- Awataka Watumishi kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa weledi
Na FAUSTINE KAPAMA
na Noel Daud-Mahakama, Songea
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amewataka
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania kutoa huduma zinazoendana na ubora wa
miundombinu ambayo imejengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Mhe. Dkt. Siyani
ametoa wito huo leo tarehe 24 Juni, 2026 mjini Songea, alipokuwa anazungumza na
Watumishi wa Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya na
Mahakama za Mwanzo mjini Songea katika ziara yake ya kimahakama, kukagua
Mahakama na Magereza mkoani Ruvuma.
“Miundombinu hii
mipya michache tutakatoipata, itakayotutoa katika majengo ya zamani inatokana
na fedha ambazo Serikali inaiwezesha Mahakama kupitia mikopo kutoka Benki ya
Dunia na fedha za maendeleo ambazo Serikali inazileta. Miundombinu hii iendane
na ubora wa huduma zitakazokuwa zinatolewa,” amesema.
Jaji Kiongozi
ameagiza kuwa wale wote wanaokwenda kufanya kazi katika miunombinu hiyo, iwe
Songea au sehemu yoyote nchini, huduma wanazozitoa ziendane na ubora wa majengo
hayo.
Mhe. Dkt. Siyani
amebainisha kuwa fedha nyingi zimewekezwa kwenye miradi hiyo, hivyo haitakuwa
sawa kwa Watumishi kuchuku changamoto zao walizokuwa nazo miaka yote na kuzihamishia
kwenye majengo hayo.
“Uwekezaji mkubwa
uliofanyika Songea na maeneo mengine nchini hautakuwa na maana yoyote kama
huduma zetu zitakuwa za kiwango cha chini, kwa hiyo, nawakumbusha kuwa
tutaendelea kufanya kila linalowezekana kuboresha miundombinu,” Jaji Kiongozi
amesema.
Amewahimiza
Watumishi wa Mahakama Songea kwenda kujifunza kwa wenzao waliotangulia kama
Geita na Simiyu, ambao wameonesha mfano na hawajahamishia matatizo yao kwenye
majengo hayo mapya.
Jaji Kiongozi
amesema kuwa mwaka huu wa 2026 wameanzisha Mahakama nyingine tano, Lindi,
Katavi, Njuombe, Songwe na Singida na kote wamewaambia mambo kama hayo.
Mhe. Dkt. Siyani amewapongeza
Watumishi wa Mahakama mjini Songea kwa kazi nzuri wanaoifanya, kwani taarifa ya
utendaji iliyowasilishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala
Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha, imeonesha mafanikio makubwa yaliyofikiwa.
Kwenye taarifa
yake, Mhe. Karayemaha ameeleza kuwa kwa Mwaka 2025, Masjala Ndogo ya Songea ilibakiwa
na mashauri 250, yaliyosajiliwa kuanzia mwezi Januari hadi Juni 19, 2026 ni
mashauri 531, yaliyosikilizwa ni 485 na hadi kufikia Juni 19, 2026 idadi ya
mashauri yaliyobaki ni 296.
Akizungumzia upade
wa Mahakama Kuu, Jaji Mfawidhi ameeleza
kuwa mashauri yaliyobaki kwa mwaka 2025 ni 156, yaliyopokelewa Januari hadi Juni
ni 174, yaliyosikilizwa 150 na yaliyobaki ni 180.
Kati ya mashauri
180 yaliyobaki, amesema, yaliyopo mbele ya Majaji ni 155 na 15 yapo mbele ya
Naibu Msajili (mashauri ya kukaza hukumu saba, maombi ya gharama saba na maombi
ya kawaida shauri moja).
Akizungumzia upande
wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, Jaji Mfawidhi ameeleza kuwa kwa mwaka
2025, Mahakama hizo zilibakiwa na mashauri 94, kuanzia mwezi Januari 2026 hadi Juni
19, 2026 zimesajili mashauri 357, zimesikiliza 334 na zimebakiwa na mashauri
117.
Ameeleza pia kuwa Mahakama
za Mwanzo kwa mwaka 2025 hazikubakiwa na mashauri, kuanzia mwezi Januari 2026 hadi
Juni 19, 2062 zimesajili jumla ya mashauri 2,530, zimesikiliza 2, 305 na zimebakiwa
na mashauri 227.
Aidha, Jaji
Mfawidhi amebainisha baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kama kusimamia na
kuratibu uharakishwaji wa usikilizaji na umalizaji mashauri kwa wakati kwa
ngazi zote za Mahakam ana kutoa elimu kwa jamii kuhusu huduma za kimahakama.
Mengine ni kurejesha
huduma kwa Mahakama ambazo zilikuwa hazifanyi kazi kwa muda ambazo ni Mahakama
za Mwanzo Chiwanda, Lukumbule, Namasakata, Myangayanga, Magazini na Wabaki na kufanya
ukaguzi wa Mahakama katika ngazi zote na kufanya utatuzi kwa changamoto
zinazojitokeza.
Mafanikio mengine
ni kusikiliza mashauri 558 kwa njia ya Mkutano Mtandao, kuhakikisha upatikanaji
wa vitendea kazi, kufanya ukarabati wa majengo ya Mahakama mbili za Mwanzo Mfaranyaki
na Mpambano na kuwa na ushirikiano mzuri na Wadau.
Wakati huo huo,
Jaji Kiongozi amewakumbusha Watumishi wa Mahakama kuendelea
kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa weledi na kutoitia madoa Mahakama.
Mhe. Dkt. Siyani
ametoa wito huo alipokwa anazungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya
Namtumbo, kama sehemu ya ziara yake ya kimahakama, kutembelea Mahakama na
Magereza katika Mkoa wa Ruvuma.
Amewaambia Watumishi
wa Mahakama hiyo kuwa wanapaswa kuwa mfano kwa Watumishiwanaotoa huduma bora
kwani mazingira waliyonayo hayafanani na maeneo mengine katika Mkoa huo.
“Fanyeni kazi na
msiitie doa Mahakama yenu. Mnapswa katika mazingira yenu kuwa vinara katika
maboresho. Kuweni wabunifu ambao utaongeza tija kwenye utendaji wetu, msifanye
kazi kwa mazoea,” Mhe. Dkt. Siyani amesema.
Akiwa katika
Mahakama hiyo, Jaji Kiongozi pia alipokea taarifa ya utendaji iliyowasilishwa
na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Gloria Lwomile. Katika taarifa yake, Mhe. Lwomile
ameeleza kuwa Mahakama ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo Namtumbo kwa pamoja
zimezingatia umalizaji wa mashauri kwa wakati kulingana na ukomo wa muda.
“Ngazi zote za Mahakama
hazina mashauri ya muda mrefu. Tunao mkakati binafsi wa kumaliza mashauri
katika Wilaya ambapo; ukomo wa Mahakama ya Wilaya ni siku sitini na ukomo wa Mahakama
ya Mwanzo ni siku 45,” amesema.
Hakimu Mfawidhi
ameeleza pia kuwa usajili na uondoaji wa mashauri katika mfumo unatekelezwa
ipasavyo katika ngazi zote na mashauri ya mirathi pia yanaendelea kufungwa;
yaliyobaki bila kufungwa 2025 yapo 11 pekee.
“Utekelezaji wa
hukumu pia umezingatia na kusimamiwa vema. Kwa sasa tuna shauri moja tu la
utekelezaji wa hukumu ambalo linaendelea kusubiri utekelezaji. Shauri hili
limechelewa kutokana na kukosekana kwa mnunuzi,” amesema.
Katika ziara yake,
Jaji Kiongozi pia ametembelea Gereza la Songea na kukutana na Wafungwa na Mahabusu.
Baada ya kupokea taaraifa ha lai ya Gereza kutoka kwa Mkuu wa Gereza hilo,
Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Afande Robert Mabeja, Mhe. Dkt. Siyani alipokea
changamboto mbalimbali na kuzitolea ufafanuzi na ufumbuzi wa papo kwa papo.
Wafungwa na
Mahabusu hao wameonekana kufurahishwa na ujio wa Jaji Kiongozi na ujumbe wake
kwani wamepata nafasi ya kueleza kero zao kwa uwazi bila kuingiliwa na mtu
yoyote.
Aidha, Jaji
Kiongozi ametumia fursa hiyo kurudia wito wake kwa Wafungwa watakaobahatika
kutoka gerezani wawe raia wema, kwani kukaa kwao huko ni hasara kwao binafsi na
kwa Taifa kwa ujumla.
Katika ziara hiyo,
Jaji Kiongozi ameambatana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala
Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha, Jaji wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Emmanuel
Kawishe, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa na Naibu
Wasajili wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele na Mhe. Asha Waziri.
Wengine ni Mtendaji
wa Mahakama Songea, Bw. Allan Mwela, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu
Mfawizi na Wilaya Songea na Watumishi wengine wa Mahakama Songea.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni