·
Jaji Mkuu awataka Naibu Wasajili
wapya kuwajibika ipasavyo
·
Awataka kusimamia ipasavyo
utekelezaji wa hukumu
·
Jaji Mkuu awataka kuimarisha
ushirikiano na watumishi walio chini yao
·
Awataka pia kusimamia Masjala Ndogo
za Mahakama Rufaa na kuandaa vema kumbukumbu za rufaa
Na
MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Naibu
Wasajili wapya 31 kuzingatia maslahi ya umma na ya Taifa katika kulinda,
kutunza heshima, mamlaka na uhuru wa Mahakama kama unavyotajwa katika Ibara ya
30(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe.
Masaju ameyasema hayo leo tarehe 17 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa
Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na Naibu
Wasajili wapya 31 walioapishwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.
“Tunapotambua
kwamba mnazo sifa za kuwa Viongozi na Tume tukawateua nendeni mziishi hizo
sifa, lakini pia tambueni tunaishi wakati gani, ni wakati ambao unasisitizwa
sana uwajibikaji na hatuwezi kuwa tu tunafurahia kuteuliwa. Kila nafasi ya
uongozi na kila nafasi ya mafanikio inakuja na wajibu mkubwa kwa mhusika,”
amesema Jaji Mkuu.
Amewataka
Naibu Wasajili hao kutambua kuwa, Mahakama ya Tanzania inawategemea kwa kuwa wao
ni kada muhimu na ndio Meneja na Injini ya shughuli za kila siku za Mahakama
katika ngazi zote kuanzia Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama za
Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
“Ingawa
mtapatiwa mafunzo elekezi, matarajio ni kwamba tayari mna ufahamu wa majukumu
yenu kutokana na uzoefu mlio nao hususan kwa wale ambao wamewahi kukaimu nafasi
hizi lakini hata wale waliokuwa Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi ngazi ya
Mkoa, ngazi ya Wilaya na mambo ni yaleyale kwa mfano masuala ya ‘execution’
kama Naibu Wasajili ninyi ndio wapishi au waratibu Wakuu wa shughuli za kimahakama,
ninyi ni Mameneja na Injini ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama,”
amesisitiza Jaji Mkuu.
Kadhalika
amewataka Wasajili hao wa Mahakama kusoma sheria mbalimbali zinazoelezea
majukumu yao ili wawe katika nafasi nzuri ya kutekeleza majukumu yao ya kila
siku ipasavyo huku akisema kuwa, “jitambueni na muwajibike kama Viongozi katika
maeneo yenu ya kazi, jitoleeni kwa moyo wote ili kuleta ufanisi katika Vituo
vyenu na kwa Mahakama kwa ujumla, kuweni na ari, ubunifu na utayari wa kutatua
changamoto zinazojitokeza katika maeneo yenu ya kazi, leteni Makao Makuu ya
Mahakama changamoto zilizo nje ya uwezo wenu badala ya kusubiri vikao ndipo
muwasilishe hizo changamoto.”
Kadhalika,
Mhe. Masaju amewataka Naibu Wasajili hao kuimarisha ushirikiano na Watumishi wa
Kada nyingine waliopo chini yao. “Kwenye ngazi ya Mkoa au Kanda wapo Watendaji
wa Mahakama lazima muwape ushirikiano ipasavyo, tumegawana majukumu ninyi
mnashughulika na shughuli za kimahakama, wenzetu wanashughulika na shughuli za
kiutawala lakini ushirikiano ni jambo la lazima, kuhusu suala ya kutunishiana
misuli lazima mshirikiane, mheshimiane kwa sababu mafanikio yetu yanategemea
tunashirikiana namna gani,” amesema Jaji Mkuu.
Amesema
kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho amekaa Mahakamani amebaini kuwa,
watumishi wanawasikiliza Viongozi lakini kumekuwa na changamoto ya kutokuchukua
hatua wakidhani mambo hayo yanatekelezwa na waliopo Makao Makuu pekee wakidhani
kuwa wao hawahusiki, hivyo amewataka kubadilika na Uongozi watawapima ipasavyo.
Aidha,
amewataka Naibu Wasajili hao kutumia vizuri kipindi cha miezi sita ya uangalizi
(Probation) kwa kuwajibika, na kwamba wao kama Viongozi watakuwa wanawafuatilia
kwa karibu kwa sababu nia yao ni njema hawawaangalii kwa karibu ili kuwaadhibu
bali waendelee kupanda katika vyeo vya juu zaidi.
“Sasa
hivi kuna nafasi zipo kwa ajili ya Majaji wa Mahakama Kuu, tunataka kadri
tunavyostaafu na wengine wanavyopanda kwenda Mahakama ya Rufani, wengine
wanaziba zile nafasi, ninyi mmeshaaminiwa na tungependa hao Majaji watokane na
ninyi, na ndio maana tunasema kwamba ile Mahakama ya Mkoa itakapokuwa
imeanzishwa itakuwa ndio Kituo cha Mafunzo cha kuwaandaa ninyi kuteuliwa kuwa
Majaji na mimi kitu ninachokizingatia sana ni uadilifu na uwezo wa kumudu
majukumu kwa ufanisi ipasavyo, kwahiyo tutakapokuwa tunawaangalia kwa namna ya
kuwalea ili kuwaandaa kushika majukumu makubwa
zaidi sio kwa maana ya kutaka kuwaadhibu,” ameeleza Mhe. Masaju.
Ameongeza
kuwa, moja ya majukumu ya Naibu Wasajili ni usimamizi wa masjala na hilo ndilo
jukumu kubwa, hivyo wao kama injini ya Mahakama na meneja wa masjala wanapaswa
kufahamu vema mwenendo wa masjala zilizopo chini ya usimamizi wao.
Katika
hatua nyingine, Jaji Mkuu amewataka Naibu Wasajili hao kudhibiti na kupunguza
mlundikano wa mashauri katika Masjala zao huku akiwataka kushughulikia ipasavyo
mashauri ya mirathi na mashauri ya watu wengine dhaifu katika jamii (vulnerable
groups) yanashughulikiwa na kuhitimishwa mapema ipasavyo na kwamba zipo kanuni
zilizotungwa na Jaji Mkuu kwa ajili hiyo.
“Na
ni kwa sababu hiyo nimewasomea Zaburi ya 82:2-4, kwa hiyo sio suala la Zaburi
tu, hata sisi tumetambua; zipo kanuni zilitungwa na Jaji Mkuu kwa ajili ya
kuzingatia makundi hayo, hivyo mashauri ya mirathi na mengine ya aina hiyo
yanayohusu watoto, masuala ya ndoa na masuala mengine, mmeshika hapa misaafu
wengine Biblia, mimi ningependa kipimo chenu kiwe ni kwa namna gani mnamtendeka
haki huyu mtu ambaye ni maskini, wajane, watoto na hasa wanaochukuliwa kuwa
dhaifu kutokana na hali yao katika jamii. Haina maana tutawapendelea hapana
lakini tusiwadhulumu haki zao kwa sababu ya hali zao,” amesema.
Mhe.
Masaju ametoa rai kwa Wasajili hao kuendelea kuwa wanyenyekevu, huku akisema
kuwa, kipimo cha mtu kipo katika mambo mawili, mosi anapopata mali na anapopata
Madaraka.
Sambamba
na hilo, Jaji Mkuu amewataka Naibu Wasajili hao kuwasimamia vizuri Mahakimu wa Mahakama
za Wilaya na kuhakikisha pia wao nao wanawasimamia vizuri Mahakimu wa Mahakama
za Mwanzo.
“Tutatengeneza
vigezo vya kuwapima kwenye miezi hii sita, na ni pamoja na kigezo hiki cha ni
kwa namna gani mnazisimamia hizo masjala zilizopo chini yenu, kuna ufanisi
kiasi gani kwahiyo haya yaangalieni sana.
Aidha,
Mhe. Masaju amewataka Naibu Wasajili hao kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa
shughuli za kimahakama ili kubaini na kuondoa vikwazo vinavyochelewesha
usikilizaji wa mashauri.
“Kama
Majaji wenu huko watakuwa na changamoto, tujulisheni lakini hatutaki tushindwe
kufanya vizuri kule kwenye Kanda kwa sababu tu ya udhaifu wetu sisi yaani ninyi
Wasajili, tekeleza wajibu wako ya Jaji tutayajua tu sisi huku lakini wewe ukiwa
umetekeleza wajibu wako. Chukueni hatua haraka pale panapotokea mkwamo katika
usikilizaji wa mashauri, lizingatieni sana hili,” amesema.
Vilevile,
Jaji Mkuu amesema, usimamizi wa uandaaji wa kumbukumbu za rufaa ni moja ya
majukumu ya Naibu Wasajili na hasa rufaa zinazokuja Mahakama ya Rufani, hivyo Wasajili
wanaofanya kazi katika Mahakama Kuu watambue kuwa Masjala Ndogo za Mahakama ya
Rufani zilizopo katika majengo ya Mahakama Kuu ni za kwao na hivyo majukumu
yanayopaswa kutekelezwa katika Masjala Ndogo hzio yanawahusu moja kwa moja.
“Baadhi
ya Wasajili wanajiona kama sio wajibu wao kuandaa kumbukumbu za rufaa, kwahiyo
hawajishughulishi kwa ufanisi ipasavyo na uandaaji wa hizi rufaa, sasa
zinaandaliwa kwa namna ambayo wakati fulani hazikidhi kile kilichotegemewa na
matokeo yake inasababisha haki kuchelewa kwahiyo hatutaki kuliendekeza na
hatutavumilia ucheleweshaji wa kumbukumbu,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Ameongeza kuwa, Mahakama itachukua hatua ipasavyo, “na hivi ninavyozungumza nipo katika hatua za kukamilisha marekebisho ya kanuni, tutaweka na muda (timeline) unapaswa kuwa umekamilisha kuandaa kumbukumbu za rufaa na ziwe zimeandaliwa kwa ufanisi ipasavyo zisije zikachelewesha haki kutendeka, hatutavumilia ucheleweshaji wa kumbukumbu za rufaa” amesema Mhe. Masaju.
Vilevile, amewataka Wasajili hao kusimamia ipasavyo utekelezaji wa hukumu za Mahakama kwakuwa eneo hilo lina changamoto huku akisisitiza kwa kusema kuwa, “kuweni makini, na waadilifu katika utekelezaji wa hukumu.”
Aidha ameeleza kuwa, pamoja na kuwepo kwa vitendea kazi vya kawaida kama vile viti, meza majengo na kompyuta vipo vitendea kazi vingine ambavyo ni uwajibikaji kama unavyoelezewa katika Ibara ya 25 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, uadilifu kama unavyoelezwa katika Sheria za Utumishi wa Umma, kuwiwa kuona haki inatendeka na kuitenda ipasavyo, uwezo wa kumudu utendaji kazi wa majukumu ya kila siku, kujituma, ubunifu katika kutatua changamoto, kuzingatia maslahi ya Umma na Taifa pamoja na kuzingatia ukweli na uhalisia bila kupendelea upande wowote.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amesema kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kuwa na mchango mkubwa na wa pekee katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ambayo inasisitiza kuhusu utawala bora na amani ya jamii, Naibu Wasajili hao watambue kuwa taifa haliwezi uwa na na maendeleo bila kuwa na amani hivyo wanapaswa Kutenda wakizingatia utawala wa sheria kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile Mhe. Masaju amewataka Naibu Wasajili hao kuendelea kuwaheshimu wake na waume zao bila kujali dhamana na cheo walichokipata “endeleeni kuwa waadilifu kwa wenza wenu, msiwadharau wenza wenu kwa ajili ya vyeo mlivyovipata” amesisitiza Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Naibu Wasajili wapya leo tarehe 17 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama mara baada ya Wasajili hao kuapishwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.
Naibu Wasajili wapya walioapishwa leo tarehe 17 Juni, 2026 na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani wakifuatilia kwa umakini hotuba ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha).


























Hakuna maoni:
Chapisha Maoni