makubwa ni kwa kiwango hicho hicho unazidi kuwa mtumishi wa wote. Sasa
ndugu yangu huu utumishi umehamia kwako, sasa wewe ni mtumishi wa wote sisi
tunakutegemea yaani mpaka yule Hakimu aliyepo Mahakama ya Mwanzo na Mhudumu
wake na Karani wake wote wanakutegemea wewe.”
Aidha, Jaji Mkuu amemtaka Mtendaji
Mkuu mpya wa Mahakama kuendeleza ushirikiano na mahusiano mazuri na wadau wa
Mahakama sambamba na kuendeleza yote mazuri aliyoacha mtangulizi wake Prof. Ole
Gabriel pamoja na kuwa mbunifu kwa kuanzisha mambo mengine zaidi ili
kuhakikisha kwamba mipango iliyopo inatekelezwa kwa ufanisi ipasavyo.
Vilevile, Mhe. Masaju amemtaka Dkt. Jingu
kuendeleza na kumaliza miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama nchini ili
wananchi waweze huduma ya haki. Ametoa mifano ya majengo yanayotakiwa
kumalizika mwaka huu ikiwa ni pamoja na majengo ya Mahakama za Wilaya Mkalama na Chamwino na mengine ili kuwaondolea shida wanayopata wananchi wa
maeneo hayo kufuata huduma ya haki mbali.
Kadhalika, katika kikao hicho, Mhe.
Masaju amekumbusha mambo muhimu ya kuzingatia katika utumishi wa umma ambayo ni
pamoja na bidii ya kazi na utii kwa mamlaka.
“Mtumishi lazima awe na bidii ya
kazi, lakini mtumishi lazima awe mtii maana asipokuwa mtii huyo hawezi tena
kuwa mtumishi, na kosa kubwa sana katika utumishi wa umma ‘Insurbodination’
kudharau/kutotii mamlaka,” amesisitiza Mhe. Masaju huku akiwataka wajumbe wa
Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania na watumishi wa kumtii na kumpa ushirikiano
Mtendaji Mkuu mpya.
Aidha, Jaji Mkuu amesema, Utii
unabeba mambo mengi ambayo ni pamoja na kutii Katiba na Sheria za Nchi kama
inavyotajwa katika Ibara ya 26 na kutii masuala yote yanayohusu maadili ya
Taasisi unayofanyia kazi, kutii maelekezo yoyote ambayo ni halali, na kwamba
mtumishi akiweza kuzingatia hayo ndio umuhimu wake unazidi kuonekana.
Kadhalika, Mhe. Masaju amezungumzia
kuhusu suala la kuendelea kuimarisha ushirikiano na mahusiano na wadau wengine Serikalini
na Bunge.
Katika hatua nyingine Mhe. Masaju
amemdokeza Mtendaji Mkuu, Dkt. Jingu juu ya Kaulimbiu ya Mahakama ya mwaka
2026; ‘Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa.’ Amesema,
“Mimi mara nyingi natembeaga na Dira ya Taifa ya Maendeleo, ukiangalia ule
msingi mkuu wa Dira, akaangalia na vile vipaumbele vyake vinne, ukaangalie na
zile nguzo tatu unakuta yote yale ni masuala ya Utawala wa Sheria, ili twende
tufikie hiyo hatua tunayotaka lazima
tuziishi sheria kwa sababu kila kitu kinasimamiwa na kutawaliwa na sheria.”
“Zipo sheria sasa hivi ninafanya
kazi hapa, nina kila kipengele kilichoainishwa pale na sheria zake, unapoenda
nguzo ya tatu Tabia Nchi na Mazingira tayari tunaainisha Sheria zinazohusika,
lakini Katiba ikiwa kila sehemu, unapoenda Nguzo ya Pili ‘Human Capacity and
Development’ ile ina sheria zake, unapoenda nguzo ya kwanza ya Uchumi nayo ina
sheria zake,” ameeleza Jaji Mkuu.
Ameongeza kuwa, katika Vipaumbele na
Msingi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 vinazungumza juu ya Utawala,
Usalama, Amani, Utulivu. Amesema, ni vema kusimamia na kutekeleza ipasavyo
sheria mbalimbali ambazo zinaendana na vipaumbele vya Dira hiyo ambavyo ni Utawala
Bora na Haki, Serikali za Mitaa Imara zinazowajibika, Utumishi wa Umma
Unaowajibika na Amani, Usalama na Utulivu.
“Zipo sheria zinazosimamia masuala
hayo, mfano zipo Sheria zinazosimamia Amani, Usalama na Utulivu ambazo ni
pamoja na Sheria za Polisi, Sheria za Usalama, Sheria za Madawa ya Kulevya, na
kadhalika. Na kwa namna hiyo Taifa ndipo linapoweza kustawi na likawa na
maendeleo,” amesema Mhe. Masaju na kumpongeza Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama
kwa kuonesha kuielewa vizuri Dira hiyo sambamba na kuelewa maelekezo ya Rais
Samia ya kutaka Mhimili wa Mahakama ya Tanzania uwe moja ya Mihimili yenye
hadhi Duniani.
Amesema zipo sheria mbalimbali
zinazosimamia masuala mbalimbali, mfano sheria za kilimo, uvuvi, ufugaji,
biashara na nyingine nyingi.
Aidha, katika hotuba yake Jaji Mkuu
amempongeza Mtendaji Mkuu Mstaafu kwa Taarifa ya Makabidhiano iliyoandaliwa kwa
kina na kuelekeza kuwa, taarifa hiyo ambayo ipo kwenye kitabu isambazwe katika
Mahakama zote nchini ili itumike kama kitendea kazi katika utekelezaji wa
shughuli za Mahakama.
“Nimshukuru Mhe. Rais, moja kwa
kukuteua katika nafasi mbalimbali na mpaka sasa kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, kazi ambayo umeifanya kwa ufanisi mkubwa sana ukiwa umerithi kwa
Watangulizi wako, umemsema Mhe. Balozi Hussein Kattanga na Ndugu Mathias Kabunduguru.
Sasa umefanya vizuri kwa ufanisi mkubwa sana, mwaka mmoja ambao tumefanya kazi
wote hapa, kuna mambo makubwa sana ambayo yamefanyika,” amesema Jaji Mkuu.
“Nimeona hii taarifa nzuri
uliyoandaa, sisi kama Viongozi ndivyo tunavyopaswa kufanya, tunarithishana kwa
namna hii, hii nyaraka kwanza inasomeka kirahisi na inafaa kwa matumizi, hii ni
nyaraka ya kudumu na ina maana kubwa sana. Sasa taarifa haikumaanisha iwe kati
ya Prof. Ole Gabriel na Dkt. Jingu bali taarifa hii inatuhusu sisi sote, sisi
Menejimenti tukiwa injini ya uongozi wa Mahakama ya Tanzania, hii inamuhusu
kila mmoja wetu, kwahiyo mlizingatie tulifanyie kazi,” amesisitiza.
Mhe. Masaju amempongeza Prof. Ole
Gabriel kwa alichokifanya na kusema kwamba, utumishi wa umma ndivyo unapaswa
kuwa hivyo kutokuoneana wivu, kutokuhujumiana, kutokuoneana.
Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipokuwa akitoa neno wakati wa
Kikao maalum kati yake na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha Kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Antony Jingu na kumuaga Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu yaWajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania. Kushoto ni Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (kushoto) na kulia Mtendaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.









Hakuna maoni:
Chapisha Maoni