Alhamisi, 25 Juni 2026

WAFUNGWA, MAHABUSU ISANGA DODOMA WAFURAHISHWA NA MABORESHO YA MAHAKAMA

Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama Kuu Dodoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, amefanya ziara ya kutembelea Gereza la Isanga Dodoma, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya za Mkoa wa Dodoma.

Ziara hiyo alianza tarehe 23 June 2026, ikiwa ni mara yake ya kwanza kutembelea Gereza hilo tangu ateuliwe kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Dodoma kutokea Mahakama Kuu Mbeya.

Akiwa katika Gereza hilo, Mhe. Tiganga alisomewa taarifa fupi kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Gereza la Isanga, Mrakibu Mwandamizi Juvenal Namwata,  ambaye aliipongeza Mahakama kwa kuendesha mashauri kwa wakati, jambo ambalo limepunguza msongamano mkubwa wa Wafungwa.

Akiwa ndani ya Gereza hilo, Jaji Mfawidhi alipata fursa ya kukutana na Wafungwa na Mahabusu kwa upande wa wanaume na wanawake, ambao waliwasilisha risala zao na kusikiliza hoja mbalimbali, changamoto na maswali ambayo baadhi yalijibiwa palepale na changamoto zingine alielekeza kwa wasaidizi wake zitatuliwa mara moja.

Kadhalika, Mhe. Tiganga aliwasisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Wadau wa haki jinai ili kuweza kutoa haki kwa Wananchi, tena kwa wakati sahihi.

Kwa upande wake, Afande Namwata   alitoa shukrani zake kwa ujio wa ziara hiyo kwa kuwa umekuwa na tija kubwa kwao na kuimarisha ushirikiano.

Katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi aliambatana na Viongozi wa Mahakama Kuu Dodoma na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, akiwemo Naibu Msajili, Mhe. Upendo Ngitiri, Mhe Zabibu Mpangule na Mtendaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Bw. Bedson Mariba.

Wengine ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Dodoma, Mhe. Thurstone Kombe, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Bahi, Mhe. Christina Mlilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Dodoma, Mhe. Ntuli Mwakaselo pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Makole, Mhe. Winnie Kayombo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga (wa saba kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa haki jinai wakati alipotembelea Gereza Kuu Isanga Dodoma tarehe 23 Juni 2026.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga (wa kwanza kutoka kulia) akiteta kitu na Mkuu wa Gereza la Isanga Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Magereza, George Wambura baada ya kuwasili gerezani hapo .

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Songea.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni