Na JAMES BUSANYA, Mahakama-Dodoma
Mtendaji Mkuu Mstaafu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amemshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kumuamini na kumpa nafasi ya kulitumikia Taifa kupitia nafasi ya Mtendaji Mkuu
wa Mahakama miaka
mitano iliyopita.
Prof. Ole Gabriel aliyasema hayo jana tarehe 24 Juni, 2026 Makao Makuu ya Mahakama Jijini Dodoma wakati wa Kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Antony Jingu na kumuaga Mtendaji Mkuu huyo aliyestaafu.
Alisema kuwa, uteuzi wake ni tukio ambalo hataweza kulisahau katika maisha yake kwa kuwa Rais alimuona kuwa miongoni mwa Watanzania waliostahili kupewa dhamana ya kuiongoza Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kipindi hicho.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu katika kipindi chote cha utumishi wangu Serikalini na Mahakamani,” alisema.
Aidha, amewashukuru Viongozi na Wajumbe wote wa Menejimenti ya Mahakama kwa
ushirikiano, ushauri na kujitolea kwao, akisema mchango wao umewezesha
kupatikana kwa mafanikio mbalimbali katika kipindi chake cha utumishi.
Ameishukuru pia familia yake hususan mkewe Bi. Devotha kwa ushirikiano aliompatia wakati wa utumishi wake.
Kwa namna ya pekee,
alimshukuru Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
pamoja na aliyekuwa
Jaji Kiongozi ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Eliezer Mbuki Feleshi, ambapo amesema alipojiunga na Mahakama, walimpokea
vizuri na kumpatia maarifa na uzoefu uliomuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi. Pia
alimpongeza mke, Bi. Devotha wake kwa uvumilivu, msaada na mchango mkubwa alioutoa katika
kipindi chote cha utumishi wake.
“Mhe. Jaji Mkuu, ingawa tumefanya kazi pamoja Mahakamani kwa
kipindi cha mwaka mmoja, lakini tumefahamiana kwa muda mrefu zaidi
kabla sijaja Mahakamani.
Ushauri na mchango wako katika masuala ya kisheria ulinisaidia sana hata
kipindi nilipokuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo,”
ameeleza Prof. Ole Gabriel.
Amebainisha kwamba, mafanikio yaliyopatikana
Mahakamani yamejengwa katika misingi ya ushirikiano mzuri kati ya Ofisi ya Jaji
Mkuu, Ofisi ya Jaji Kiongozi, Ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama, Ofisi ya
Mtendaji Mkuu wa Mahakama pamoja na Menejimenti nzima ya Mahakama.
Alisisitiza kuwa, ushirikiano na kuheshimiana kati ya Maofisa
wa Kada za Mahakama na wale wasio wa kada hizo umekuwa msingi muhimu wa
mafanikio ya Taasisi hiyo.
Katika hatua nyingine, Prof.
Ole Gabriel amempongeza Dkt. Jingu kwa kuteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu mpya wa
Mahakama ya Tanzania, huku akimshauri kutekeleza majukumu yake kwa bidii,
uadilifu na weledi.
Alisema kazi hiyo ni kubwa na
yenye matarajio makubwa kutoka kwa Watanzania, licha ya kuonekana ya kawaida
kwa mtazamo wa nje
lakini ukiingia ndani utaona uhalisia.
“Taasisi hii ina wataalamu
wazuri, mazingira bora ya kazi na watu wenye utayari wa kushirikiana.
Usitishike, fanya kazi kwa bidii na pale utakapohitaji ushauri sisi
tuliokutangulia tutakuwa tayari kukusaidia,” amesema.
Ameeleza kuwa, ana imani na
uwezo wa Dkt. Jingu kutokana na umahiri wake katika kazi na kujituma kwake,
akiongeza kuwa ataendelea kufuatilia maendeleo ya Mahakama hata baada ya
kustaafu na kusema kuwa Mahakama ikipiga hatua atafurahi na
ikikumbana na changamoto ataguswa kwa sababu amekuwa sehemu ya Taasisi hiyo
muhimu.
Akihitimisha hotuba yake,
Mtendaji Mkuu huyo mstaafu amemshukuru Jaji Mkuu, Mhe. George
Masaju, Viongozi, Menejimenti na Watumishi wote wa Mahakama kwa ushirikiano
waliompatia katika kipindi chote cha utumishi wake.
Kadhalika amesema kuwa,
ataendelea kuwa tayari kutoa ushauri, msaada na ushirikiano kwa Mahakama na
watumishi wake wakati wowote atakapohitajika.
Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa neno wakati wa Kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Antony Jingu na kumuaga Mtendaji Mkuu huyo aliyestaafu. Kikao hicho kilifanyika jana tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (kushoto) na Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) wakati wa Kikao maalum kilichofanyika jana tarehe 24 Juni, 2026 kwa ajili ya kumkaribirsha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Anthony Jingu na Kumuaga, Prof. Ole Gabriel ambaye amestaafu.









Hakuna maoni:
Chapisha Maoni