Jumatano, 17 Juni 2026

JAJI KISANYA AKABIDHIWA RASMI OFISI MASJALA NDOGO MWANZA

Na. REHEMA AWET – Mahakama, Mwanza

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Mwanza imeingia katika awamu mpya ya Uongozi leo tarehe 17 Juni, 2026, baada ya hafla ya makabidhiano ya Ofisi ya Jaji Mfawidhi kufanyika.

Hafla hiyo iliyofanyika katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi Masjala Ndogo ya Mwanza, ilishuhudiwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Dkt. Ntemi Kilekamajenga akikabidhi rasmi kijiti cha uongozi kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ephery Kisanya.

Makabidhiano hayo yalijikita katika kukabidhi majukumu ya kiutawala, nyaraka mbalimbali za ofisi, na taarifa muhimu za utendaji kazi, zote zikiwa na lengo la kuhakikisha mwendelezo wa utoaji wa huduma za kimahakama na usimamizi wa shughuli za Mahakama katika Masjala Ndogo hiyo ya Mwanza.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Dkt. Ntemi Kilekamajenga alimpongeza Jaji Ephery Kisanya kwa kukabidhiwa majukumu hayo na kumtakia mafanikio katika utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Jaji Ephery Kisanya aliahidi kuendesha ofisi hiyo kwa weledi, kuendeleza ushirikiano baina ya wafanyakazi, na kuimarisha upatikanaji wa huduma za haki kwa wananchi wa Masjala hiyo ya Mwanza.

Makabidhiano hayo yanaashiria mwanzo wa awamu mpya ya uongozi katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mwanza, huku yakisisitiza dhamira ya kuendeleza ufanisi, uwazi na ubora katika utoaji wa huduma za Mahakama kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Mwanza ambaye amehama Kituo Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga (kushoto) akimkabidi Ofisi Jaji Mfawidhi Mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Mwanza Mhe. Ephery Kisanya (kulia).

Jaji Mfawidhi Mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Mwanza Mhe. Ephery Kisanya akisaini Kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili ofisini Masjala Ndogo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni