Na HABIBA MBARUKU- Mahakama, Dodoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amewataka Naibu Wasajili
wapya 31 kutobweteka na kutowaangusha Viongozi waliowaamini kutekeleza jukumu
la utoaji haki kupitia nafasi hizo.
Mhe. Siyani ameyasema
hayo baada ya kuwaapisha Naibu Wasajili hao leo tarehe 17 Juni, 2026 katika
Ukumbi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma.
“Sisi tunaofanya kazi
katika Mahakama ya Tanznaia ni Watumishi wa Serikali. Nafasi tunazozipata, ziwe
ni nafasi za ajira au nafasi za uongozi kama hizi, ni nafasi ambazo wenzetu
wengi zaidi ya milioni 60 hawajabahatika kuzipata, ni nafasi ambazo zinabeba
dhamana kubwa, kwa hiyo nitumie nafasi hii kuwasihi sana kutobweteka,”
amesisitiza Jaji Kiongozi.
Ameongeza kuwa Naibu
Wasajili wa Mahakama ndio injini, moyo na uhai wa Mahakama, hivyo
watakapokwenda katika maeneo ambayo watapangiwa watambue kuwa wamebeba
matarajio ya wale waliowaamini, kwa niaba ya Watanzania wote.
Amesema kuwa katika
Taasisi, zipo changamoto ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu na kwamba wao
wanatarajiwa kwenda kuzifanyia kazi, huku akibainisha moja ya changamoto
inayoikabili Mahakama ni watu kutoridhika na huduma za Mahakama, licha ya uwepo
wa takwimu zinazoonesha kuridhika kwa Wananchi, hivyo wanapaswa kuwajibika bila
kubweteshwa na takwimu.
Katika hatua nyingine, Mhe.
Dkt. Siyani amewataka Naibu Wasajili wapya kufanya kazi bila hofu, huku
wakitenda haki, kwa kuzingatia Katiba, Sheria mbalimbali, mila na desturi
pamoja na maelekezo ya Viongozi. Amewaeleza kuwa wasiwe na hofu katika
kutekeleza majukumu yao kwa sababu wanatarajiwa kwenda kuwahudumia watu, na wanapaswa
kuwa na hofu na Mungu pekee ambaye wameapa kwake.
“Msiende kupeleka hofu
zenu kazini, mnatarajiwa kwenda kuwahudumia watu na mkiwa na weledi hakuna
sababu ya kuwa na hofu, timizeni majukumu yenu vile inavyotarajiwa, hofu
itawafanya mkosee, hofu yenu iwe kwa Mungu ambaye mmeapa kwake, msipoweza
kudhibiti hali hiyo mtakosea. Katika zama tulizonazo haitajariwi Maaoisa wenye
hadhi yenu kufanya makosa yasiyotarajiwa….mkachape kazi,” amesisitiza Jaji
Kiongozi.
Ameongeza kuwa miezi sita
ijayo itakuwa miezi ya matazamio, hivyo wakienda kubweteka watakosa sifa za
kuendelea kuwa Naibu Wasajili kwa sababu uvivu na ukosefu wa weledi ni vitu
ambavyo havina nafasi ya kuvumiliwa katika nyakati za sasa na kuwa kila mtu
atapimwa kwa haki juu ya namna anavyofanya kazi.
Jaji Kiongozi amewatakiwa
kila la heri, huku akiwakumbusha kuiishi kauli mbiu ya Mahakama inayosema, “Uadilifu,
Weledi na Uwajibikaji,” akieleza kuwa mambo hayo matatu ndio masingi wa
utendaji ulio imara.
Amesema kwamba
atakayekosa uadilifu, weledi na kushindwa kuwajibika atakuwa amepoteza sifa ya
kuwa Naibu Msajili, hivyo wawe kundi la mageuzi na kundi ambalo litaleta
taswira ya kuwa hakukuwa na makosa kwenye kuweka imani kwao.
Sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Tume ya Utumishi wakiwa kwenye uapisho huo (juu na chini).










Hakuna maoni:
Chapisha Maoni