Alhamisi, 25 Juni 2026

JAJI BAHATI AFANYA ZIARA YA KIKAZI GEREZA LA MIFUGO UBENA

  ·       Achangia Matofali Wodi ya Wazazi katika Gereza hilo

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Kibaha

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Angela Bahati amefanya ziara ya kikazi katika Gereza la Mifugo Ubena na kufanikiwa kuchangia Tofali za ujenzi wa kuboresha Wodi ya Wazazi katika Kituo cha Afya cha Gereza ambacho ameonesha kutoridhishwa nacho.

Akiwa katika ziara hiyo jana tarehe 24 Juni, 2026, Mhe. Bahati alisema hajaridhishwa na hali ya wodi hiyo ambayo  iko katika hali ya kuchakaa na hivyo akasema na yeye atachangia matofali ili wodi hiyo ya wazazi iboreshwe.

Akizungumza kuhusu dhumuni la ukaguzi huo, Jaji Bahati alisema Mahakama na Wadau wa Haki Jinai wajibu wao ni kuangalia mazingira pamoja na haki za wafungwa kama zinafuatwa kulingana na sheria, kama kuna hukumu zinatolewa na ambao hawajapata nakala za hukumu, kupokea na kufanyia kazi malalamiko yoyote kuhusu hali zao na kama kuna utengano kati ya watu wa makundi tofauti.

Lakini pia kama kuna malalamiko yoyote yaliyo ndani ya uwezo wao wanayatatua na yaliyo nje ya uwezo wao wanatakiwa kuyapeleka mbele.

Naye Kaimu Mkuu wa Gereza la Mifugo Ubena, Mrakibu wa Magereza Simon Metta akitoa historia ya Gereza hilo amesema, Ubena ni Gereza la wazi lililoanzishwa mwaka 1964 kwa madhumuni ya kuhifadhi wafungwa waliokuwa Watumishi wa Serikali. Japo kwa sasa linahifadhi wafungwa pamoja na mahabusu wenye mashauri mbalimbali.

Akitoa taarifa wakati wa ziara ya ukaguzi wa Gereza hilo Mrakibu wa Magereza, Simon Metta amesema shughuli kubwa ya gereza hilo ni ufugaji wa Ng’ombe wa nyama aina ya Borani na pia mifugo wengine kama Mbuzi, Kondoo, Bata na Kuku wa Kienyeji.

Amesema pamoja na mifungo pia wanafanya shughuli za Kilimo cha mahindi, mboga mboga (Bustani) upandaji wa miti mbalimbali  ikiwemo miti ya matunda, mbao na kivuli.

Pia Mrakibu Metta ameendelea kusema kwamba wafungwa na Mahabusu wa Gereza hilo wanaendelea wanapata huduma ya lishe vizuri. Na pia wanatembelewa na ndugu zao kila siku za mwisho wa juma na siku za sikukuu na pia wanatembelewa na Viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo Kamati ya Haki Jinai kwa ajili ya kusikiliza kero zao mbalimbali zinazohusu kesi zinazowakabili.

Vilevile Mrakibu Metta amesema, huduma za ustawi wa Wafungwa na Mahabusu zinatolewa kwa kutumia Ofisa Ustawi wa Jamii wa Magereza, Wafungwa na Mahabusu wanapata fursa ya kufanya mazoezi ya viungo  kila siku asubuhi baada ya mafungulio.

Lakini pia Mrakibu ameeleza changamoto zinazolikabili Gereza hilo ni pamoja na ikiwemo ukosefu wa huduma ya Mahakama Mtandao yaani ukosefu wa vifaa kuwezesha Mahakama Mtandao, uhaba wa mablanketi na uchakavu wa magodoro ya kulalia.

Amesema, changamoto hizo zinaendelea kushughulikiwa  na Uongozi wa Kituo na zipo katika hatua mbalimbali.

Akiendelea kusoma taarifa hiyo Mrakibu Metta ametoa idadi ya mifugo iliyopo kwa siku hiyo gerezani hapo ikiwa ni pamoja na Ng’ombe 570, Kondoo238, Mbuzi 230, Kuku wa Kienyeji 271, Bata wa kienyeji 42 na Bata weupe 02. Jumla ya mifugo yote ni 1,353.

Ameongeza kuwa, Gereza la Mifugo Ubena limeanzisha Mradi wa Gesi Vunde kupitia kinyesi cha mifugo na Mradi huo unakaribia kukamilika ili nishati hiyo iweze kutumika ili kupunguza gharama za nishati.

Naye Mfungwa namba 185, Christopher akisoma taarifa ya wafungwa na mahabusu wa Gereza hilo amemuomba Mhe. Bahati kuwa, Kituo cha Lugoba wapatiwe Hakimu wa kukaa hapo ili Mahakama ianze kusikiliza mashauri mapema na kusikiliza mashauri mengi zaidi.

Pia wameomba kupatiwa vifaa vya Mahakama Mtandao ili wakati mwingine mashauri yao yasikilizwe kwa njia ya mtandao wakiwa hapohapo gerezani.

Mahabusu hao wameushukuru Uongozi wa Magereza kwa kuwalea katika misingi ya haki za binadamu na malezi bora ya urekebu kwa kutoa elimu ya mafunzo na ufundi kama njia ya kurekebisha fikra za kihalifu na kuwa raia wema wanapotoka gerezani.

Pamoja na kupatiwa ujuzi mbalimbali ili uweze kuwasaidia  uraiani, amesema gerezani hapo wanajifunza ushonaji kwa njia ya cherehani, ujenzi, ufyatuaji wa matofali ya kuchoma na ya sementi, kilimo cha mbogamboga, ufugaji na uhifadhi wa malisho  ya mifugo, unenepeshaji na uhimilishaji wa mifugo na utunzaji wa mazingira.

Pia gerezani hapo inatolewa elimu kwa wasiojua kusoma na kuandika na hata elimu za ujasiriamali na saikolojia kwa wengine wanaojua kusoma na kuandika.

Wamesema wanaaamini kupitia stadi hizo za kazi wanazofundishwa  zitawasaidia kubadili mwenendo wao watakapomaliza vifungo vyao.

Ziara hiyo imehusisha wadau wa haki jinai wa Mkoa wa Pwani.

 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe, Angela Bahati (wa pili kushoto) akipokea maelekezo ya Kituo cha Afya cha Gereza la Mifugo Ubena kutoka kwa Daktari wa Kituo hicho Mkaguzi wa Magereza Christina Gunzu wakati wa ziara yake katika Gereza hilo.

 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Angela Bahati  (wanne kulia) akipokea taarifa ya ujenzi wa Mradi wa Gesi Vunde kutoka kwa Mhandisi wa Mradi huo, Mhandisi  Robert Makapu (wa kwanza kulia) kutoka Kampuni ya Kamatek.

Ujenzi wa Mradi wa Gesi Vunde ukiendelea katika Gereza la Mifugo Ubena.


 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Angela Bahati  akizungumza baada ya kupokea taarifa ya Kaimu Mkuu wa Gereza la Mifugo Ubena (hayupo katika picha).

Kaimu Mkuu wa Gereza la Mifugo Ubena, Mrakibu wa Magereza Simon Metta (aliyesimama) akitoa taarifa ya Gereza hilo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Angela Bahati (aliyeketi mbele). Wa kwanza kutoka kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Joyce Mkhoi, anayefuata ni Mhe. Hussein Mushi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

(Habari imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni