Alhamisi, 25 Juni 2026

JAJI KIONGOZI AHITIMISHA ZIARA YA MAHAKAMA MKOANI RUVUMA

  • Ataka ufanisi katika kutekeleza majukumu ili kuongeza imani ya Wananchi kwa Mahakama
  • Ahimiza Watumishi kutambua maeneo Mahakama inayolalamikiwa na kuchukua hatua

Na FAUSTINE KAPAMA na Noel Daud-Mahakama, Songea

Ziara ya kimahakama ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, aliyokuwa anaifanya kukagua Mahakama na Magereza mkoani Ruvuma, imehitimishwa leo tarehe 25 Juni, 2026.

Mhe. Dkt. Siyani amehitimsha ziara hiyo kwa kukagua Gereza la Wafungwa na Mahabusu Tunduru na Mahakama ya Wilaya Tunduru na kisha kuongea na Watumishi wa Mahakama hiyo na baadaye Wawakilishi wa Watumishi wa Mahakama Masjala Ndogo Songea.

Katika kikao cha majumuisho, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma, Bw. Ginaweda Nashoni, waliwasilisha hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Watumishi, Wafungwa na Mahabusu wakati wa ziara hiyo.

Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na maslahi ya Watumishi wa Mahakama katika Masjala Ndogo Songea, kwa Wafungwa na Mahabusu kucheleweshwa kupata nakala za hukumu na vitabu vya rufaa katika Mahakama ya Rufani na wito wa kuanza kusikiliza mashauri Mahakama Kuu.

Changamoto nyingine ni kwa Watuhumiwa kubaki kwenye Vituo vya Polisi kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani. Viongozi hao wameeleza, kwa nyakati tofauti, namna hoja hizo zitakavyoshughulikiwa na nyingine tayari zimeshaanza kufanyiwa kazi na kutatuliwa.

Wakati wa kuhitimisha ziara hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha, alimshukuru Jaji Kiongozi kwa kuamua kuja Songea kuwatembelea na kuonesha njia ya namna ya kuzungumza na Watumishi, Wafungwa na Mahabusu.

Ametumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa Mahakama kwa kuja Songea na kuahidi yote ambayo Jaji Kiongozi ameyatoa kama ushauri na maelekezo watayafanyia kazi na kufanya kila linalowezekana ili kuyatimiza na kujenga imani ya watu kwa Mahakama.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Tunduru, Mhe. Dkt. Siyani amewahimiza kufanya kazi kwa bidii na kuweka utaratibu wa kujipima, kwani kutokufanya hivyo kunaweza kusababisha watu kutokuwa na imani na Mahakama.

“Vinavyowaondolea watu imani siyo utovu wa maadili pekee, hata msipotimiza wajibu ipasavyo. Kama watu wanakuja mahakamani na mashauri yanachukua muda mrefu, wanaweza kukata tamaa na kuona hakuna sababu ya kwenda mahakamani,” Jaji Kiongozi amesema.

Amesisitiza kuwa kila Mtumishi wa Mahakama anapaswa kuaminiwa na umma na mtaji wa Mahakama kuendelea kuaminiwa ni imani ya umma, kwani watu wasipokuwa na imani na Mahakama, hakutakuwa na sababu ya uwepo wake.

“Kila Mtumishi anapaswa kujua kuwa namna anavyotenda au kutimiza wajibu wake kunachangia watu kuwa na imani na Mahakama. Watu wasipokuwa na imani na Mahakama, hawataitumia. Uhalali wetu wa kuwepo mahakamani ni kwa sababu watu wanatuamini kwamba tunaweza kufanya kazi ya kutoa haki,” amesema.

Aidha, Jaji Kiongozi amewasihi Mahakimu kutumia nafazi waliyonayo kujenga imani ya Wananchi katika nyanja zote, ikiwemo kutoa haki mapema ipasavyo.

Halikadhalika, Mhe. Dkt. Siyani amewataka Watumishi wote wa Mahakama ya Tanzania kutambua maeneo ambayo Mahakama inalalamikiwa, kuchukua hatua na kuzifanyia kazi changamoto zote kwa ufasaha.

Kabla ya kuzungumza na Watumishi hao, Jaji Kiongozi alipokea taarifa ya utendaji iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Shughuli Mwampashe.

Katika taarifa yake, Mhe. Mwampashe ameeleza kuwa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Juni, 19 2026, Mahakama ya Wilaya ya Tunduru na Mahakama zake za Mwanzo zimesajili na pia kuamua mashauri mbalimbali.

Amesema kuwa kwa upande wa Mahakama ya Wilaya, mashauri yaliyobaki Desemba 2025 yalikuwa 13, yaliyopokelewa January 2026 hadi Juni 19, 2026 yalikuwa 65 na yaliyoa, yaliyosikilizwa kwa kipindi hicho ni 59 na mashauri yaliyobaki ni 19.

Katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo, hapakuwemo na mashauri yaliyobaki mwaka 2025, mashauri yaliyosajiliwa kuanzia Januari hadi June 19, 2026 yalikuwa 378, yaliyosikilizwa ni 353 na yaliyobaki ni 25.

Aidha, ameleeza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Januari hadi Juni 2026 kama kusimamia uharakishwaji na usikilizwaji wa mashauri kwa Mahakama wa Wilaya na Mwanzo, kufunga mashauri 44 ya mirathi na kupokea na kutuma barua na taarifa mbalimbali kwa njia ya Ofisi Mtandao (e-Office).

Ameeleza pia kuwa wanaendelea kusikiliza mashauri kwa njia ya Mtandao (Virtual Court), ikiunganisha Mikoa tofauti na kutoa elimu kwa Wadaawa kabla ya kuanza shughuli za Mahakama.

Katika ziara yake, Jaji Kiongozi aliambatana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha, Jaji wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Emmanuel Kawishe, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele na Mhe. Asha Waziri.

Wengine ni Mtendaji wa Mahakama Songea, Bw. Allan Mwela, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu. Mahakama za Wilaya Songea, Nyasa, Mbinga na Namtumbo na Watumishi wengine wa Mahakama Songea.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Tunduru (hawapo kwenye picha).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha, akizungumza kwenye kikao cha majumuisho ya ziara ya Jaji Kiongozi Songea. Kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa. Picha chini akiongea kwenye kikao hicho.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tunduru, Mhe. Shughuli Mwampashe akiwasilisha taarifa ya utendaji kwenye kikao hicho.

Sehemu ya Mahakimu Wafawidhi Mahakama za Wilaya wakiwa kwenye kikao hicho.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Tunduru (juu na chini) wakiwa kwenye kikao hicho cha majumuisho ya ziara ya Jaji Kiongozi.




Meza kuu inayoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, ikiwa kwenye picha ya pamoja. Picha chini ni makundi mbalimbali baada ya kikao cha majumuisho ya ziara ya Jaji Kiongozi.






Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akiwasili kwenye Gereza la Mahabusu na Wafungwa Tunduru.

Picha na Magoiga Mtatiro-Mahakama, Songea.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni